Hatimaye Tanzania imefuzu Fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 (AFCON U17) baada ya ushindi wa penalti 4-3 dhidi ya Ethiopia, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Matokeo hayo yametokana nasare ya 1-1 leo kwenye mchezo wa nusu fainali uliochezwa katika dimba la Umuganda uliopo Rubavu nchini Rwanda.
Ushindi huo unawafanya Desemba 22, 2020 kukutana na mabingwa watetezi wa Uganda katika fainali itakayochezwa ndani ya dimba hilo la Umuganda nchini humo.
The Cubs wao wameingia fainali baada ya kuitoa Djibouti mapema leo mchana hapo hapo Umuganda
Serengeti Boys sasa itashiriki Fainali za AFCON U17 kwa mara ya tatu mfululizo Julai, 2021 nchini Morocco baada ya 2017 Gabon na 2019 walipokuwa wenyeji.
Hata hivyo,Serengeti Boys, mabingwa wa CECAFA U-17 mwaka 2018 nchini Burundi, wanafuata nyayo za kaka zao, Ngorongoro Heroes waliofuzu Fainali za AFCON U-20 zitakazofanyika nchini Mauritania kuanzia Februari 14 hadi Machi 4, 2021.
Awali, Tanzania walikuwa wenyeji wa CECAFA U-20 mwishoni mwa Novemba na wakamaliza nafasi ya pili baada ya kufungwa 4-1 na Uganda Uwanja wa Black Rhino Academy, Karatu jijini Arusha Desemba 2, 2020.
Tanzania iliongoza kwa bao la mapema dakika ya 37 kupitia Omar Sultan ambalo baadaye lilisawazishwa na Ganta ndani ya dakika 69 ambalo lilidumu mpaka dakika za mwisho na baadae penaliti zikaamua mshindi.
Tags
Michezo