Ripoti ya polisi yaanika matukio yaliyotikisa 2020

Ripoti ya Jeshi la Polisi nchini imebainisha kuwa, mauaji yanayotokea kwa kiasi kikubwa nchini yanahusiana na wivu wa mapenzi kutokana na wananchi kujichukulia sheria mkononi, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Kwa mujibu wa ripoti ya Jeshi la Polisi kuhusiana na matukio yaliyotokea mwaka huu iliyotolewa jijini Dodoma na Kamishna wa Operesheni na Mafunzo Makao Makuu ya Polisi, Liberatus Sabas imebainisha kuwa, kwa kiasi kikubwa mauaji yanayotokea kwa sasa nchini ni wivu wa mapenzi na wananchi kujichukulia sheria mkononi. 

Amesema, kutokana na hali hiyo Jeshi la Polisi limefanikiwa kutoa elimu kwa wananchi kutokujichukulia sheria mkononi, huku likiwataka viongozi wa dini kuingilia kati katika kutoa elimu kusaidia kupunguza mauaji yatokanayo na wivu wa mapenzi, kwani wengi ni waumini wa madhebu yao na wanawasikiliza sana.

Kamanda Sabas alitaja matukio mengine yaliyotikisa mwana huu kuwa ni kuungua moto shule, "Miongoni mwa matukio yalioshika kasi na nafasi kubwa mwaka huu ilikuwa ni kuungua kwa majengo ya shule na hii imetokana na sababu tofauti ambazo ni hitilafu za mmeme,"amesema.

Aidha, amesema sababu nyingine ni migogoro shuleni na uzembe, huku shule za watu binafsi zikiwemo taasisi za didini zilizoungua moto zikiwa ni 20 na za Serikali zikiwa ni 11 na kufanya idadi ya shule zilizoungua kuwa 31 kuanzia Januari hadi Novemba, mwaka huu. 

Sabas amesema, kumekuwa na matukio ya wanafunzi kuacha masomo na kujiunga na makundi ya kihalifu. 

Amesema,Jeshi la Polisi nchini linawaomba wazazi na walezi kufuatilia nyendo za watoto wao, kwani kumekuwa na wimbi kubwa la watoto kuacha shule na kwenda kujiunga na makundi ya kihalifu.

Pia amesema, miongoni mwa wahalifu hao ni wale waliokuwa Kibiti mkoani Pwani na hatimae baada ya kupigwa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama walikimbilia nchi jirani ya Msumbiji.

Kamishna Sabas amesema hadi sasa wapo wanafunzi waliokuwa wameacha shule na kujiunga na vikundi vya kihalifu ambao wamekamatwa wakiwa wanavuka kuelekea nchini Msumbiji na wengine tayari wameishafanikiwa kuvuka kuingia nchini humo.

Aidha , Kamishna Sabas amesema, licha ya kuwataka wazazi kuwalinda na kufuatilia mienendo ya watoto wao amewataka wananchi kuchukua tahadhari wakati huu wa kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka kwani Jeshi la Polisi kwa kushiliriana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama vimejipanga kikamilifu kukabiliana na uhalifu.

Akizungumzia ajali za barabarani kwa mwaka 2019 na 2020, Kamanda Sabas amesema Januari hadi Novemba 2019 matukio ya ajali yalikuwa 2,722 ambazo zilizosababisha vifo ni 1,117.

Pia amesema waliokufa ni 1,329 huku majeruhi wakiwa 2,717. Kwa mwaka huu amesema, kuanzia Januari hadi Novemba 2020 matukio ya ajali 1,800, ajali za vifo 935, waliokufa 1,158 na majeruhi 2,089, huku kukiwa na utofauti wa matukio ya ajali 922 sawa na asilimia 33.9, ajali za vifo 182 sawa na 16.3, waliokufa 171 sawa na asilimia 12.9 na waliojeruhiwa 628 sawa na asilimia 23.1. 

Amesema hali ya ulinzi na usalama wa nchi imeendelea kuwa shwari kutokana na kazi kubwa inayofanywa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama.

Hata hivyo, Sabas amesema kuwa,jeshi limepata ushirikiano mkubwa kutoka kwa wananchi wapenda amani/raia wema ambao wamekuwa wakitoa taarifa za uhalifu pamoja wahalifu kwa Jeshi la Polisi nchini licha ya kuwa yapo matukio machache yamekuwa yakijitokeza ambayo ni tofauti na matukio ya kipindi cha huko nyuma.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news