Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Mhe. Mattar Zahor Massoud amehudhuria katika sherehe ya kuwapongeza wagombea na wateule walioshika nafasi mbalimbali katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), anaripoti Mwandishi Diramakini.
Sherehe hiyo iliandaliwa na Umoja w Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Tawi la Kichungwani lililopo katika Wiilaya ya Chake Chake Mkoa wa Kusini Pemba katika kiwanja cha kufurahishia watoto Tibirinzi.
Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba ametoa pongezi kwa vijana wa Kichungwani kwa kujipanga na maandalizi ya shughuli kama hiyo.
Amesema, kuna changamoto nyingi zinataka kufanyiwa kazi, "tushirikiane kwa pamoja katika kutatua changamoto hizo, kila mtu kwa nafasi yake asaidie kuunga mkono juhudi za mapambano ya kuleta maendeleo,
"Naahidi kutoa ushirikiano katika kutatua changamoto zilizopo, nawaahidi watu wa Kichungwani kuwatafutia eneo la kuwawekea ofisi ya uhakika, Tumeridhishwa na kazi kubwa waliyoifanya vijana wa Kichungwani katika uchaguzi Mkuu uliopita,"amesema.
Katibu wa Tawi la Kichungwani Bibi Salha Issa Nassour amemshukuru Mhe. Mkuu wa Mkoa kwa kuungana nao katika sherehe hiyo, na kumuomba Mkuu wa Mkoa huyo kuwapa ushirikiano katika kazi zao za chama na kijamii ili kuleta maendeleo na kufunguwa fursa za ajira kwa vijana.
Katibu huyo amemuomba Mkuu wa Mkoa kuweza kufanya juhudi ya kuweza kuwapatia jengo la tawi ili kuendeleza harakati zao za kichama na kijamii, jambo hilo likiwa ni changamoto kubwa walionayo Tawi la Kichungwani kwa kukosa jengo la kuendesha harakati zao.
Pia mwakilishi wa vijana Tawi la Kichungwani katika sherehe hiyo ya Desemba 12,2020, Zadida Abdalla Rashid ametoa shukrani kwa niaba ya vijana wa Tawi la Kichngwani na kutoa ahadi ya ushrikiano mkubwa kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuleta maendeleo ya nchi yetu.
"Vijana wa Kichungwani tupo tayari kuitikia wito muda wowote katika kukijenga Chama na katika harakati za kuleta maendeleo pindi tutakapohitajika,"amesema.