Rais Dkt.Mwinyi, wasaidizi wake wafanyiwa dua maalum

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhadj Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema viongozi wa kisiasa wana dhima kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu na kubainisha maridhiano ya kisiasa yaliofanyika yameonyesha njia sahihi katika kudumisha umoja na mshikamano nchini, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabi akisoma dua maalum ya kuiombea Nchi amani na utulivu pamoja na kumuombea dua Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi (kushoto) iliyofanyika leo katika Masjid Mushawal Mwembeshauri Jijini Zanzibar (wa pili kulia) Makamo wa Pili wa Rais Mstaafu Balozi Seif Ali Iddi.[Picha na Ikulu)

Alhadj Dkt. Mwinyi amesema hayo katika Dua maalum ya kuiombea nchi na viongozi wake amani, hafla iliyofanyika katika Msikiti wa Mushawarra uliopo Muembeshauri jijini hapa.

Amesema, kuna umuhimu kwa wananchi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwaongezea neema ya maridhiano yaliofanikisha uundaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, baada ya uchaguzi mkuu kumalizika.

Amesema, viongozi wana dhima kubwa ya kuhakikisha wanadumisha amani na mshikamano na hivyo akatumia fursa hiyo kumpongeza Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad na Chama chake cha ACT Wazalendo kwa kukubali kushiriki katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).

Amesema, yeye binafsi anaamini Wazanzibari wote ni kitu kimoja wakiwa na dhamira ya kuijenga Zanzibar na hivyo akawataka viongozi wa Dini kuendelea kuwaombea dua viongozi ili waendelee kuiongoza nchi kwa ufanisi.

“Viongozi wana dhima kubwa kwa Mwenyezi Mungu, maridhiano yaliofanyika yameonyesha mwelekeo sahihi wa nchi,”amesema Rais Dkt.Mwinyi.

Ameeleza kuwa, pamoja na Wazanzibari kuwa na mengi ya kumshukuru Mwenyezi Mungu, pia wanapaswa kuendeleza amani iliopo nchini ili kazi ya kuleta maendeleo na kukuza uchumi wa Taifa iweze kufanikiwa.

Alhadj Dkt. Mwinyi amesema, wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu uliopita alitoa ahadi nyingi sana kwa wananchi ikiwemo ile ya kusisitiza kuendeleza amani na utulivu iliyopo nchini pamoja na kuwataka wananchi kuunga mkono juhudi za Serikali katika kufanikisha azma hiyo.

Aidha, amewataka Wazanzibari kufanya kazi kwa bidii kwa kila mmoja kutekeleza wajibu wake kikamilifu mahala alipo ili kuleta ustawi wa maisha ya wananchi.

Ametoa shukurani kwa wananchi wote wa Zanzibar kwa hatua zao za kumtumia pongezi kwa kuleta maridhiano na kubainisha kuwa hatua hiyo inaleta matumaini kuwa wananchi wengi wameridhia na kukubali jambo hilo.

Vile vile amesiitiza dhamira yake ya kuendelea kusimamia umoja na mshikamano katika nchini ili kuharakisha kasi ya maendeleo.

Alhadj Dkt. Mwinyi amemshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kuibariki Zanzibar na kubaki katika hali ya mani, sambamba na kuwapongeza waandaaji wa Dua hiyo kwa kuona umuhimu wa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupokea maombi yao , ikizingatiwa dua kama hiyo ilifanyika kabla ya Uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, 2020.

Mapema, Waziri wa Nchi (OR) Katiba, Sheria,Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman alitoa shukrani kwa viongozi wakuu wa kitaifa pamoja na wananchi waliohudhuria katika hafla hiyo muhimu yenye faida kubwa kwa taifa.

Nae, Katibu wa Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khalid Mfaume amesema dua hiyo inalenga kumshukuru Mwenyezi Mungu pamoja na kumuombea Dua Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhadj Dkt. Hussein Ali Mwinyi na wasaidizi wake ili waweze kutekeleza vyema majukumu yao ya kitaifa.

Viongozi mbali mbali wa kitaifa wamehudhuria katika dua hiyo wakiwemo Marais Wastaafu Alhadj Amani Abeid Karume, Alhadj Ali Mohamed Shein, Alhadj Balozi Seif Ali Idd, Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mariamu Ali Mwinyi, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dkt. Abdulhamid Yahya Mzee, Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kaabi, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Dkt. Mwinyi Talib Haji, Mawaziri, Mwakilishi wa Mufti Mkuu kutoka Tanzania Bara Sheikh Alhad Mussa Salum pamoja na wananchi wa Mikoa ya Unguja. 

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news