Rais Dkt.Mwinyi aahidi ushirikiano kwa dini zote, Kanisa la TAG lampongeza

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameupongeza uongozi wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) kwa kuendelea kuhubiri amani na kuliombea Taifa wakati wa uchaguzi, kabla na baada uchaguzi, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akisalimiana na Askofu Mkuu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), Dkt.Barnanas Weston Mtokambali alipofika Ikulu jijini Zanzibar kwa mazungumzo na kutoa pongezi zake kwa Rais, kulia kwa Askofu ni Askofu wa Jimbo la Zanzibar,Dikson Kaganga mazungumzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar Desemba 11,2020. (Picha zote na Ikulu).

Rais Dkt.Hussein ameyasema hayo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa kanisa hilo ukiongozwa na Askofu Mkuu wa Tanzania, Barnanas Weston Mtokambali akiwa amefuatana na Askofu wa Jimbo la Zanzibar, Dikson Kaganga, uliofika Ikulu kwa ajili ya kumpongeza baada ya kushinda uchaguzi wa mwaka huu.

Katika maelezo yake, Rais Dkt. Hussein ametoa shukurani kwa uongozi huo kwa ujio wao sambamba na pongezi na maneno ya hekima waliyayatoa kwa Rais.

Rais Dkt.Hussein ametoa pongezi kwa uongozi huo wa Kanisa la TAG kwa ushirikiano uliotoa kanisa hilo katika kipindi chote cha kabla, wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu 2020 katika kuliombea amani Taifa.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Askofu Mkuu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God, Dkt.Barnanas Weston Mtokambali (kulia kwa Rais) akiwa na Askofu wa Jimbo la Zanzibar,Dikson D.Kaganga, walipofika Ikulu Zanzibar kwa mazungumzo.

Amesema kuwa, katika kipindi cha kampeni aliweza kukutana na waumini wa dini ya Kikristo na wa madhehebu mbalimbali na kuzungumza nao ambapo pia na wao walieleza changamoto walizonazo ambapo aliahidi kuzifanyia kazi.

Aidha, Rais Dkt.Hussein Mwinyi ametoa shukurani kwa kanisa hilo kwa kuiunga mkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kusema kwamba Serikali anayoiongoza itashirikiana na kanisa hilo kwa kuthamini huduma inazozitoa kwani mbali ya huduma za kiroho pia, limekuwa likichangia katika sekta ya afya, elimu na maji na nyinginezo.

Amesema kuwa, maombi yote ya wananchi yameweza kukubaliwa na Mwenyezi Mungu na hivi sasa tayari kuna maridhiano ambapo lengo lake ni kuondoa kasoro katika kada za kisiasa hivyo, aliwanasihi waumini wote kuendelea kuliombea Taifa.

Rais Dkt. Hussein amempongeza Askofu Dk. Barnanas Weston Mtokambali, kwa nafasi yake ya uongozi aliokuwa nayo kwa Tanzania na pia kuwa kiongozi mkuu wa Makanisa yote 48 ya TAG barani Afrika, Mjumbe wa Halmashauri ya Kanisa hilo katika makanisa 150 duniani na kueleza kuwa yeye akiwa Rais yuko tayari kushirikiana nae na milango yake iko wazi.

Mapema Askofu Dkt. Barnanas Weston Mtokambali amempongeza Rais Dkt. Hussein Mwinyi kwa niaba ya Maaskofu wote, waumini na viongozi wengine wa kanisa hilo kwa ushindi wa kishindo alioupata katika uchaguzi Mkuu uliofanyika mwaka huu 2020.

Katika maelezo yake amemueleza historia ya kanisa hilo ambalo lina majimbo 71 hapa nchini likiwemo Jimbo la Zanzibar na kueleza kuwa kanisa hilo lilianza rasmi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnamo mwaka 1927 na kuingia Zanzibar mwaka 1929 na mwaka 1939 lilipata usajili rasmi ambapo tayari limeshatimiza miaka 81.Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akimsikiliza Askofu Mkuu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God, Dkt.Barnanas Weston Mtokambali, alipofika Ikulu jijini Zanzibar kwa mazungumzo na kumpongeza. 

Askofu Dkt. Mtokambali amempongeza Rais Dkt. Hussein Mwinyi kwa kuonesha ukaribu mkubwa kwa madhehebu mbalimbali ya dini ya Kikristo wakati wa kampeni na kuzipongeza hotuba zake alizokuwa akizitoa ambazo zimewapa mwanga mkubwa waumini hao na kusisitiza kuwa licha ya uchache wao, lakini wamekuwa wakiishi salama hapa Zanzibar.

Kiongozi huyo pia amepongeza uteuzi alioufanya Rais Dkt.Mwinyi wa Mwakilishi wa Baraza la Wawakilishi aliyetoka katika dini ya Kikristo, Anna Athanas Paul ambaye alisema anatoka katika kanisa la TAG.

Aidha, amesema kuwa kanisa lao hilo lina sera tatu ambapo ya kwanza ni ya kiroho, ya pili ni kuendeleza utume wa Kikristo na ya tatu ni kushiriki katika shughuli mbalimbali za maendeleo ambapo kwa upande wa Zanzibar wameweza kushirikiana vyema na Serikali zilizopita na kuahidi kushirikiana na Serikali hii ya Awamu ya Nane.

Amesema kuwa, kanisa hilo limekuwa likitoa msaada wa kuchimba visima, huduma za elimu na za afya Tanzania Bara na Zanzibar ambapo tayari kwa Zanzibar wana shule tatu za Kiingereza na wanatarajia kujenga moja huko kisiwani Pemba.

Sambamba na hayo, uongozi huo wa Kanisa la TAG waliahidi kuendelea kushirikiana na Rais Dkt.Hussein Mwinyi pamoja na kuendelea kumuombea ili aendelee kuwa kiongozi mwema na kuweza kuiongoza Zanzibar na watu wake pamoja na kuiletea maendeleo endelevu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news