Rais Dkt.Mwinyi: Nipo tayari kutekeleza ahadi

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewaeleza wananchi kwamba yuko tayari kutekeleza ahadi alizoziahaidi huku akisisitiza kwamba ataifanya Pemba kuwa sehemu maalum ya uwekezaji, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt. Hussein Ali Mwinyi akizungumza na baadhi ya Vikundi vya Wajasiriamali mbalimbali kutoka Mkoa wa Kusini Pemba wakati wa mkutano wake wa kutoa shukrani kwao kwa kumchagua kuwa Rais wa Zanzibar katika uchaguzi mkuu wa Zanzibar uliofanyika mwezi Oktoba 2020, mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa Skuli ya Sekondari ya Fidel Castro Wilaya ya Chakechake Pemba. (Picha na Ikulu).

Rais Dkt. Hussein Mwinyi ameyasema hayo huko katika ukumbi Fidel-Castro, Wilaya ya Chake Chake, Mkoa wa Kusini Pemba wakati alipokutana na vikundi vya wajasiriamali vya Mkoa wa Kusini Pemba kwa ajili ya kutoa shukurani na kutekeleza ahadi aliyoitoa wakati wa kampeni ya kurudi kuonana nao maara baada ya uchaguzi. 

Katika maelezo yake Rais, Dkt. Hussein amesema kuwa, Serikali ya Awamu ya Nane itaweka vivutio vya uwekezaji ili iwe rahisi zaidi kuekeza katika kisiwa cha Pemba.

Amesema kuwa, mbali na hatua hiyo, Serikali ya Awamu ya Nane itahakikisha inapunguza kodi kwa wawekezaji wote walioamua kuekeza katika kisiwa cha Pemba.

Rais Dkt.Hussein Mwinyi ameeleza kuwa , mazingira mazuri yatawekwa katika kuhakikisha hilo linafanikiwa ikiwa ni pamoja na kuimarisha bandari, uwanja wa ndege, barabara sambamba na kuwa na maeneo maalum ya uwekezaji. 

Amesisitiza kuwa, kuiweka Pemba kuwa ni sehemu maalum kutapelekea azma ya kutekeleza uwezekano wa ajira 300,000 zilizoahidiwa katika Ilani ya Uachaguzi ya mwaka 2020-2025 kwa upande wa Pemba unafikiwa na kutekelezwa kama ilivyoahidiwa.

Rais Dkt.Hussein ametumia fursa hiyo kutoa shukurani kwa wananchi wote kwa kufanya uchaguzi kwa amani sambamba na kuendelea kudumisha amani na umoja miongoni mwao.

Ametoa shukurani kwa vikundi vyote vya wajasiriamali ambao aliwaahidi kukutana nao baada ya kumchagua na kumalizika kwa uchaguzi ambao umempa ushindi mkubwa na akaona haja ya kutekeleza ahadi yake hiyo. 

Aidha, Rais Dkt.Hussein Mwinyi amesisitiza kwamba bila ya amani na umoja hakuna maendeleo na kuwataka wananchi kujipongeza kwa hatua iliyofikiwa ya kudumisha amani iliyopo.

Ameongeza kuwa, vyama vyote vya siasa hapa Zanzibar vimekubali kuwa kitu kimoja katika kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa, hivyo aliwataka wananchi kuweka tofauti zao za kiitikadi pembeni na kuwa kitu kimoja katika kuleta maendeleo.

Amewataka wale wote ambao hawajaona umuhimu wa kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa watambue umuhimu wake na kuwataka wananchi wote kuunga mkono hatua hiyo ambayo itawaletea manufaa makubwa mbele yao. 

Rais Dkt.Hussein Mwinyi amesisitiza kwamba uchaguzi umekwisha na lililobaki hivi sasa ni kushirikiana katika kuijenga nchi na kuwaletea wananchi maendeleo hasa ikizingatiwa kwamba safu ya Mawaziri na Wakuu wa Mikoa ikotayari.

Rais Dkt.Hussein Mwinyi ametumia fursa hiyo kuwapongeza viongozi wote wa dini kwa kuliombea taifa na kuahidi kufanya kazi nao ili kuondoa changamoto zinazowakabili.

Pia, amewaeleza wakulima atahakikisha kwamba changamoto zao walizomueleza wakati wa kampeni zinafanyiwa kazi kwa azma ya kuwaletea maendeleo na kuvitaka vikundi vyote kuwasilisha changamoto zao kwa Wakuu wa Mikoa na Mawaziri aliowateua. 

Ameeleza kwamba, mabenki mengi ambayo uongozi wake amekutana nao hivi karibuni yameahidi kushirikiana na Serikali katika kuwasaidia wajasiriamali wadogo wadogo ikiwa ni pamoja na kuwapunguzia masharti ya mikopo.

Amesema kwamba, kinachohitajika hivi sasa kwa mabenki hayo ni kuwapatia wajasiriamali mikopo nafuu sambamba na kuwapa elimu ya kuwasaidia katika shughuli zao mara baada ya kupata mikopo hiyo. 

Pamoja na hayo, ameeleza kwamba tayari wapo wawekezaji ambao wameahidi kuja kuwekeza katika sekta mbalimbali ikiwemo ya uvuvi ambao wameahidi kujenga bandari,viwanda vya kusindika samaki, viwanda vya kutengeneza nyavu na vyenginevyo.

Ameeleza kuwa hatua za makusudi pia, zitachukuliwa katika kuwasaidia wavuvi ili waweze kufanya shughuli zao kwa ustadi zaidi ikiwa ni pamoja na kupata soko na kuondokana na uvuvi usio na tija.

Pia, Ris Dkt. Hussein Mwinyi amewahakikishia wajasiriamali ambao ni mafundi wa gereji wakae pamoja na kueleza mahitaji yao yakiwemo upatikanaji wa dhana. 

Kwa upande wa Wajane, Rais Dkt. Hussein alisema kuwa tayari Mama Mariam Mwinyi ameshaeleza utayari wake wa kuwa mlezi wa kundi hilo huku akiwataka kukaa pamoja na kueleza changamoto zao ili zipate kufanyiwa kazi.

Aidha, kwa upande wa wanamichezo, Rais Dkt. Hussein Mwinyi ameeleza juhudi zitakazochukuliwa katika suala zima la kupata udhamini ambalo ndio muhimu katika kuimarisha michezo.

Ameongeza kuwa, bado kuna changamoto katika michezo hasa katika mpira wa miguu ambapo katika chama cha mpira wa miguu ZFF kina changamoto katika uongozi wake na kusisitiza kwamba kwa vile wanamichezo wapo, viwanja vipo cha muhimu hivi sasa ni kutafuta viongozi bora. 

Ameeleza azma ya kuondosha utitiri wa kodi kwa wajasiriamali wadogo wadogo sambamba na kuwapatia vitambulisho pamoja na kulipa kodi ndogo kwa mwaka.Alieleza haja kwa wafanyabiashara kulipa kodi na Serikali itawawekea mazingira mazuri katika kuhakikisha wanafanyabiashara zao lakini cha muhimu ni kuja kulipa kodi zitakazowekwa japo kuwa ni ndogo. 

Rais Dkt. Hussein Mwinyi ameeleza azma ya Serikali anayoiongoza katika kuwasaida watu wenye mahitaji maalum wakiwemo walemavu na kuwataka viongozi aliowateua wanatekeleza majukumu yao kwa kuwasaidia watu wenye ulemavu. 

Nao wajasiriamali hao wametumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dkt. Hussein Mwinyi kwa kutekeleza ahadi yake aliyoahidi wakati wa kampeni ya kuja kuonana nao baada ya kumaliza uchaguzi.

Wameeleza kwamba, hatua anazozichukua Rais Dkt. Hussein zitasaidia katika kutekeleza azma yake ya kupambana na umasikini.

Sambamba na hayo, wajasiriamali wamempongeza Rais Dkt. Hussein Mwinyi kwa kusimamia vyema Serikali ya Umoja wa Kitaifa hatua ambayo italeta manufaa makubwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news