Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameahidi kutekeleza ahadi yake ya kupambana na rushwa, ubadhirifu wa mali za umma na uzembe katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) ambacho hivi sasa anakiongoza rasmi, anaripoti Mwandishi Maalumu Diramakini.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambae pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA), Mhe.Dkt. Hussein Ali Mwinyi akihutubia wakati wa hafla ya Mahafali ya 16 ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) katika ukumbi wa Dk. Ali Mohamed Shein Tunguu Wilaya ya Kati Unguja leo Desemba 30, 2020.(Picha na Ikulu).
Ameyasema hayo katika hotuba yake aliyoitoa katika sherehe za mahafali ya 16 ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), mara baada ya kutawazwa rasmi kuwa Mkuu wa Chuo hicho, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Dkt. Shein, ndani ya kampasi ya Chuo hicho huko Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja
Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa vyama na serikali akiwemo Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad
Katika hotuba yake, Rais Dkt. Hussein Mwinyi amesema kuwa akiwa Mkuu wa Chuo, atafuatilia kwa karibu makusanyo ya ada, ruzuku kutoka Serikalini na kwa wahisani, matumizi ya thamani ya vitu vinavyonunuliwa pamoja na viyanzo mbalimbali.
Rais Dkt. Mwinyi ameutaka uongozi wa chuo hicho kusimamia vizuri na kwa umakini na uadilifu rasilimali za chuo, watunze vizuri nyaraka mbalimbali zenye kuonesha mali zinazomilikiwa na chuo zikiwemo hati miliki za ardhi, nyumba na majengo mengineyo huku akihimiza haja ya kufanyiwa matengenezo na nyumba zote zinazokaliwa wakati wote.
Amewataka wahadhiri na wafanyakazi kufanya kazi kwa bidii na nidhamu kwa kuzingatia sheria na maadili yanayoongoza kazi zao pamoja na kujiandaa kitaaluma ili wawe wanapanda daraja kulingana na taratibu zilizopo
Amesisitiza umuhimu wa usafi wa mazingira na kuutaka uongozi kuhakikisha unaweka mazingira katika kampasi zao yanavutia kwa kuwa na miti ya vivuli na bustani huku akiwataka kujiandaa kwani hivi karibuni atafanya ziara katika kampasi zote kuangalia hayo yote aliyoyasema.
Aidha, Rais Dkt. Hussein Mwinyi amesema kuwa Rais Mstaafu wa Awamu ya Saba, Dkt. Ali Mohamed Shein alionesha njia kwamba chuo hicho ni miliki ya watu wa Zanzibar na kinaendeshwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa hivyo ni lazima kifundishe masomo yanayoendana na mahitaji ya wananchi kiuchumi na kijamii
Kwa msingi huo Rais Dkt. Mwinyi ameitaka SUZA kuwa mfano wa chuo chenye mitaala na programu mbalimbali za ufundishaji zinazozingatia mahitaji ya nchi pamoja na sera na mipango ya maendeleo ya muda mfupi, muda wakati na muda mrefu.
Ameeleza kuwa, SUZA ina kazi kubwa ya kufundisha wataalamu wa kutosha wanaohitajika kusimamia uchumi wa Buluu.
Rais Dkt. Mwinyi ametumia fursa hiyo kumpongeza Rais Mstaafu Dkt. Shein kwa kumkabidhi chuo kikiwa kimepiga hatua kubwa za maendeleo katika kipindi cha miaka 10 cha uongozi wake ambapo miundombinu imeimarika, idadi ya kampasi na idadi ya wanafunzi imeongezeka, wahadhiri na wafanyakazi pamoja na programu zinazofundishwa na hadhi na sifa ya elimu inayotolewa imekuwa.
Rais Dkt. Hussein ameitaka SUZA kuandaa utaratibu mzuri zaidi wa kufanya tafiti na kuweka mkazo wa matumizi ya tafiti katika maeneo mbalimbali yanayohusu uchumi wa Buluu na sekta nyingine za uchumi.
Ameeleza kuwa, ni kazi ya SUZA kwa kushirikiana na taasisi nyingine za elimu ya juu ikiwemo Tume ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (COSTECH) kufanya tathmini ya tafiti zilizofanywa ndani ya kipindi cha 2015-2020 na uhalisia wa tafiti hizo kwa mahitaji ya nchi.
Hivyo, ameeleza kuwa, Zanzibar ina haja ya kuwa na ajenda mpya ya utafiti wa Kitaifa na kusisitiza kuachana na tabia ya kutegemea wahisani hata mambo muhimu ya maendeleo wanayoweza kufanywa na Wazanzibari wenyewe.
Amesisitiza kwamba, atahakikisha wataalmu wote walioajiriwa na wanaolipwa mishahara wanatumia taaluma na uzoefu wao kwa faida ya wananchi na wao wenywe kwani chuo hicho ni lazima kiongeze kasi katika kufanya tafiti mbalimbali.
Ameeleza kuvutiwa na dhamira iliyokuwepo ya kuifanya SUZA kuwa ni Oxford ya Kiswahili na iwe chimbuko la wataalamu, waandishi na malenga wa mashairi na kwa kushirikiana na Baraza la Kiswahili la Zanzibar iwe ni kitovu cha kutoa Kamusi zinazopendwa na zinazoaminika katika lugha ya Kiswahili.
Aidha, ameutaka uongozi wa SUZA, kuandaa mikakati mizuri ya kulinda lahaja za Kizanzibari, kuwa wepesi, kubuni misamiati na istilahi zinazohitajika ili kuweza kwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia.
Rais Dkt. Mwinyi ametoa kazi kwa uongozi wa SUZA kushirikiana na uongozi wa BAKIZA katika kuandaa mikakati na kufanya jitihada za kutafuta ajira nje ya nchi za Kiswahili kwa ajili ya wataalamu mbalimbali waliopo Zanzibar.
“Lazima tuwe na mipango ya kutumia hazina yetu, kiswahili, katika kukuza ajira pamoja na kuhakikisha kwamba tuna mipango imara ya kufundisha na kukieneza katika mataifa mengine,”amesema.
Pia, ameeleza haja ya chuo hicho kuangalia upya mitaala yake na mbinu za ufundishaji kwani wawekezaji wengi katika sekta ya utalii wanapenda kuajiri wafanyakazi kutoka nje ya Zanzibar jambo ambalo yeye haridhishwi kuona hali hiyo licha ya kwua wahitimu wengi wanatolewa katika eneo hilo lakini bado vijana hawapati ajira.
Kwa wale walioomba mikopo ya elimu ya juu na wakapata, Rais Dkt. Mwinyi amewahimiza wawe tayari kulipa deni liliopo kwa kuzingatia sheria na makubaliano yaliyo katika mikataba waliyoijaza.
Amewapongeza wahitimu wote na kuwataka kujiepusha na vishawishi na anasa vinavyoweza kuathiri masomo yao huku akiekeza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuweka mkazo katika sekta ya elimu katika ngazi zote kwa misingi na dhamira ile ile ya waasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar ya 1964.
Wakati huo huo, Rais Dkt.Mwinyi amemtunuku Shaha ya Heshima ya Udaktari wa Falsafa katika Sayansi za Tiba, Rais Mstaafu wa Zanzibar Awamu ya Saba, Dkt. Ali Mohamed Shein na kumpongeza huku akisisitiza kwamba wananchi wa Zanzibar wataendelea kumkumbuka kwa ubunifu wake wa kuanzisha mambo mazuri ambayo watu wengi walihisi hayawezekani.
Rais Mstaafu Dkt. Shein akitoa salamu zake za shukurani ameupongeza uongozi wa chuo hicho kwa kumtunuku shahada hiyo ambayo itaendelea kumpa hadhi huku akieleza imani yake kwamba Rais Dkt. Miwnyi atakiendeleza vyema chuo hicho.
Nae Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Simai Mohamed Said alieleza jinsi wizara yake itakavyoendelea kumuunga mkono Rais Dkt. Hussein pamoja na kueleza miakakati mbalimbali iliyowekwa na wizara hiyo ili iweze kuleta manufaa katika sekta ya elimu.
Mapema Makamu Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Dkt. Zakia Mohammed Abubakar alimueleza Rais Dkt. Hussein kwamba jamii ya chuo hicho cha SUZA, iko tayari kwa moyo mkunjufu kufanya kazi na yeye kwa kufuata kikamilifu ushauri na maelekezo katika kukiendelza chuo hicho.
Aidha, amempongeza Rais Mstaafu Dkt. Ali Moahmed Shein ambaye alikuwa Mkuu wa Chuo tokea mwaka 2010 hadi 2020 kwa juhudi zake kubwa za kukitumikia chuo hicho ambapo kwa juhudi hizo ndipo chuo hicho kikaamua kumtunuku Shahada ya Udaktari wa Falsafa katika Sayansi za Tiba kwa sababu sheria inaruhusu kufanya hivyo.
Makamu Mkuu huyo wa SUZA ameeleza kuwa mwaka huu chuo hicho kinawahitimu jumla ya wanafunzi 1524 ambao Rais Dkt. Mwinyi aliwatunuku vyeti vyao kutoka programu 56 zinazofundishwa na chuo hicho cha (SUZA).
Mkuu huyo ameeleza kwamba katika wahitimu wa mwaka wa masomo 2029/2020 jumla ya wanafunzi ambao wamefanya vizuri zaidi ni 41 ambao kati yao 24 (52%) ni wanawake na 17 (48%) ni wanaume na wanafunzi bora ni watatu.
Katika hafla hiyo Rais Dkt. Mwinyi amewatunuku wanafunzi 244 wa ngazi ya cheti, 799 kwa ngazi ya Stashahada, 453 kwa ngazi ya Shahada na 28 kwa ngazi ya Uzamili huku akiwakabidhi vyeti na zawadi wanafunzi bora watatu akiwemo Nassra Suleiman Mohammed wa Shahada ya Kwanza aliyepata GPA 4.9, Ali Abdalla Moh’d wa Stashahada aliyepata GPA 5.0 na Hanafi Abdallah Moh’d aliyepata GPA 4.9.