Rais Dkt.Mwinyi awapa faraja wawekezaji, wavutiwa kuwekeza zaidi

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewahakikishia wawekezaji wanaotaka kuja kuwekeza Zanzibar kwamba Serikali ya Awamu ya Nane itawawekea mazingira mazuri, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Ameyasema hayo Ikulu jijini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na Mmiliki wa Hoteli ya Park Hyatt, Ali Saeed Juma Albwardy kutoka nchini Dubai akiwa amefuatana na Nicolas Cedro, Meneja Mkuu wa Hoteli ya Park Hyatt, Nicolas Kong, Meneja Mkuu wa Melia, Zanzibar pamoja na Yakoub Osman Sidik.

Katika maelezo yake, Rais Dkt. Hussein Mwinyi alimueleza muwekezaji huyo kwamba Serikali anayoiongoza itahakikisha inafanya kazi vizuri na wawekezaji sambamba na kuwawekea mazingira bora ya uwekezaji.

Ameeleza kuwa, kwa upande wa sekta ya utalii ambayo ndio inayochangia zaidi katika pato la Taifa, Serikali ya Awamu ya Nane itahakikisha sekta hiyo inawekewa mazingira bora pamoja na wawekezaji wake.

Rais Dkt.Hussein Mwinyi ameeleza kwamba, Serikali yake imekusudia kufanya kazi na sekta binafsi kwani inatambua umuhimu wa sekta hiyo katika kukuza uchumi na kuinua pato la Taifa.

Ameongeza kuwa, Serikali anayoiongoza itahakikisha inashirikiana vyema na sekta binafsi katika kuinua uchumi wa Zanzibar.

Amesisitiza kwamba, sekta binafsi ndio injini ya uchumi, hivyo Serikali ya Awamu ya Nane itaweka mikakati maalum ya kuhakikisha sekta hiyo inaimarika ili kuleta tija kwa nchi na wananachi wake kwani kuimarika kwake kutaongeza soko la ajira sambamba na pato la Taifa.

Aidha, Rais Dkt.Hussein Mwinyi ameeleza umuhimu wa kuimarisha bandari na viwanja vya ndege ili sekta ya utalii, biashara na uwekezaji zizidi kuimarika na kusisitiza kwamba hio ndio azma ya Serikali ya Awamu ya Nane.

Sambamba na hayo, Rais Dkt.Hussein Mwinyi ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji, wafanyabishara na wenye viwanda wa ndani na nje ya Zanzibar waje kuwekeza kutokana na kuwepo fursa nyingi hapa nchini.

Amesisitiza kuwa, juhudi za makusudi zitachukuliwa na Serikali yake katika kuhakikisha inaweka miundombinu rafiki ili wawekezaji, wafanyabiashara na wenye viwanda waje Zanzibar kufanya shughuli zao hizo.

Pamoja na hayo, Rais Dkt.Hussein Mwinyi amekiri kwamba Zanzibar ina vivutio vingi vya kitalii sambamba na ukarimu wa watu wake na utamaduni walionao ambavyo vyote hivyo ni miongoni mwa vivutio vikubwa vya kitalii na kuahidi kwamba vyote hivyo vitaimarishwa katika kufikia lengo lililokusudiwa.

Mapema mmiliki wa Hoteli ya Park Hyatt, Ali Saeed Juma Albwardy alimpongeza Rais Dkt.Hussein Mwinyi kwa kuchaguliwa na wananchi wengi wa Zanzibar na kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi hatua ambayo inatokana na imani ya wananchi hao kwa Rais Dkt.Mwinyi.

Albwardy amemueleza Rais Dkt. Hussein azma ya Kampuni Park Hyatt ya kuongeza uwekezaji hapa Zanzibar kutokana na kuwepo kwa vivutio kadhaa sambamba na ukarimu na utamaduni wa watu wake.

Ameongeza kuwa, kampuni yake yenye makao makuu yake nchini Dubai, lakini ina hoteli kadhaa katika nchi mbalimbali duniani inavutiwa zaidi na Zanzibar kutokana na mazingira yake mazuri ya kitalii ukiwemo Mji Mkongwe.

Mmiliki huyo wa Hoteli ya Park Hyatt amesifu ushirikiano mzuri alioupata na anayoendelea kuyapa kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kuahidi kwamba atahakikisha anaendelea kuitangaza zaidi Zanzibar Kimataifa.

Aidha, Albwardy amemueleza Rais Dkt.Hussein azma yake ya kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Nane ya kuimarisha sekta za biashara na viwanda, vikiwemo viwanda vya nguo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news