Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa siku saba kuanzia leo Desemba 17,
2020 kwa Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, maofisa wanaochambua maombi
ya ununuzi wa magari Ofisi ya Waziri Mkuu na wakurugenzi wa Jiji la
Mwanza, Halmashauri ya Wilaya ya Chato, Msalala na Kahama wajieleze kwa
sababu gani magari hayo yalinunuliwa kwa gharama kubwa, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Ametoa
agizo hilo leo Desemba 17, 2020 wakati akizungumza na watumishi wa
umma,waheshimiwa wabunge, madiwani katika jiji la Mwanza na Manispaa za
Ilemela na Nyamagana katika hoteli ya Malaika jijini Mwanza. Amesema
magari hayo ni mzigo kwa wananchi.
Waziri Mkuu amesema hayo ni
matumizi mabaya ya fedha za umma na haiwezekani viongozi hao watumie
magari ya gharama kubwa badala ya kutumia fedha hizo kwa ajili ya
maendeleo ya wananchi na ametaka muongozo wa ununuzi wa magari
uliotolewa na Serikali uzingatiwe.
Amesema, matumizi ya fedha za
umma lazima yasimamiwe ipasavyo na kwamba Serikali haina mzaha na
mtumishi yeyote atakayebainika kutumia vibaya fedha za umma, hivyo
amewataka madiwani wakasimamie vizuri maeneo yao.
Waziri Mkuu
amewataka wakurugenzi wahakikishe wanatoa ushauri ipasavyo katika
Mabaraza ya Madiwani kuhusu matumizi na manunuzi, pia watoe kipaumbele
katika udhibiti wa mapato na rasilimali za umma. “Wakurugenzi zingatieni
vipaumbele vya wananchi na Halmashauri zetu katika kupanga matumizi na
manunuzi na tumieni fedha za mapato ya ndani kutekeleza miradi ya
kimkakati.
Waziri Mkuu amewataka viongozi wa halmashauri waweke
mikakati madhubuti itakayowezesha makusanyo ya halmashauri zao yafikie
asilimia 100 au zaidi. “Kuweni wabunifu wa vyanzo vipya vya mapato na
ongezeni kasi ya ukusanyaji wa mapato kwenye Halmashauri zenu.”
Kadhalika,
Waziri Mkuu amewataka watumishi wa umma wahakikishe wanawafuata
wananchi hasa waishio maeneo ya vijijini walipo na kuwasikiliza kero zao
na kushirikiana nao katika kuzipatia ufumbuzi
Wakati huo huo,
Waziri Mkuu amerejea kauli yake aliyoitoa Desemba 7, 2020 ya kuwataka
Makatibu Tawala wa Mikoa yote nchini wahakikishe kuwa watumishi wa idara
nzima ya elimu hawaendi likizo mwisho wa mwaka huu, badala yake
wakasimamie ukamilishaji wa ujenzi wa vyumba vya madarasa na madawati na
wawe wamekamilisha ifikapo Februari 28, 2021.
“Watumishi wa
idara ya Elimu Maafisa Elimu Wilaya na Mkoa, Wahandisi wa ujenzi,
Maafisa Manunuzi wa Wilaya na Wakurugenzi wasipewe likizo kipindi hiki
kuelekea sikukuu ya Krismasi na Mwaka mpya hadi Februari 28, 2021 ili
wakamilishe ujenzi wa vyumba vya madarasa zaidi ya 3,000 kwa ajili ya
wanafunzi wapya wa kidato cha kwanza ili waweze kuingia
madarasani,"amesema.
Kuhusu suala la kufanya ibada siku ya Krismas
na Mwaka Mpya, Waziri Mkuu amesema watumishi hao hawajazuiwa kufanya
ibada na badala yake watasali vituoni kwao na kwamba hajazuia watumishi
hao kufanya ibada wakati wa sikukuu hizo.
Jumatatu, Desemba 7,
2020 Waziri Mkuu aliendesha kikao na Wakuu wa Mikoa, Katibu Mkuu Wizara
ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI
kwa njia ya video akiwa ofisini kwake Mlimwa, jijini Dodoma na kupokea
taarifa ya maandalizi ya mapokezi ya wanafunzi wa kidato cha kwanza,
2021.
Tags
Habari