Rais Dkt.Mwinyi:Mwenyenzi Mungu atuongoze, 2021 tufanye kazi kwa bidii

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewataka wananchi kuuanza mwaka mpya wa 2021 kwa kufanya kazi kwa ari mpya pamoja na kuiunga mkono Serikali kwa yale mambo yaliyopangwa kutekelezwa, anaripoti Mwandishi Maalum Diramakini.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi akitoa salamu za mwaka mpya kwa wananchi wa Zanzibar, amewatakia heri wananchi wote wa Zanzibar na Tanzania kwa kuukaribisha Mwaka 2021 na kuuaga 2020. (Picha na Ikulu/Diramakini).

Rais Dkt. Hussein Mwinyi ameyasema hayo leo wakati akitoa salamu za mwaka mpya wa 2021 kwa wananchi kupitia vyombo vya habari katika hotuba aliyoitoa katika ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar.

Dkt. Hussein Mwinyi amesema kuwa, mapinduzi makubwa ya kiuchumi yaliyodhamiriwa kufanywa katika uchumi wa buluu, ujenzi wa miundombinu, uwekezaji, utalii, biashara, viwanda, kilimo, uvuvi, ufugaji, elimu, afya, usambazaji wa maji safi na salama na uwezeshaji wa wananchi yatafikiwa iwapo kila mmoja atafanya kazi kwa bidlii na kutekeleza wajibu wake.

Rais Dkt. Hussein Mwinyi amewataka wananchi kuunga mkono juhudi za Serikali katika kupambana na rushwa, wizi, ubadhirifu wa mali ya umma na uzembe katika sehemu za kazi pamoja na kuunga mkono utekelezaji wa mipango ya kukomesha udhalilishaji wa watoto na unyanyasaji wa kijinsia.

Amesisitiza kuwa mwaka 2021 uwe ni mwaka wa kuwa na mipango imara ya usafi wa miji na uhifadhi wa mazingi na kwa pamoja wananchi wahimizane katika matumizi bora ya ardhi na washirikiane katika kuitatua migogoro ya ardhi iliyopo na itakayojitokeza.

Ameongeza kwamba, miezi miwili ya awamu ya uongozi wa Serikali katika kipindi hiki Serikali ya Umoja wa Kitaifa imeundwa kama Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 inavyoelekeza ambapo moja kati ya malengo ya kuwepo kwa mfumo huo ni kuimarisha umoja na mshikamano miongoni mw awananchi wa Zanzibar.

“Kipindi cha mwaka mmoja ni kirefu katika maisha ya mwanaadamu hutokea mambo mengi makubwa ambayo baadhi yao huacha alama na kumbukumbu za historia katika ngazi ya kitaifa, kimataifa na hadi ngazi ya familia na mtu mmoja mmoja,"amesema Dkt.Mwinyi.

Aidha, Dkt Mwinyi amesema kuwa, kwa ngazi ya Kimataifa, moja kati ya mambo makubwa yaliyotokea katika mwaka 2020 ni kuenea na kusambaa kwa maradhi ya Virusi vya Korona (COVID-19) ambayo yalijulikana na kutangazwa rasmi mwezi wa Disemba, 2019.

Alieleza kwamba athari za maradhi hayo kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii ni kubwa ambapo kwa nchi za visiwa ni kubwa zaidi kutokana na utegemezi wa sekta za huduma hasa utalii kwa maendeleo ya kiuchumi hali ambayo imeonekana kujitokeza hata hapa Zanzibar.

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa mwaka 2020 unaagwa ikiwa kasi ya ukuaji wa uchumi imeathirika sana kutokana na maradhi hayo hivyo, ni vyema zikachukuliwa changamoto zilizojitokeza zikafanyiwa kazi ili zisiendelee kuathiri kasi ya utendaji na uwajibikaji.

Alisisitiza kwamba kamwe isiwe kuendelea kuwepo kwa maradhi hayo katika mataifa mengine kuwa kisingizio au kikwazo kwa kila kitu kilichopangwa kufanywa kwa maendeleo ya Zanzibar.

Kwa ngazi ya Kitaifa, alisema kuwa mwaka 2020 utakumbukwa kwa tukio la kuondokewa na Kiongozi Mpendwa, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Marehemu Benjamin Mkapa ambae alifariki Julai 24, 2020 na kuzikwa Julai 29. 2020 kijijini kwao Lupaso, Mkoani Mtwara.

Dk. Mwinyi pia, alilitaja tukio la uchaguzi Mkuu ambalo limefanyika kwa hali ya amani na utulivu na hatimae kumuwezesha Dk. John Pombe Joseph Magufuli kuendelea kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kipindi cha Pili cha Serikali ya Awamu ya Tano anayoiongoza.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Watanzania wataendelea kuukumbuka mwaka 2020 kwa maendeleo makubwa ya kiuchumi yaliyopatikana ndani ya mwaka 2020 chini ya uongozi wa Rais Dk. Magufuli ikiwa ni pamoja na Benki ya Dunia kuitangaza rasmi Tanzania kuingia katika uchumi wa kipato cha kati ngazi ya chini kuanzia Julai mosi 2020.

Kwa upande wa Zanzibar Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa mwaka 2020 utakumbukwa kwa tukio lililotokea katika Mji Mkongwe wiki iliyopita ya Disemba 25. 2020 la kuanguka sehemu kubwa ya Jengo la Beit El Ajab na kusababisha vifo vya watu wawili na wengine kadhaa kujeruhiwa.

“Tunamuomba Mwenyezi Mungu azilaze mahala pema peponi roho za marehemu wote kwa mara nyengine tunatoa mkono wa pole kwa familia za marehemu vile vile, tunamuomba Mwenyezi Mungu awape uzima na nguvu za kuendelea na maisha ya kawaida wale wote walioumia kutokana na ajali hiyo”, alisema Dk. Mwinyi.

Hivyo, Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba kwa pamoja azimio la mwaka mpya wa 2021 liwe ni kuungana katika kutafuta njia bora na endelevu za kuulinda na kuuhifadhi Mji Mkongwe, ikiwa ni pamoja na kuyatekeleza mapendekezo yote yalitolewa katika mkutano uliofanyika Disemba 28 mwaka 2020 baina ya viongozi wa Serikali na Wadau mbali mbali wa Mji Mkongwe.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa mwaka 2020 utakumbukwa kwa kufanya Uchaguzi Mkuu na kufanikisha zoezi hilo muhimu kwa salama na amani huku muda wa uongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Awamu ya Saba iliyokuwa ikiongozwa na Rais Mstaafu Dk. Ali Mohamed Shein kumalizika na kaunza Serikali ya Mapinduzi Awamu ya Nane anayoiongoza.

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa mwaka 2020 ni mwaka ambao Zanzibar imekamilisha utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2020 na kufikia lengo la kiwango cha nchi zenye kipato cha kati kwa kuzingatia vigezo vya kiuchumi vilivyowekwa na Jumuiya za Kitaifa.

Katika kipindi cha uongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Awamu ya Saba, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa maendeleo makubwa ya kiuchumi yameshuhudiwa yakiwemo kukamilika kwa miradi mikubwa ya ujenzi wa miundombinu, skuli za ghorofa, majengo ya Ofisi, makaazi na maduka ya kisasa pamoja na miradi ya suambazaji wa maji safi na salama.

Aliongeza kuwa kati ya miradi hiyo, imo miradi ya jengo la Abiria la Terminal III katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, Maduka ya Michenzani (Michenzani Shopping Mall) na barabara mbali mbali za Unguja na Pemba zilizojengwa kwa kiwango cha lami.

Rais Dk. Mwinyi alitoa salamu za mwaka mpya kwa wananchi wote wa Tanzania pamoja na kutoa salamu hizo kwa viongozi wa nchi marafiki, Taasisi za Kimataifa na washirika mbali mbali wa maendeleo. “Tunamuomba Mola wetu aujaalie kheri na baraka nyingi mwaka mpya wa 2021”, alisisitiza Rais Dk. Mwinyi katika hotuba yake hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news