Kaimu Waziri wa Afya Ustawi wa Jamii Jinsia na Watoto ambae pia ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mhe. Simai Mohammed Said amesema kuwa na bidhaa bora na zenye kiwango imara kutapelekea taifa kuwa na jamii yenye afya imara, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Amesema hayo wakati alipofanya ziara ya kushtukiza katika ofisi za Wakala wa Chakula na Dawa (ZFDA) na kukagua shughuli mbalimbali zilizopo chini ya ofisi hiyo huko Mombasa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.
Amesema, ili jamii ihakikishe inatumia bidhaa bora ipo haja ya kuhakikisha kuwa bidhaa zinafanyiwa ukaguzi kabla ya matumizi.
Aidha,amewataka watendaji wa ZFDA kuwa na ushirikiano mzuri katika kazi ili kuendelea kuimarisha huduma za upatikanaji wa bidhaa zilipo kwenye kiwango kizuri kwa ajili ya matumizi ya binadamu.
Kwa upande wao watendaji wa mamlaka ya chakula na dawa ZFDA wamempongeza Mhe. Simai kwa kujionea utendaji kazi kwa mamlaka yao jambo ambalo linaashiria ushirikiano wa karibu baina ya viongozi na watendaji wa chini.
Katika ziara hiyo kaimu Waziri wa Afya Ustawi wa Jamii Jinsia na Watoto, Mhe, Simai Mohammed Said alitembelea ghala la kuhifadhi chakula lijukanalo kwa jina la Zenji General Merchandise lilipo Mombasa Unguja.