Vijana wa Tanzania wameendelea kuonyesha kandanda safi, baada ya leo Desemba 14, 2020 Serengeti Boys kuichapa Rwanda 3-1, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Mtanage huo umepigwa katika dimba la Umuganda uliopo Rubavu nchini Rwanda ambapo wao walikuwa wageni.
Aidha, mabao ya Serengeti Boys leo yamefungwa na Kassim Yahya dakika ya 10 na Omar Abbas dakika ya 14 na 61, wakati la Rwanda limefungwa na Irihamye Eric kwa penalti ndani ya dakika ya 18.
Kwa sasa Serengeti Boys watacheza dhidi ya Djibouti endapo wakishinda ama kutoa sare watakuwa wamefuzu kucheza hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo ambapo bingwa wa CECAFA U17 atacheza fainali za AFCON U17 zitakazofanyika Julai, 2021 nchini Morocco.
Wakati huo huo, kaka zao timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20, Ngorongoro Heroes leo imefungwa 1-0 na wenyeji, Saudi Arabia katika mchezo wa kirafiki Uwanja wa Chuo Kikuu cha Prince Muhammad Bin Fahd mjini Khobar nchini humo.
Huo ni mwendelezo wa mechi za kirafiki, kwani baada ya kupata tiketi ya kucheza michuano ya Africa kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20 walikwea pipa hadi Saudi Arabia kuweka kambi.
Mchambuzi wa masuala ya michezo, chumba cha habari cha Diramakini amemueleza Mwandishi Diramakini kuwa, huenda matokeo ya leo kutoka kwa Saudi Arabia ni ya kisasi kwani mwishoni mwa wiki vijana hao waliwachapa 1-0.
Chini ya kocha wao Jamhuri Kiwelu (Julio), Ngorongoro Heroes wanaendelea na maandalizi ya kujiweka sawa kwa ajili ya michuano ya AFCON U-20 yanayotarajiwa kufanyika nchini Mauritania 2021.
Aidha, vijana wa Ngorongoro walifuzu kucheza AFCON U-20, baada ya kufanikiwa kutinga fainali ya michuano ya CECAFA U-20 iliyomalizika Desemba 2, 2020 wilayani Karatu,Arusha.
Wao walichukua nafasi ya pili baada ya Uganda kuwapachika mabao 4-0 kwenye mtanange huo wa fainali ambo vijana walionyesha kandanda safi tangu awali.