Rais mstaafu wa Burundi, Pierre Buyoya afariki

Mheshimiwa Pierre Buyoya (71) ambaye aliwahi kuwa Rais wa Jamhuri ya Burundi Pierre Buyoya amefariki dunia kutokana na maambukizo ya virusi vya ugonjwa wa corona (COVID-19), anaripoti Mwandishi Diramakini (Mashirika).
Kwa mujibu wa vyombo mbalimbali ya habari za Kimataifa vilivyonukuliwa na Mwandishi Diramakini vimebainisha kuwa, Mheshimiwa Buyoya alipatwa na virusi hivyo akiwa mjini Bamako, Mali. 

Vyombo hivyo vya Magharibi mwa Afrika vimesisitiza kuwa, baada ya Mheshimiwa Buyoya kugundulika kuwa ana virusi hivyo, alilazwa hospitalini kwa wiki moja mjini humo akipewa huduma za afya ingawa matokeo hayakuwa mazuri.

Kwa mujibu wa vyombo hivyo, baada ya hali yake kuwa mbaya ghafla alisafirishwa kwa ndege yenye matibabu mjini Paris, Ufaransa usiku wa Desemba 17, 2020 lakini alifariki dunia baada tu ya kuwasili nchini Ufaransa kabla ya kufikishwa hospitali iliyokusudiwa. 

Wiki tatu zilizopita, Buyoya alijiuzulu kwenye wadhifa wake kama mwakilishi maalum wa Umoja wa Afrika nchini Mali na katika kanda ya Sahel, akisema alifanya hivyo ili aandae utetezi wake katika kesi ya mauaji ya mtangulizi wake Melchior Ndadaye iliyokua inamkabili. 

Alijiuzulu kwenye wadhifa huo ambao alikuwa anashikilia tangu mwaka 2012 baada ya kuhukumiwa na Mahakama ya Juu ya Burundi kifungo cha maisha jela, katika kesi ilioendeshwa bila yeye mwenyewe kuwepo ingawa alikana tuhuma hizo.

Mheshimiwa Buyoya aliiongoza Burundi mara mbili kuanzia mwaka 1987 hadi 1993, alipokabidhi madaraka kwa rais wa kwanza kutoka Kabila la Wahutu Melchior Ndadaye ambaye alimshinda kwenye uchaguzi.Ndadaye aliuawa katika mapinduzi ya kijeshi baada ya kuongoza kwa miezi mitatu. 

Buyoya alirudi tena madarakani mwaka 1996 katika mapinduzi ya kijeshi dhidi ya Rais Sylvestre Ntibantunganya na kuongoza hadi mwaka wa 2003.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news