Wamiliki wa viwanda vya kuchenjua madini aina ya dhahabu maarufu kama Plant zaidi ya 30 katika Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale mkoani Geita wameilalamikia halmashauri hiyo kwa kufunga kwa siku tisa sasa viwanda hivyo vya kuchenjulia dhahabu kwa madai ya kutolipa tozo ya huduma kiasi cha sh. millioni tano kila mwaka kama kodi ya huduma ya halmashauri, anaripoti Robert Kalokola (Diramakini) Geita.
Francis Kiganga akimuonyesha Mwandishi Diramakini (hayupo pichani) kofuli ambalo limetumika na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Nyang'hwale kufunga kiwanda (Plant) chake cha uchenjuaji kwa madai ya kutolipa kodi ya sh.milioni tano kwa mwaka, (Picha na Robert Kalokola/ Diramakini).
Wafanyabiashara hao wamesema sheria wanayotambua ya madini inawataka kulipia asilimia 0.3 ya mapato yao kama kodi halali ya kodi za madini baada ya marekebisho ya kodi za madini,lakini halmashauri hiyo inawatoza tena sh. milioni 5 kila kiwanda kimoja kila mwaka.
Wamiliki hao wamesema, ongezeko hilo la tozo limekuwa ni mzigo kwao,na hivyo baadhi yao kufikiria kufunga shughuli na kusitisha uzalishaji wa dhahabu kutokana na kufanya kazi bila kupata faida.
Mwenyekiti wa Wachimbaji hao, Charles Masanyiwa amesema kodi hiyo inawafanya wafanyabiashara hao kufanya kazi hiyo kwa hasara.
Amesema, wanaomba serikali kulitazama tena kwa sababu wachenjuaji hao wamekuwa wanalipa kodi zilizopo bila usumbufu, lakini hiyo tozo ya sh.milioni 5 kwa mwaka kila plant inawaongezea mzigo wa kodi katika biashara hizo .
Francis Kiganga ambaye ni mmiliki wa kiwanda cha kuchenjua dhahabu amesema, kwa mujibu sheria kodi za madini inabidi walipe asilimia 0.3 kutokana na mapato yao yote kwa mwaka.
Amesema, tozo ya sh. milioni 5 kwa mwaka inayotozwa na Halmashauri ya Nyang'hwale iko kinyume na sheria ya madini ndiyo maana wafanyabiashara hao waipinga na kuikataa lakini pia siyo kiwango ambacho ni rafiki kwao kumudu kulipia.
Ameongeza kuwa, wamejitahidi kukaa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Mariam Chaurembo wafikie makubaliano lakini muafaka umeshindikana na kuomba viongozi wa juu zaidi ya hapo kuingilia kati ili kutatua tatizo.
Amesema wamemuomba mkurugenzi kuwaonyesha sheria anayotumia kuwatoza tozo hiyo lakini siku zote yeye amedai ni makubaliano yalifanyika baina ya Halmashauri na wafanyabiashara hao, lakini haonyeshi makubaliano hayo yalipo.
Francis Kiganga ambaye kitaaluma ni Wakili wa Mahakama Kuu amesema, Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa,na Sheria ya Madini na mabadiliko yake zinaelekeza namna wafanyabiashara hao wanavyotakiwa kulipa kodi na kwamba zote wanalipa.
Wakili Kiganga amesema, kodi hiyo ya Halmashauri ya Nyang'hwale ya milioni 5 kwa mwaka inakiuka sheria nyingine za madini na fedha zinazo toa utaratibu wa kulipa Kodi za madini.
Misana Nyabange na Mihaya Bundala wamiliki wa viwanda vya kuchenjua dhahabu wanasema wanalipa kodi asilimia 0.3 wanapoenda kuuza dhahabu pamoja na kodi nyingine, lakini bado Mkurugenzi anataka walipe milioni 5 kwa mwaka.
Wamesema kodi hiyo inawaongezea utitiri wa kodi na kuwafanya wasipate faida hivyo wanafikiria kusitisha kuendelea kufanya biashara hiyo.
Aidha, wamesema kufungia viwanda hivyo ni kuendelea kuwatia hasara zaidi kwa sababu viwanda hivyo vina kemikali ambayo inaendelea kutumika katika mitambo hiyo, lakini wataalam wao hawawezi kuingia kwa sababu vimefungwa.
Wamesema,kuna hatari ya mitambo yao kulipuka kutokana na kemikali inayoendelea kwenye mitambo bila kufanyiwa uchunguzi wa kitaaluma kurekebisha kiwango wakati wa kuendelea kuchenjua.
Akijibu mamalamiko hayo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale, Mariam Chaurembo amesema utaratibu wa kulipa milioni 5 kwa kila plant ni makubalianao ya kikao cha baraza la madiwani katika kipindi cha mwaka 2015/2016.
Mariam Chaurembo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Nyang'hwale. (Picha na Robert Kalokola/Diramakini).
Wakati Chaurembo anasema ni makubaliano ya baraza la madiwani la mwaka 2015/2016 Serikali ya Tanzania ilifanya maboresho ya sheria ya madini kuanzia mwaka 2017 pamoja na kupunguza kodi mbalimbali za madini kuanzia mwaka huo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Nyang'hwale Mariam Chaurembo amesisitiza kuwa, ataendelea kufunga viwanda hivyo hadi pale watakapolipia kodi hizo kwani zipo kwa kwa mujibu wa maamuzi ya baraza la madiwani la halmashauri hiyo.
Tags
Habari