Rais Xi Jinping wa China ampigia simu Rais Magufuli wa Tanzania

Rais wa  Jamhuri ya Watu wa China, Xi Jinping leo Desemba 15, 2020 amempigia simu Rais Dkt.John Magufuli ambapo viongozi hao wamezungumzia kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania hususani katika masuala ya uchumi, anaripoti Mwandishi Maalum Diramakini.
Katika mazungumzo hayo yaliyodumu kwa muda wa saa moja,  Rais Xi Jinping amempongeza, Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kipindi cha pili.

Pia ameeleza kuwa, kuchaguliwa kwake kumetokana na kazi nzuri iliyofanywa katika kipindi cha miaka 5 ya kwanza ambapo uchumi umeimarika zaidi na kwamba anaiona Tanzania kuwa nchi itakayoongoza kwa ukuaji wa uchumi Barani Afrika.

 Xi Jinping amempongeza Rais Magufuli kwa namna Tanzania ilivyokabiliana na ugonjwa wa Korona (Covid-19) na ameeleza jinsi China inavyoendelea kukabiliana na ugonjwa huo.

Amempongeza Rais Magufuli kwa utekelezaji mzuri wa miradi ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (standard gauge railway) na ujenzi wa bwawa la kuzalisha megawati 2,115 za umeme katika mto Rufiji (Bwawa la Mwl. Nyerere) na ameeleza kuwa China itaangalia namna ya kushirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa miradi hiyo mikubwa.
Kwa upande wake,  Rais Magufuli amemshukuru, Rais Xi Jinping kwa kumpigia simu, kumpongeza kwa kuchaguliwa kwake kuiongoza Tanzania kwa kipindi cha 2 na kumpongeza kwa hatua za kimaendeleo zinazopigwa na Tanzania hasa katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati.

Rais Magufuli amemhakikishia, Rais Xi Jinping kuwa Tanzania itaendeleza na kukuza zaidi uhusiano wake na China uliodumu kwa takribani miaka 55 baada ya kuasisiwa na Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Hayati Mwenyekiti Mao Zedong, na kwamba Tanzania itaendelea kuiunga mkono China katika masuala mbalimbali ya kimataifa.

Rais Magufuli amesema, Tanzania inawakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka China kuja kuwekeza katika maeneo mbalimbali ya uzalishaji, utalii, ujenzi na biashara kwa manufaa pande zote mbili.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza kwa njia ya Simu na Rais wa China Xi Jinping Ofisini kwake Ikulu, Chamwino mkoani Dodoma leo tarehe 15 Desemba 2020. (PICHA ZOTE NA IKULU).

Aidha, Rais Magufuli ameiomba China kushirikiana na Tanzania katika uwekezaji wa miradi mikubwa kwa kutoa mikopo nafuu na ameitaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni wa kuzalisha megawati 358 za umeme katika mto Ruhudji, Megawati 222 za umeme katika mto Rumakali na ujenzi wa barabara Visiwani Zanzibar.

Halikadhalika, Rais Magufuli ameiomba China kufungua zaidi masoko ya bidhaa mbalimbali kutoka Tanzania hususani mazao mbalimbali ya kilimo.

Rais Xi Jinping ameahidi kufanyia kazi maombi yaliyotolewa na Mhe. Rais Magufuli ikiwemo ujenzi wa miradi ya kuzalisha umeme ya Ruhudji na Rumakali, ujenzi wa reli, Bwawa la Nyerere na ununuzi wa mazao ya Tanzania.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news