Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesisitiza kwamba Serikali ya Awamu ya Nane itashirikiana vyema na sekta binafsi ili kuhakikisha uchumi wa Zanzibar unaimarika zaidi, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi (katikati) alipokuwa akizungumza na ujumbe wa Bodi ya Jumuiya ya Wafanyabiashara (ZNCC) ukiongozwa na Kaimu Mwenyekiti Nd.Ali S.Amour (wa saba kushoto) katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.
Rais Dkt.Hussein Mwinyi ameyasema hayo leo Desemba 14, 2020 Ikulu jijini Zanzibar wakati alipokutana na Ujumbe wa Bodi ya Jumuiya ya Wafanyabiashara Zanzibar (ZNCC), kufuatia muendelezo wa mkutano mkuu wa wafanyabiashara wa Zanzibar, uliofanyika huko ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil, Kikwajuni jijini Zanzibar mnamo Disemba 5, 2020.
Katika maelezo yake Rais Dkt.Hussein Mwinyi amesema kuwa, azma yake ni kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi katika kuimarisha uchumi wa Zanzibar ikiwa ni pamoja na kuwawekea mazingira mazuri wafanyabiashara.
Amewataka kutoa ushauri juu ya mamlaka za udhibiti zipo nyingi ambazo zimekuwa zikileta mkanganyiko katika ulipaji wa kodi na kusisitiza haja ya mamlaka hizo kuwa pamoja na kuwa katika eneo moja ili kuondoa usumbufu.
Amesisitiza azma yake kwa Mamlaka ya Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA) katika kuhakikisha inajumuisha masuala yote muhimu kwa wawekezaji ambapo wahusika wote ni lazima wawepo pamoja ili kurahisisha shughuli zao ikiwa ni pamoja na utoaji wa vibali kwa wawekezaji.
Hivyo, Rais Dkt. Hussein Mwinyi ameeleza haja ya sekta binafsi kutoa ushirikiano wake kwa kutoa ushauri ili kuhakikisha mamlaka hiyo ya ZIPA, inafanya kazi vyema katika kuwasaidia wawekezaji.
Ameeleza haja ya kuwepo kwa mawasiliano kati ya sekta binafsi na Serikali kwa kujadiliana pamoja katika kuzitafutia ufumbuzi changamoto zilizopo na kueleza haja kwa bodi hiyo kutafuta uwezo wa kuondoa matatizo katika sekta ya biashara kwa kupanga mambo vizuri.
Ameeleza umuhimu kwa kufanya kazi kati ya sekta binafsi na sekta ya umma na kuwekwa watu wenye utaalamu katika kazi wanazozifanya.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (kulia) alipokuwa akizungumza na ujumbe wa Bodi ya Jumuiya ya Wafanyabiashara (ZNCC) ukiongozwa na Kaimu Mwenyekiti Nd.Ali S.Amour katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.
Kwa upande wa uimarishaji wa viwanda vya ndani, Rais Dkt.Hussein ameeleza haja ya kuvilinda viwanda vya ndani ikiwa ni pamoja na kulipa kodi ili kupatikana uwezo wa kuviendeleza na hatimae kuweza kuwasaidia wananchi wa Zanzibar hasa katika sekta ya ajira.
Aidha, Rais Dkt.Hussein Mwinyi amesisitiza haja katika kuwasaidia wakandarasi wa kizalendo ili kampuni zao ziweze kufanya kazi vyema hapa Zanzibar badala ya kuyatumia makampuni kutoka nje hata kwa kazi ndogo hasa ikizingatiwa kwamba wakandarasi wa kizalendo walio wengi kampuni zao hazina uwezo mkubwa.
Ameeleza, umuhimu wa vyuo vikuu vyote kuweka mitaala inayohusiana na suala zima la ‘Uchumi wa Buluu’, ili kuwepo kwa matayarisho ya kuelekea katika uchumi huo kama vile sera zinavyoelezea kwani watendaji wakuu wa uchumi huo wanatarajiwa kutoka huko.
Halikadhalika Rais Hussein Mwinyi amesema kuwa, elimu ya kutosha inahitajika katika kuuelezea na kuufahamu ‘Uchumi wa Buluu’, hivyo muongozo unahitajika hasa kwa upande wa wanawake ili nao wajijue kuwa ni sehemu ya uchumi huo.
Baadhi ya wajumbe wa Bodi ya Jumuiya ya Wafanyabishara (ZNCC) wakimsikiliza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani) wakati wa mazungumzo yaliyofanyika leo katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar. (Picha zote na Ikulu).
Ameeleza, azma yake ya kuanzisha utaratibu maalum wa kupokea changamoto kutoka kwa wananchi na hatimae changamoto hizo kupatiwa ufumbuzi kwa utaratibu maalum utakaowekwa.
Rais Dkt.Hussein Mwinyi ameahidi kufanya mikutano na sekta zote za biashara na kuwataka wajiandae ili watakapokutana waweze kutoa changamoto zao ambapo Serikali kwa upande wake itaangalia namna ya kuzitafutia ufumbuzi hatua ambayo alisema ni nzuri kuliko kufanya kazi kwa makongamano na semina ambazo hazina tija.
Amewasisitiza wafanyabiashara kulipa kodi huku akisema kuwa kodi maalum zimewekwa Zanzibar ili kuwasaidia Wazanzibari kupata unafuu katika bidhaa zao licha ya kuwa bado wananchi wa kawaida hawanufaiki.
Kwa upande wa pili amesema kuwa, kwa upande mwingine kodi kwa Zanzibar imeshushwa hivyo ni vyema viongozi hao wakawataka wafanyabiashara kulipa kodi kwani kodi hiyo ndio inayosaidia kuimarisha sekta za maendeleo ikiwemo elimu, afya na nyinginezo huku akiwataka wafanyabiashara kuwahurumia wananchi wa Zanzibar.
Amewataka wafanyabiashara wazungumze juu ya kuwasaidia wanyonge sambamba na kufikia malengo katika kujenga nchi.
Amesema kuwa, ipo haja ya kuangaliwa tena katika suala zima la mikataba kwani kuna baadhi ya mikataba serikali haipati mapato yanayostahiki.
Amepongeza azma ya sekta binafsi kuwasaidia vijana walioko vyuoni kufanya mazoezi ya masomo katika sekta binafsi zikiwemo hoteli na kampuni nyingine za ujenzi.
Sambamba na hayo, Rais Hussein Mwinyi ameahidi kukutana na wafanyabiashara wa kila sekta, alieleza kuwa changamoto zao ni nini na ufumbuzi unatokana na nini na hiyo ni mwanzo wa majadiliano kati ya Serikali na wafanyabiashara huku akisisitiza haja kwa wafanyabiashara kushauri juu ya ukusanyaji na ulipaji wa kodi.
Mapema wajumbe hao wameeleza azma yao ya kushirikiana na Serikali katika kuimarisha sekta ya biashara hapa Zanzibar na kupongeza hotuba ya Rais Dkt.Hussein Mwinyi aliyoitoa katika mkutano wa wafanyabiashara uliofanyika Disemba 5, mwaka huu 2020 huko katika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakil, Kiwkajuni Jijini Zanzibar.
Kwa upande wake Kaimu Mwenyekiti wa jumuiya hiyo ya Wafanyabiashara Zanzibar (ZNCC), Ali Amour alieleza jinsi wafanyabiashara walivyofarajika na utayari wa Serikali anayoiongoza Rais Dkt. Hussein mwinyi katika kushirikiana pamoja kuinua uchumi wa Zanzibar.
Amesema kuwa, Rais Dkt. Hussein Mwinyi ameonesha azma ya ushirikiano kati ya sekta binafsi na sekta ya umma huku akieleza kwamba wataitumia hotuba hiyo katika vikao vyao kama dira ya kuwapeleka kwenye lengo lililokusudiwa.
Ameeleza jinsi hapo siku za nyuma walivyokuwa wakifanya mikutano mingi ambayo haikuwa na tija hata kidogo huku akiahidi kuwa jumuiya hiyo itafuata nyayo za Rais Dkt. Hussein Mwinyi katika suala zima la ufuatiliaji na utekelezaji katika sekta ya biashara hapa nchini.
Nao wajumbe wa bodi hiyo wameeleza haja ya wafanyabiashara kulipa kodi na kuahidi kufanya makongamano ili kuhamasisha ulipaji wa kodi huku wakieleza haja kwa sekta binafsi kushirikishwa katika upangaji wa kodi.
Sambamba na hayo viongozi hao wa ZNCC wameeleza matumaini yao kwa Rais Dkt. Hussein Mwinyi na kuahidi kuendelea kumuunga mkono kwa lengo la kuhakikisha uchumi wa Zanzibar unaimarika na wananchi wake nao wanaimarika zaidi.
Tags
Zanzibar