NA FRESHA KINASA
Wajumbe Saba wa Prof. Wakuru Magige wametembelea Kituo cha Nyumba Salama Kiabakari Wilaya ya Butiama mkoani Mara kinachohudumia wasichana waliokimbia ukeketaji na ndoa za utotoni kutoka maeneo ya Mkoa wa Mara na kutoa vyakula kwa ajili ya Sikukuu ya Krismas, ambapo wamepongeza juhudi kubwa zinazofanywa na kituo hicho ikiwemo kuwapa hifadhi na kuwahudumia wasichana kituoni hapo.
Wajumbe wa Prof. Magige wakikabidhi misaada ya vyakula kwa viongozi wa Nyumba Salama kwa ajili ya Sikukuu ya Krismas itakayofanyika Desemba 25, 2020. (Picha na Diramakini).
Wajumbe hao wameongozwa na Neema Bisofu Wambura leo Desemba 24, 2020 Katibu wa Umoja wa Kinamama wa Chama Cha Mapinduzi Tawi la Nyamisisye ambaye pia ni Mama wa Prof.Magige ambapo amesema lengo la kutoa msaada huo ni kuwawezesha washerehekee sikukuu ya Krismas kwa furaha, amani na upendo.
Misaada iliyotolewa ni pamoja na kilo 100 za Mchele, Mbuzi, mfuko wa Sabuni za Unga, sabuni za mche, ndoo ya mafuta ya kupikia pamoja na kreti nne za soda.
"Prof.Magige ameomba mpokee zawadi hii kipindi hiki cha sikukuu na pia anaomba watoto wote kituoni hapa msome kwa bidii kwa kutanguliza nidhamu bidii katika kufikia malengo yenu, anatambua kazi kubwa zinazofanywa na Shirika la Hope for Girls and Women Tanzania chini ya Mkurugenzi wake Rhobi Samwelly kutetea haki za watoto wa kike, wanawake na kuwapa hifadhi wanaokimbia ukatili hasa ukeketaji pamoja na kuwaendeleza kimasomo,"amesema.
Kwa upande Wake Lucas Kichonge Katibu Mwenezi CCM Kata ya Kukirango ambaye pia ni Katibu wa Wafugaji Wilaya ya Butiama amewaomba wasichana hao kuendelea kusoma kwa bidii na kumtanguliza Mbele Mungu katika maisha yao, huku akiahidi pia kushirikiana na Shirika hilo kupambana na ukatili.
Akitoa taarifa ya kituo cha Nyumba Salama Kiabakari Mkuu wa Kituo hicho, Suzana Denis amesema kituo kilianza mwaka 2017na kimekuwa kikipokea watoto wa kike waliokimbia ukeketaji na ndoa za utotoni na pia kimekuwa kikiwaendeleza katika mafunzo ya ufundi, ujasiriamali na kuwaendeleza kimasomo ikiwemo shule za msingi na sekondari ambao hukakatiliwa na wazazi wao ili wafikie ndoto zao.
Mwakilishi mkuu wa timu ya Wajumbe Saba wa Prof. Wakuru Magige, Neema Wambura akizungumza wakati wa kukabidhiwa misaada ya vyakula kwa wasichana wa Nyumba Salama kinachomilikiwa na Shirika la HGWT waliokaa mbele Kiabakari Butiama walipotembea leo Desemba 24, 2020. (Picha na Diramakini).
"Tumekuwa tukiwajenga pia kisaikolojia wajione wanathamani kubwa katika jamii na kuwarejeshea matumaini yao, na pia tunaendelea kufanya kazi bega kwa bega na Serikali katika kuhakikisha haki za watoto wa kike zinalindwa na kuheshimiwa kwa mujibu wa sheria za nchi,"amesema.
Kwa upande wake Msaidizi wa Mkurugenzi wa shirika hilo, Amony Chakushemeire ameshukuru msaada huo na kupongeza kwamba utawafaa sana wasichana hao kipindi hiki cha sikukuu na amesema mpaka sasa vituo vyote viwili kikiwemo cha Nyumba Salama cha Kiabakari na Nyumba ya Matumaini Mugumu Serengeti vimepokea jumla ya watoto wa kike wapya 210 waliokimbia ukeketaji msimu huu, huku jumla kuu katika vituo vyote watoto wanaohudumiwa wakiwa ni 333.
Wasichana wa Nyumba Salama Kiabakari Butiama wakiimba. (Picha na Diramakini).
Chakushemeire ametumia fursa hiyo, kuwaomba wananchi kusimama kidete kupinga ukatili wa kijinsia kwani vitendo hivyo vinaathari kubwa kwao ikiwemo kuwafanya wakatize masomo yao na wengine kuozwa katika umri mdogo baada ya kukeketwa kwa ajili ya kujipatia mali pamoja na madhara mengine ikiwemo kutokwa damu nyingi wakati wa kukeketwa, hatari ya kupata magonjwa ya maambukizo ikiwemo UKIMWI.
"Sasa hivi kuna ukeketaji wa mbali, mtoto anawezesha kusafirishwa akaenda kukeketwa eneo jingine, hii ni hatari sana kwa watoto ambao ni tegemeo la siku za usoni kufanyiwa ukatili huo lazima kila mmoja wetu asimame kwa dhati kupambana na vitendo hivyo ambavyo pia nikinyume cha haki za binadamu na sheria zetu za nchi,"amesema Chakushemeire.
Ameongeza kuwa, shirika hilo limekuwa likichukua mzigo wa kuwasomesha mabinti wanaokataliwa kupokewa na wazazi wao baada ya msimu wa ukeketaji kuisha ambao hufanyika mwezi Desemba.
Wasichana wa Nyumba Salama Kiabakari Butiama wakiwa wamekaa wakisikiliza jambo. (Picha na Diramakini).
Naye Royce Muga ambaye ni Mwenyekiti wa Huduma za Jamii Mazingira na Afya Kijiji Cha Nyamisisye amelipongeza Shirika la Hope for Girls and Women Tanzanaia kwa juhudi kubwa zinazofanya kuwahudumia wasichana hao, huku akiwataka wazazi na walezi kuwa na uchungu na watoto wao na waachane na tabia ya kuwafanyia vitendo vya ukatili ambapo pia ameliomba shirika hilo kwa Mungu lizidi kufanya kazi hiyo bila kuchoka.
"Muendelee kuwasaidia hawa watoto bila kuchoka, kazi yenu ina malipo makubwa sana kwa Mungu. Nimefurahishwa sana na kazi nzuri ya Rhobi Samwelly kuamua kujitolea kwa dhati kuwasaidia watoto hawa tutazidi kumuombea katika juhudi hizi na kumuunga mkono kwa dhati,"amesema.
Tags
Habari