Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto Prof. Mabula Mchembe amewapongeza viongozi na
watumishi wa huduma za chanjo ngazi zote nchini kwa utendaji bora wa
utoaji wa chanjo kwa bidii na kuhakikisha kuwa malengo yaliyowekwa
kitaifa na kimataifa yanafikiwa,anaripoti Catherine Sungura (WAMJW)
Dodoma.
Pongezi hizo zimetolewa leo wakati akifungua mkutano wa
mwaka wa tathimini wa huduma za chanjo Tanzania unaofanyika kwenye
ukumbi wa Mt. Gasper jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Prof. Mabula Mchembe akiongea na Waganga wakuu wa Mikoa na Waratibu wa huduma za chanjo nchini wakati wa ufunguzi wa mkutano wa mwaka wa tathimini wa huduma za chanjo nchini unaofanyika jijini Dodoma.
"Niwapongeze kwa jitihada zenu na kuifanya nchi kufanikiwa katika
utoaji wa huduma za chanjo kwa kuvuka kiwango cha asilimia 90
kilichowekwa kimataifa, hivyo nawataka mkubaliane na kupanga mbinu na
mikakati ya kudumisha na kuboresha zaidi viwango vya chanjo nchini".
Hata
hivyo katibu Mkuu huyo alisema licha cha kufanikiwa huko Serikali
kupitia Wizara yake itaendelea kudumisha kiwango cha chanjo nchini na
ana uhakika takwimu za mwaka 2020 zitakapotolewa na Shirika la Afya
Duniani(WHO) itafikia asilimia 98 au zaidi.
Waganga Wakuu wa Mikoa na Waratibu wa chanjo nchini wakimsikiliza mgeni rasmi wakati wa ufunguzi wa mkutano huo ambao lengo lake ni kuangalia hatua zipi wamefikia katika kuwafikia watoto.
Mkurugenzi wa Huduma za Afya,Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Rais-TAMISEMI Dkt. Ntuli Kapologwe akiongea na viongozi na waratibu wa chanjo nchini.
Licha ya pongezi hizo Prof. Mchembe amewaagiza viongozi wa afya ngazi
za Mikoa na wilaya kuhakikisha kuwa huduma za chanjo zinapewa
kipaumbele ili usitokee tena mkoa utakaoshindwa kudumisha kiwango
kilichofikiwa kwani ili watoto waendelee kuwa na afya njema hakuna budi
kuwapa chanjo bora za kuwakinga dhidi ya maradhi.
"Nchi yetu
imekuwa na utekelezaji wa mkakati wa Fikia kila Wilaya,Fikia kila mtoto
apate chanjo,nawasisitiza waratibu wa huduma za chanjo kuhakikisha kuwa
mikoa inayofanya vibaya inatumia mkakati huu ili kuhakikisha kuwa
watoto na walengwa wote wanafikiwa katika kupata haki yao ya msingi ya
chanjo".
Mwakilishi wa Wadau wa Maendeleo ambaye ni mwakilishi kutoka Shirika la Afya Dunia(WHO) Bw.Nasoro Mohamed akitoa salamu kwa niaba ya wadau wa chanjo nchini.
Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Kinga kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Leonard Subi akiongea kwenye mkutano huo.
Aidha, Prof. Mchembe amewashukuru wadau wote wa maendeleo kwa michango yao mbalimbali katika kuhakikisha kwamba watoto wanapatiwa chanjo bora ambayo inaleta kinga dhidi ya maradhi ambayo yanaweza kusababisha ulemevu na vifo kwa watoto.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Rais-TAMISEMI Dkt. Ntuli Kapologwe amewapongeza Waganga Wakuu wa Mikoa pamoja na waratibu wa huduma za chanjo nchini kwa kuwa kinara wa utoaji wa chanjo na kuweza kuwafikia walengwa wote nchini na kuongoze kuwa TAMISEMI inaipa uzito mkubwa suala la chanjo kwani kinga ya mtoto inaanza na chanjo.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Serikali ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya kinga Kutoka Wizara ya afya, Dkt. Leonard Subi amesisitiza kuwa wizara ya afya inasimamia ubora na usalama wa huduma wanazozitoa hasa upande wa chanjo ambao mara kadhaa umekua na mapokeo tofauti,hivyo amesisitiza kuwa wizara ipo makini zaidi na afya za wananchi
Wakati huo huo Mwakilishi wa wadau wa maendeleo ambaye anatoka WHO Nassoro Mohamed ameipongeza Wizara ya afya pamoja na viongozi wa mikoa kwa kuhakikisha watoto wote nchini wanafikiwa licha ya changamoto za hapa na pale hivyo kama wadau wanashiriki ili kuhakikisha Serikali inafikia malengo waliyojiwekea katika kutoa huduma za chanjo.