Serikali yawataka wahitimu wa vyuo kujiandaa kufanya kazi kwa bidii

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Seleman Jafo ametoa wito kwa wahitimu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini kujiandaa kufanyakazi kwa bidii na kuleta mabadiliko katika jamii pale wanapopatiwa dhamana ya kulitumikia Taifa, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Waziri Jafo ametoa wito huo leo katika mahafali ya 34 katika Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini Kampusi kuu ya Dodoma na kuwataka wahitimu hao kujiaanda kisaikolojia kwenda kulitumikia taifa linalokuwa kwa kasi kimaendeleo.

“Nendeni mkafanye kazi, Nendeni mkawajibike, mkawe mfano kwa jamii ambayo mtaitumikia na kuleta mabadiliko, msijikweze kwa ajili ya elimu mliyonayo bali mkawasaidie wananchi katika kuleta maendeleo, hii ndio ikawe nguzo yenu,” amesisitiza Waziri Jafo

Amesema kuwa chuo cha Mipango kimewajenga katika misingi ya umahiri ambao unawasaidia wahitimu katika Soko la ajira na kukuza uchumi wa nchi, hivyo fanyeni kazi kwa umakini na ubunifu mkubwa pale unapopatiwa nafasi katika Sekta binafsi au Serikalini ili kulinda heshima ya chuo hicho.

Amewataka Wahitimu kushirikiana na jamii katika masuala ya maendeleo kwa kuwa waaminifu ili jamii ijivunie kuwa na wasomi wabobezi ambao wataleta chachu ya maendeleo katika maeneo yao.

Waziri Jafo ameendelea kufafanua kuwa wahitimu watakaopata nafasi ya kulitumikia Taifa wahakikishe wanafanyakazi kwa weledi na uaminifu mkubwa ili kuacha alama na kumbukumbu kwenye maeneo yao ya kazi.

Aidha, amewataka wahitimu hao kuhakikisha wanatunza amani ya nchi ili Taifa liweze kufanya shughuli zake za kimaendeleo kwa malengo yaliyo kusudiwa.

Kwa upande wake Mkuu wa chuo cha Mipango ya maendeleo vijijini Prof. Hozen Mayaya amesema katika mwaka wa masomo 2018/2019 kwa kampasi kuu pekee kumekuwa na ongezeko la udahili wa wanafunzi wapya kutoka wanafunzi 4,317 mwaka 2019/2020 hadi wanafunzi 5,856 ikiwa ni ongezeko asilimia 26.

Ameeleza kuwa wahitimu waliomaliza masomo yao mwaka huu ni wanafunzi 4072 ambapo kati ya hao wanaume ni 1.756 na wanawake 2, 316 ambapo ni ongezeko la asilimia 27 ukilinganisha na wahitimu wa mwaka 2018.

Kwa kuongezea Prof. Mayaya amesema kuwa chuo kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo kimeendelea kutekeleza miradi mbalimbali yenye lengo la kuboresha hali maisha ya wananchi ikiwa ni pamoja mradi wa kuboresha ustahimilivu wa jamii za wafugaji na wakulima wa Serengeti kwa ajili ya kupunguza migogoro ya Rasilimali za kiikolojia na nyingine zinazofanana na hizo(2019-2023).

“Miradi mingine ni mradi wa kuwajengea uwezo watumishi wa mamlaka za serikali za Mitaa za serikali ya mapinduzi Zanzibar(Agosti 2018-Julai 2021),mradi Wa kuwajengea uwezo watumishi wa wizara ya mamlaka za serikali za Mitaa Katika uandaaji mipango na bajeti inayozingatia mahitaji ya watoto (Agosti 2018-Julai 2021)”, ameeleza Prof. Mayaya.

Hata hivyo amesema miongoni mwa miradi ni pamoja na mradi wa kuandaa mipango mikakati Tanzania Bara (Julai 2020-2021)na mradi wa tathmini ya mbinu za upangaji wa mipango ya maendeleo na uhusishaji wa programu ya O&OD Katika mitaala ya vyuo vyuo vya elimu ya juu (2020-2021).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news