Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema kuanzia sasa viongozi wote wa utumishi wa umma watakaotuhumiwa kuhusika na vitendo vya rushwa pamoja na ukiukwaji wa maadili, watasimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi, anaripoti Mwandishi Maalum Diramakini (Zanzibar).
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi (kulia) alipokuwa akitoa hotuba yake kwa viongozi mbalimbali katika Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu yaliyofanyika leo katika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakil Kikwajuni jijini Zanzibar (Picha na Ikulu).
Dkt. Mwinyi amesema hayo leo Desemba 29, 2020 katika Ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdul-wakili Kikwajuni jijini hapa, wakati alipozungumza na viongozi, watendaji na wafanyakazi wa utumishi wa umma katika kilele cha maadhimisho ya siku ya Maadili na Haki za Binadamu.
Amesema, mara tu baada ya kuingia madarakani, Serikali imeanza kuwachukulia hatua za kisheria viongozi wasiowajibika na wasioshikamana na maadili ya kazi zao, kufuatia ziara zilizofanyika katika taasisi mbalimbali, ikiwemo Bandari, Hospitali ya Mnazi Mmoja na maeneo mengine yaliomo katika Mpango wa Utekelezaji wa Mradi wa Kuendeleza huduma Mjini (ZUSP).
Amesisitiza na kurejea maelezo aliyoyatoa kwa nyakati tofauti dhidi ya watendaji waliohusika au kutiliwa shaka ya kuhusika na vitendo vya rushwa na ukiukwaji wa maadili kuwa, Serikali anayoiongoza itakabiliana ipasavyo na vitendo vyote vinavyoathiri utekelezaji wa misingi ya utawala bora.
Amesema, anafurahishwa na hatua ya wananchi ya kuiunga mkono Serikali na kubainisha kuwa yeyote yule atakayetuhumiwa na hatimaye kubainika hana kosa, atarejeshwa kazini na kupata haki zake kama sheria zinavyoelekeza.
“Kiongozi wa umma lazima afanye kila linalowezekana kuwa mfano na kigezo cha tabia njema na ajiepushe hata na vitendo vinavyoweza kumfanya atiliwe shaka,”amesema.
Dkt. Mwinyi amesema, ni jambo la kusikitisha kuona taarifa iliyowasilishwa kwake kutoka ZAECA , kuonyesha kuwepo tatizo kubwa la ubadhirifu wa mali za Serikali na wizi katika utekelezaji wa miradi mikubwa.
Hata hivyo amesema, amefurahishwa na kazi inayoendelea ya ufuatiliaji, hivyo akawataka viongozi wote watakaotuhumiwa kuhusika na ubadhirifu huo kutoa ushirikiano wa kisheria kwa chombo hicho.
“Nimevutiwa sana na ari na utayari wa watendaji wa ZAECA katika kufanikisha vita dhidi ya rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma, tutayazingatia maombi yao waliyotueleza,”amesema.
Aidha, amesema anatambua hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali kuwa hazitawafurahisha watu wote, hivyo akawataka wananchi kuikubali hali hiyo kwa msingi kuwa wengi wataguswa, akibainisha nchi kughubikwa na muhali.
Amesema, kuna miradi kadhaa mikubwa inayoonyesha kuwepo matumizi makubwa ya fedha, ambazo hazikutumika vyema (kwa mujibu wa taratibu).
Amesema, wale wote watakaobainika kuhusika na uzembe, wizi au ubadhirifu wa mali ya umma, mahali popote walipo watachukuliwa hatua na kusisitiza azma ya Serikali katika kuzingatia haki na kuepuka uonevu.
Amepongeza kazi kubwa iliyofanywa na awamu zote za Serikali zilizotangulia ya kuunda taasisi na kutunga sheria bora katika kufanikisha dhana ya uimarishaji utawala bora, akinasibisha hatua hiyo kuwa ni ujenzi wa miundombinu iliyo bora.
Ameeleza kuwa, serikali imefanikiwa kuanzisha Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, Idara ya Utawala Bora, Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi, Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma pamoja na kuimarisha Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ili kutekeleza majuku yake kwa ufanisi.
Amesema, ni jambo lisilopendeza na kukubalika kwa wananchi, inapotokea fedha nyingi za Serikali kupotea kimya kimya wakati Ofisi ya Mdhibiti Mkuu wa Serikali ipo, ikiwa na majengo na vifaa vya kisasa pamoja na watendaji wa kutosha.
“Halitokuwa jambo la maana hata kidogo kuwepo Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka yenye kulalalmikiwa na kuonekana kikwazo katika kutafuta ushahidi wa kesi mbalimbali,”amesema.
Aidha, Dkt. Mwinyi amesema, Serikali imeunda Tume ya Madili ya Viongozi wa Umma, ambapo miongoni mwa majukumu yake ni kuhakikisha viongozi wote wa umma waliotajwa na sheria ya maadili (Namba 4 ya mwaka 2015) wanajaza na kuwasilisha fomu ya tamko la rasilimali na madeni.
Amechukua fursa hiyo kuwakumbusha viongozi wote waliotajwa chini ya sheria hiyo; kwa mujibu wa vyeo na nafasi zao kuhakikisha wanajaza fomu hizo sio zaidi ya Disemba 30, 2020 na kuzirejesha Ofisi ya Tume ya Maadili kwa wakati uliowekwa na sheria.
Akigusia juu ya kauli mbiu ya maadhimisho hayo “Tuimarishe utoaji wa huduma za jamii kwa kuzingatia maadili, kuheshimu haki za binadamu na mapambano dhidi ya rushwa,”Dkt. Mwinyi alisema inaendana na wakati uliopo ambapo Serikali imeongeza kasi katika kusimamia haki za binadamu , sambamba na uimarishaji wa huduma za jamii.
Amewataka washiriki wa mkutano huo kuyatumia maadhimisho hayo kutafakari umuhimu wa kuendeleza maadili mema ndani ya jamii, sambamba na kupiga vita vitendo vya udhalilishaji wa watoto na unyanyasaji wa kijinsia.
Aidha, amewataka kushirikiana na jamii katika kukomesha vitendo hivyo pamoja na kuendeleza matumzii mazuri ya mitandao, sambamba na kupiga vita utumiaji wa dawa za kulevya.
Mapema, Waziri wa Nchi (OR) Katiba,Sheria,Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman, alitoa wito kwa wananchi kuunga mkono juhudi za Rais wa Zanzibar katika kuimarisha Utawala Bora pamoja na kulaani kwa nguvu zote vitendo vya rushwa.
Aidha, amewataka watumishi wote wa Serikali kudhibiti siri za Serikali na kubainisha hatua zitachukuliwa dhidi ya watumishi wasio waaminifu watakaovujisha siri hizo.
Nae Mwenyekiti wa Tume ya Madili ya Viongozi wa Umma, Asaa Ahmada Rashid alisema, maadhimisho hayo ni muhimu kwani yanaongeza uelewa kwa wananchi juu ya dhana ya utawala bora na misingi yake, ikiwemo mapambano dhidi yarRushwa, haki za binadamu, uwajibikaji, uwazi, uadilifu na athari ya mgongano wa maslahi.
Amesema, kuimarika kwa misingi hiyo kutaisaidia jamii kuzitambua na kupata haki za msingi ili kuendeleza ustawi wa maisha yao, kupunguza umasikini pamoja na kukuza uchumi.
Amesema, kuna mafanikio makubwa yaliopatikana katika utendaji wa taasisi hizo, ikiwemo utoaji wa elimu kwa umma juu ya umuhimu wa maadili kwa viongozi wa umma, mapambano dhidi ya rushwa, ubadhirifu, matumzii mabaya ya fedha na rasilimali za umma.
Aidha, ameipongeza hatua ya Serikali ya kupitisha na kusimamia utekelezaji wa Mkakati Shirikishi wa Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi (ZISAECA) kuwa ni wa kupigiwa mfano na unaopaswa kupongezwa.
Viongozi mbalimbali wa Kitaifa na kijamii wamehudhuria mkutano huo, akiwemo Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdalla, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Dkt. Abdulhamid Yahya Mzee.
Wengine ni Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Dkt. Mwinyi Talib Haji, mawaziri, wakuu wa vikosi vya SMZ, viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa dini pamoja na wafanyakazi wa utumishi wa umma.