Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amevitaka vyombo vya Ulinzi na Usalama kufanya uchunguzi wa haraka ili kubaini chanzo cha ajali ya kuporomoka sehemu ya jengo la makumbusho la Taifa la Beit al Ajab iliyotokea Desemba 25, mwaka huu, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi (kushoto) akimjulia hali, Gharibu Juma (14) mkazi wa Kijichi Magharibi"A"akiwa katika Wodi Namba 1 ya wagonjwa mbalimbali katika Hospitali ya Mnazi Mmoja alipowatembelea wagonjwa waliolazwa katika haospitali hiyo leo. (Picha na Ikulu).
Dkt. Mwinyi ametoa agizo hilo leo, wakati alipofanya ziara ya kutembelea Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja kwa lengo la kutoa rambirambi kwa wafiwa pamoja na kuwapa pole majeruhi wa ajali hiyo.
Amevitaka vyombo hivyo kufanya uchunguzi wa kina na wa haraka ili kubaini chanzo cha tukio zima la kuporomoka sehemu ya jengo hilo na kuleta maafa kwa wananchi, ili Serikali iweze kuchukua hatua madhubuti na kwa haraka.
Amesema, msiba uliotokea ni wa Taifa na hivyo akawapa pole wafiwa pamoja na kuwaombea dua majeruhi wa tukio hilo ili waweze kupona kwa haraka na kurudi katika shughuli za ujenzi wa Taifa.
Aidha, amezitaka mamlaka mbalimbali, ikiwemo mji Mkongwe, Shirika la Nyumba pamoja na taasisi ya Wakfu na Mali ya Amana kufanya tathmini ya haraka ya majengo yote yalioko katika hali mbaya, ili yaweze kufungwa na tathmini hiyo iweze kuielekeza Serikali namna ya kuyafanyia matengenezo ili kuepusha ajali kama hiyo.
Amesema, Serikali itagharamia mazishi ya wananchi waliopoteza maisha kutokana na ajali hiyo, sambamba na kuchukua hatua nyingine ili kuhakikisha matukio ya aina hiyo hayatokei tena.
Katika hatua nyingine, Dkt. Mwinyi ametembelea majeruhi wa ajali hiyo waliolazwa hospitalini hapo pamoja na wagonjwa mbalimbali wanaohitaji matibabu kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ajali.
Ameeleza kuwa, majeruhi waliopatwa na ajali ya kuangukiwa na sehemu ya jengo la Beit Al Ajaib wanahudumiwa vizuri na kusema Serikali itachukua hatua muhimu ili kuhakikisha changamoto ya upungufu wa vifaa pamoja na dawa inapatiwa ufumbuzi.
Rais Dkt. Mwinyi amewapongeza wafanyakazi wa hospitali hiyo, wakiwemo madaktari na wauguzi kwa kazi kubwa na nzuri wanayofanya kuwahudumia wagonjwa na kuwataka kuongeza juhudi.
Kutokana na tukio la kuporomoka sejemu ya jengo la Beit al Ajaib, wananchi Burhani Ali Makune (35) mkazi wa Mtoni Kidatu pamoja na Pande Makame Haji (25) mkazi wa Bumbwini walifariki dunia, wakati ambapo Hemed Mattar Abdalla (39), Dhamir Salum Dhamir (37) pamoja na Ali Ramadhan Juma (23) wanaendelea na matibabu Hospitalini hapo.
Katika ziara hiyo Dkt. Mwinyi ameongozwa na Kaimu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Simai Mohamed Said, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Halima Maulid Salum pamoja na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Rufaa Mnazimmoja, Marijani Msafiri Marijani.