Mgogoro wa kugombania shimo la madini eneo la mlima Igae katika Kijiji cha Suguta Wilaya ya Kongwa jijini Dodoma lenye leseni namba PML 0193DOM inayomilikiwa na kikundi cha Hapa Kazi Tu umetatuliwa, anaripoti Issa Mtuwa (WM) Kongwa.
Naibu Waziri wa Madini, Prof. Shukrani Manya akitoka kukagua eneo la Mgodi wa Igae unaomilikiwa na wachimbaji wadogo wilayani Kongwa jijini Dodoma jana. Prof. Manya alifanikiwa kutatua mgogoro ambao ulikuwa umedumu kwa muda mrefu mgodini hapo. (Picha na Issa Mtuwa-WM).
Hatua hiyo imefikiwa baada ya mgogoro huo kutawaliwa na hali ya vuta nikuvute, hivyo kupelekea hali ya uvunjaji wa amani baina ya Colyn Mallya, Kimaro na Kikundi cha Hapa Kazi Tu wote wakitaka kuchimba bila utaratibu na kupelekea kutokuelewana.
Utatuzi huo umefanyika leo Desemba 15, 2020 mara baada ya ziara ya Naibu Waziri wa Madini, Prof. Shukrani Manya kutembelea eneo la mgodi wa Mlima Igae huku akisisitiza kuwa,ulipaji wa tozo ya Serikali na uuzaji wa madini kwenye masoko rasmi ni jambo muhimu.
Kabla ya kutatua mgogoro huo, Naibu Waziri ametoa nafasi ya kusikiliza kila upande wa mgogoro huo ili kupata picha kamili.
Aidha, baada ya kuwasikiliza mgogoro huo umetatuliwa kwa kutoa haki kwa wote, wachimbaji na wafadhili,Colyn Mallya ambaye amepewe kuchimba miezi mitatu kisha atapewa Kimaro miezi mitatu baada ya hapo ataachia mgodi kwa kikundi cha Hapa Kazi Tu waendelee kuchimba.
Kwa upande wake, Colyn Mallya amesema, amekubaliana na maamuzi hayo ili aendelee kuchimba kwa mujibu wa makubaliano, huku mwakilishi wa Kimaro akikubaliana na maamuzi hayo ili uchimbaji uwe wa amani.
Naibu Waziri wa Madini, Prof. Shukrani Manya akitoa maelekezo kwa wachimbaji wadogo kwenye mgodi wa Igae wilayani Kongwa leo Desemba 15, 2020. (Picha na Issa Mtuwa-WM).
Wakati huo huo, Yusto Chalo ambaye ni Mwenyekiti wa Kikundi cha Hapa Kazi Tu amekubali kwa niaba ya wanachama wake namna Naibu Waziri alivyotatua mgogoro huo.
Amesema, Naibu Waziri amezingatia maslahi yaa kila mtu na kwamba, "wote huwa tunategemea hapa.
Huu utatuzi nimeupenda, kila mtu amepewa haki na lazima kila mtu aridhike na umeona kila mtu yuko sawa kama ikitokea mtu akabadilika huyo atakuwa ana jambo lake,”amesema Yusto.
Akitoa taarifa mbele ya Naibu Waziri katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Afisa Madini Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Nachagwa Marwa amesema, baadhi ya migogoro iliyopo imeibuka mara baada wamiliki wa leseni Kikundi cha Hapa Kazi Tu kuwalalamikia baadhi ya wafadhili ambao wamekuwa wakifanya kazi za uchimbaji kwenye eneo hilo kwa kuwarubuni baadhi ya wanachama wa kikundi bila kuushirikisha uongozi wa kikundi.