Wekundu wa Msimbazi, Simba SC wameibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji, Mbeya City katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Mtanange huo wa leo Desemba 13, 2020 umepigwa katika Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya ambapo nahodha na mshambuliaji, John Raphael Bocco dakika ya 32 alimalizia pasi ya kiungo, Clotous Chama.
Bao hilo lilidumu kuanzia dakika hizo hadi tisini, hivyo Simba SC kufikisha alama 29 baada ya kucheza mechi 13 na kupanda hadi nafasi ya pili.
Kwa ushindi huo, Simba SC wanairejesha Azam FC nafasi ya tatu huku Yanga SC wakiwa kileleni kwa alama 37 wakiwa wamecheza mechi mbili zaidi kwa sasa.
Wakati huo huo,Adam Adam ndani ya dakika ya 15 kwa penalti na Edward Songo dakika ya 17 wameipa JKT Tanzania ushindi wa 2-0 dhidi ya Biashara United katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
Pia Coastal Union imelazimishwa sare ya bila kufungana na Tanzania Prisons Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga huo ukiwa ni mwendelezo wa michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Tags
Michezo