Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesisitiza kwamba katika maendeleo ya watu hatokuwa na muhali (huruma) kwani muhali ndio unaoiathiri Zanzibar, anaripoti Mwandishi Maalum Diramakini (Pemba).
Mheshimiwa Rais Dkt. Hussein Mwinyi ameyasema hayo Desemba 17, 2020 huko katika ukumbi Fidel-Castro, Wilaya ya Chake Chake, Mkoa wa Kusini Pemba wakati alipokuwa akitoa shukukrani kwa viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na jumuiya zake pamoja na wazee na mabalozi wa chama hicho.
Amewaeleza viongozi hao kwamba katika uongozi wake fedha atakazozitafuta hatakubali kuchezewa hata kidogo kwani amegombea nafasi hiyo ya Urais kwa lengo la kuwatumikia wananchi.
Ameeleza dhima aliyokuwa nayo kwa Mwenyezi Mungu na kwa wananchi kwa kutekeleza aliyowaahidi na kuwataka viongozi hao kuwa tayari kwa yale yote watakayoyasikia katika kipindi hiki.
Ameahidi kuisimamia miradi hiyo ili kuweza kupata thamani ya matumizi ya fedha zilizotumika ambazo ni nyingi na kueleza kwamba katika hatua hiyo wapo watu watakaoguswa.
Ameeleza kuwa, kuwepo kwa amani kutapelekea wepesi katika kuleta maendeleo na ndio maana wakati wa uchaguzi katika kampeni zake alizozifanya Unguja na Pemba alihubiri amani.
Amesisitiza kwamba, kazi kubwa iliyobaki hivi sasa ni kutekeleza Ilani ya Uchaguzi wa CCM ya mwaka 2020-2025 sambamba na ahadi zote alizoziahidi wakati wa kampeni za uchaguzi.