Rais Dkt.Mwinyi ateta na wajumbe Jumuiya ya Maimamu Zanzibar

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa Serikali anayoiongoza itahakikisha inashirikiana vyema na Jumuiya ya Maimamu Zanzibar (JUMAZA) katika kujenga misingi ya dini ya Kiislamu hapa nchini, anripoti Mwandishi Maalum Diramakini.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussei Ali Mwinyi (katikati) akisitiza jambo wakati wa mazungumzo na Ujumbe wa Jumuiya ya Maimamu (JUMAZA) waliofika Ikulu jijini Zanzibar leo kumpongeza kutokana na ushindi alioupata katika Uchaguzi Mkuu uliopita mwaka 2020. (Picha na Ikulu).

Dkt.Hussein Mwinyi ameyasema hayo leo Desemba 28, 2020 wakati alipofanya mazungumzo na Wajumbe wa Jumuiya Maimamu Zanzibar (JUMAZA) wakiongozwa na Kaimu Katibu Sheikh Ali Abdalla Amour. 

Wajumbe wengine kutoka JUMAZA waliofika Ikulu kuzungumza na Rais ni Dkt. Moh’d Hafidh Khalfan, Sheikh Masoud Hemed Nassor, Sheikh Yussuf Khamis, Sheikh Abdalla Issa Makame, Sheikh Muhiddin Zubeir Muhiddin na Ukhti Halima Qasim Moh’d.

Katika mazungumzo hayo, Rais Dkt. Hussein Mwinyi amesema kuwa, miongoni mwa mambo makubwa ambayo yanapaswa kupewa kipaumbele katika kujenga misingi ya dini ya Kiislamu ni umoja, amani na mshikamano.

Hivyo, ameeleza kuwa, kuwepo kwa maridhiano ya kisiasa hapa Zanzibar kumetoa nafasi nzuri ya kuimarisha umoja, amani na mshikamano miongoni mwa viongozi,wananchi pamoja na kuamsha ari ya kushirikiana.

Amesema kuwa, hatua hiyo, imesaidia kuweka pembeni kasoro zilizokuwepo hapo siku za nyuma hali ambayo itapelekea kupata maendeleo makubwa hivyo, ni jukumu la viongozi wa siasa, viongozi wa dini pamoja na wananchi kuhakikisha hilo linafanikiwa.

Aidha, Rais Dkt.Mwinyi ameeleza juhudi za makusudi zinazokusudiwa kufanywa na Serikali katika kupambana na udhalilishaji wa kijinsia ikiwa ni pamoja na kuwaita wadau na kukaa nao pamoja na kujadili hatua za kuchukuliwa katika kupiga vita janga hilo wakiwemo viongozi hao wa dini ambao wako katika jamii.

Rais Dkt.Mwinyi ameeleza jukumu kubwa la viongozi wa dini katia kuielewesha jamii juu ya athari za janga hilo ambalo hivi sasa limeshika kasi katika jamii.

Katika maelezo yake Rais Dkt.Mwinyi pia ameeleza haja ya kutafutiwa ufumbuzi changamoto za Hijja huku akieleza umuhimu wakuwepo Mfuko wa Hijja ambao umeweza kuzinufaisha nchi nyingi duniani ambazo zimeuanzisha.

Rais Dkt.Mwinyi ameeleza haja ya kuwekwa kwa utaratibu maalum kwa ajili ya walimu wa madrasa ikiwa ni pamoja na kuwepo miongozo ya utoaji elimu wa madrasa kwa ushirikiano na viongozi wa dini, Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Ofisi ya Mufti pamoja na wadau ambao ni walimu hao wa Madrasa.

Sambamba na hayo, Rais Dkt.Mwinyi ameeleza azma ya Serikali ya kuwaangalia kimaslahi walimu pamoja na madaktari kutokana na kazi kubwa wanazozifanya katika kutoa huduma katika jamii.

Nao Wajumbe wa jumuiya hiyo ya JUWAZA wamempongeza, Rais Dkt. Hussein Mwinyi kwa kuchaguliwa na wananchi wa Zanzibar na kuweza kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

Katika maelezo yao wamempongeza kwa kasi yake aliyoanza nayo katika kuwaletea maendeleo wananchi ikiwa ni pamoja na kuona umuhimu wa kuwepo amani, umoja na mshikamano katika jamii na kuamua kusimamia maridhiano.

Wameeleza kuwa, hatua zake za kurudisha mshikamano nchini na kuleta umoja ni jambo kubwa na la kuungwa mkono na kupongezwa kwani bila ya kuwepo amani, umoja na mshikamano maendeleo hayawezi kupatikana.

Aidha, viongozi hao wa JUWAZA, wameeleza haja ya kufuatwa hatua za makusudi za kupambana na udhalilishaji katika jamii kwani janga hilo limekuwa likipoteza haiba ya nchi.

Uongozi huo pia, ulieleza changamoto zilizopo katika utekelezaji wa safari za Hijja, haja ya kuwepo Mfuko wa Hijja, Benki za Kiislamu kusaidia mchakato wa Hijja, kuwepo utaratibu wa kuwasaidia walimu wa madrasa kutokana na kuwa na mchango mkubwa katika jamii na kuwekewa utaratibu wa kusomesha katika madrasa zao pamoja na kuhakikisha wanyonge wanapata haki zao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news