Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa wabadhirifu na wezi wa mali ya umma hawana nafasi katika Serikali ya Awamu ya Nane anayoiongoza, anaripoti Mwandishi Maalum Diramakini (Pemba).
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Vikundi vya Wajasiriamali mbalimbali kutoka Mkoa wa Kaskazini Pembe wakati wa mkutano wake na wajasiriamali hao kutowa shukrani zake kwao kwa kumchagua kuwa Rais wa Zanzibar katika uchaguzi Mkuu wa Zanzibar uliofanyika mwezi Oktoba 2020, mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi Wete Pemba. (Picha na Ikulu).
Mheshimiwa Rais ameyasema hayo katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba wakati alipokutana na makundi ya wajasiriamali wa Mkoa huo kwa ajili ya kuwashukuru na kuwapongeza kufuatia ushindi mkubwa katika uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba mwaka huu.
Amesema kuwa, kuna matatizo ya wizi wa mali ya umma na ubadhirifu ambapo kuna miradi mikubwa ya mikopo ya serikali ambayo haina thamani ya fedha zilizotolewa na kusema imetosha na kuanzia sasa kila mradi utasimamiwa na kupatikana thamani kwa fedha zake.
Ameeleza uwepo wa tatizo la rushwa katika utoaji wa huduma katika jamii ambayo ni haki ya mwananchi kama vile hospitali, skuli, kwenye ofisi za serikali pamoja na huduma za vyeti vya kuzaliwa “mtoto anakaa hadi anakuwa mtu mzima hajapata cheti cha kuzaliwa jambo hili haliwezekani,” amesisitiza.
Ameeleza kwamba huduma za kijamii zimekuwa zikitolewa vibaya ikiwa ni pamoja na usumbufu katika utoaji wa vyeti hivyo vya kuzaliwa na kuwataka wahusika wote waliokuwa kwenye serikali na wenye dhamana ya kutoa huduma kwa wananchi watoe huduma hiyo na kamwe hatowavumilia wale wasiofanya kazi zao.
Amewataka Mawaziri, Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha matatizo hayo yanaondolewa kwa haraka iwezekanavyo huku akitolea mfano huduma ya dawa jinsi inavyotolewa hospitali na kutaka matatizo hayo kuondolewa haraka.
Amesema kuwa, hivi sasa kumetengenezwa tabia ya kutoa fedha ili kupatikane ajira na tayari anajua wapo waliotoa fedha na hata hizo ajira hawajazipata.
Sambamba na hayo amesema kuwa, matatizo yaliopo katika jamii yanajulikana na yale yanayotekelezwa na watendaji wa serikali yanajulikanwa na hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wale wote wanaofanya vitendo hivyo na kueleza namna atakavyowapima watendaji wake kwa jinsi watakavyotekeleza kero za wananchi na kusema wasiotekeleza hawafai ndani ya Serikali yake.
Kwa upande wa madhila katika jamii, Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa madhila katika jamii yataondoshwa kwani kuna kasoro nyingi ikiwemo dhuluma kwa wananchi kukosa haki zao kutokana na umasikini walionao.
Ameongeza kuwa, wapo wanaonyanganywa mali zao vikiwemo viwanja kwa umasikini tu walionao na kueleza kwamba tayari ameshaatoa maelekezo kwa Wakuu wa Mikoa kufuatilia na wasikae maofisini na badala yake wakawasikilize wananchi wanaodhulumiwa ili wachukue hatua mara moja.
Amesisitiza kwamba, Mkuu wa Mkoa ama Mawaziri aliowateua iwapo wasipofanya kazi ya kuwaondoa matatizo wananchi basi hawafai katika Serikali anayoiongoza.
Amesema kuwa, uwajibikaji ni suala la lazima na kila mtu awajibike kuanzia ngazi za juu mpaka ngazi za chini kuanzia Makamu wa Kwanza wa Rais, Makamu wa Pili wa Rais, Mawaziri mpaka ngazi ya Masheha wote hao wanatakiwa kuwajibika.
Ameeleza kuwa, madhumuni ya mkutano huo ni kutoa shukurani ambapo mara ya kwanza kukutana na makundi hayo ni pale alipokuwa mgombea wa Urais ambapo aliyaomba kumuunga mkono wakati huo na walifanya hivyo kwa juhudi kubwa.
Amesisitiza kuwa, tayari ameshaunda Serikali na ataendelea na nafasi zilizobaki na iko tayari kwa kazi na yale yote aliyowaahidi vikundi hivyo atayatekeleza.
Amesema kuwa, mafanikio zaidi yatapatikana kutokana na kuwepo kwa amani na umoja wa kitaifa na kusisitiza kulindwa kwa amani ili kuleta maendeleo.
Amesema kuwa, kuunda serikali ya Umoja wa Kitaifa lengo lake ni kuwaunganisha wananchi, kuondoa chuki, kuondoa mifarakano na kujenga umoja wa watu wanaopendana jambo ambalo litapelelekea maendeleo na kutaka wananchi waunge mkono juhudi hizo.
Amesema kuwa, si wote waliofurahi kutokana na jambo hilo lakini jambo hilo lina heri ndani yake kwani ubaguzi, chuki vikiondolewa mafanikio makubwa yatapatikana katika jamii.
Ameongeza kuwa hapo siku za nyuma mifarakano ya kila aina ilikuwepo lakini umefika wakati mambo hayo yaachwe nyuma na watu wawe wamoja ili kuleta maendeleo yaliyoahidiwa na wale waliokuwa hawajawa tayari wataendelea kupewa elimu.
Ameeleza kuwa, wale wote waliokuwa hawajawa tayari kuunga mkono umoja huo wataendelea kunasihiwa ili wawe pamoja kwa lengo la kuuendeleza umoja wa kitaifa kwani amani na umoja vikiwemo maendeleo yatapatikana.
Rais Dkt.Hussein amesema kuwa, katika wakati wa kampeni alikutana na makundi mbali mbali ambao walimpa changamoto zao na kuahidi kwamba changamoto hizo zote atazifanyia kazi ilimradi waweze kuongeza kipato chao.
Miogoni mwa makundi hayo ni wakulima ambapo alisema kuwa atahakikisha kwamba changamoto zao walizomueleza wakati wa kampeni zinafanyiwa kazi kwa azma ya kuwaletea maendeleo na kuvitaka vikundi vyote kuwasilisha changamoto zao kwa Wakuu wa Mikoa na Mawaziri aliowateua.
Pamoja na hayo, alieleza kwamba tayari wapo wawekezaji ambao wameahidi kuja kuekeza katika sekta mbali mbali ikiwemo ya uvuvi ambao wameahidi kujenga bandari,viwanda vya kusindika samaki, viwanda vya kutengeneza nyavu na vinginevyo.
Ameeleza kuwa, hatua za makusudi zitachukuliwa katika kuwasaidia wavuvi ili waondokane na uvuvi wa kizamani wa kutumia zana duni kwa kujenga viwanda vya kusindika samaki, bandari maalum pamoja na nyenzo kama vile nyavu ambazo zitatengenezwa hapa hapa Zanzibar.
Pia, alieleza kuwa wawekezaji wengi wameshaonesha nia ya kuja kuekeza katika sekta ya uvuvi kwani lengo ni kuwa wakezaji wakubwa wawasaidiwa wavuvi wadogo kwa kuwapatia soko la uhakika huku serikali ikishirikiana nao ili kuwasaidia wavuvi hao kuondokana na umasikini.
Kwa upande wa Wajane, Rais Dkt. Mwinyi alisema kuwa tayari Mama Mariam Mwinyi ameshaeleza utayari wake wa kuwa mlezi wa kundi hilo ambapo pia. amemteua Mkuu wa Mkoa huo mwanamke ili kuhakikisha matatizo yao yanatatuliwa sambamba na maisha yao kuwa bora zaidi.
Pia, Ris Dkt. Hussein Mwinyi amewahakikishia wajasiriamali wadogo wadogo kwamba watajengewa masoko ya kisasa, watapewa vitambulisho na kulipa kodi mara moja kwa mwaka na linalofanywa na serikali hivi sasa ni kutafuta fedha kwa ajili ya utekelezaji ili wajasiriamali hao wapate kunufaika na biashara zao.
Amesema kuwa kwa upande wa wafugaji samaki juhudi za makusudi zitachukuliwa katika kuhakikisha wanafanya shughuli zao vyema ikiwa ni pamoja na kuwapa vifaranga vya samaki sambamba na kutafuta njia bora zaidi za ufugaji.
Aidha, amesema kuwa kila aina ya udhibiti utafanyika ili fedha za mfuko wa TASAF na kuweka kila aina ya udhibit kwa lengo la kuwafikia wale wanaostahiki kuzipata.Aliwataka wafanyakazi wa gereji kuorodhesha vifaa wanavyovitaka na kumfikishia Mkuu wa Mkoa ili taratibu za kupata vifaa hivyo zifanyike katika kipindi kifupi.
Kwa upande wa walemavu Rais Dkt. Hussein amesema kuwa kundi hilo linahitaji msaada zaidi na kuahidi kila juhudi zitachukuliwa ili kundi hilo lisibaki nyuma.
Kwa upande wa kundi la vijana katika suala zima la ajira, alisema kuwa juhudi za makusudi zitachukuliwa katika kuhakikisha viwanda vingi vinajegwa Unguja na Pemba ili vijana wengi waweze kupata ajira.Alisema kuwa tayari ameshatoa maelekezo kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya ili kila Wilaya iwe na eneo maalum la viwanda na miuondombinu iwe tayari kwani wawekezaji wapo na wako tayari.Hivyo, aliwataka vijana wawe tayati kufanya kazi kwani juhudi za makusudi zitachukuliwa ili ajira zipatikane.
Alieleza azma yake ya kwenda Pemba na kukutana na wananchi wote katika mkutano wa hadhara huku akieleza azma ya Serikali ya kuifanya Pemba kuwa eneo maalum la uwekezaji ili maendeleo ya Unguja na Pemba yaende sambamba.
Amesema kuwa, miundombinu itajengwa ikiwemo bandari ili mizigo inayokwenda kisiwani humo iwe rahisi kufika pamoja na ujenzi barabara na miundombinu mengine.
Katika maelezo yake hayo, Rais Dkt. Mwinyi ameeleza juhudi zitakazochukuliwa katika kupambana na udhalilishaji katika jamii kwani ni jambo baya sana na kusisitiza kamwe serikali haitokubali kushindwa na kadhia hiyo.
Amewapongeza wananchi hao kwa kumpa kura nyingi na njinsi walivyojitokeza kwa wingi katika mkutano huo huku akiwataka kumuombea dua yeye na watendaji wenzake, kuiombea dua nchi iendelee kuwa na amani na umoja uliopo ili kupata maendeleo zaidi.
Nae Waziri wa Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman amempongeza Rais kwa hatua yake hiyo na kueleza hatua zitakazochukuliwa na Wizara yake katika kuunga mkono juhudi za Rais.
Mapema Mkuu wa Mkoa huo, Salama Mbarouk alimpongeza Rais kwa ziara yake hiyo ya kuomana na makundi hayo ambayo aliyapitia wakati wa kampeni huku akiahidi kuwatumikia wajasiriamali, wafanyabiashara na wengine ili wawze kufanikiwa.
Ametumia fursa hiyo kumsifu na kumshukuru Mke wa Rais wa Zanzibar, Mama Mariam Mwinyi kwa kumuunga mkono Rais wakati wote tokea wakati wa kampeni zake hadi hivi leo.
Nae Askofu Kefa Martin Mjuangwa akitoa neno la shukurani amempongeza Rais Dkt.Hussein kwa ushindi wake mkubwa aliopata katika uchaguzi uliopita sambamba na kumpongeza Mama Mariam kwa kumuunga mkono Rais.
Amempongeza Rais kwa kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa sambamba na kutimiza ahadi yake ya kushukuru baada ya uchaguzi.