Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mwita Waitara amesema, Mgodi wa Uchimbaji wa Dhahabu wa Geita (GGML) una rekodi nzuri ya kutunza mazingira katika eneo lake la shughuli za uchimbaji,anaripoti Robert Kalokola (Diramakini) Geita.
Msafara wa Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mwita Waitara ukitazama bwawa la mabaki ya sumu iliyotumika kwenye shughuli za dhahabu katika mgodi wa GGML. (Picha na Robert Kalokola/ Diramakini)
Amesema kuwa, ameridhishwa na utunzaji wa mazingira katika mgodi huo na kuelekeza kuendelea kuheshimu Sheria zilizopo kwa ajili ya kutunza mazingira kwa viwango vinavyotakiwa.
Naibu Waziri Waitara amesema, taarifa alizozikuta ofisini kwake baada ya kuteuliwa, alikuta GGML ina rekodi nzuri ya kutunza mazingira,hivyo ameutaka mgodi huo kuendelea kufanya hivyo.
Naibu Waziri Waitara amesema hayo wakati akiongea na uongozi wa GGML alipofanya ziara katika mgodi huo kukagua na kuona maeneo mbalimbali yanayohusika na shughuli za utunzaji wa mazingira.
Moja ya mlima ambao umeandaliwa kitaalam kwa ajili ya kupanda miti ya asili ili kurudishia uoto wa asili. Mlima huu ni marundo ya vipande vya miamba iliyopasuliwa wakati wa kuchimba dhahabu, lakini imewekewa udongo mpya na kupanda miti ili kuhifadhi mazingira. (Picha na Robert Kalokola/Diramakini).
Maeneo aliyotembelea ni eneo la vifusi vikubwa vya mabaki ya mawe ambavyo viko kama vilima ambavyo vinapandwa miti ya asili ili kurudishia uoto.
Eneo lingine ni pamoja na bwawa la kutunzia masalia ya maji ya sumu iliyotumika kwenye shughuli za mgodi.
Mkuu wa Kitengo cha Mazingira wa GGML, Yusuph Mhando amesema kuwa, mgodi huo unaendelea kuheshimu sheria zinazohusika na kutekeleza maelekezo ya viongozi wa Serikali.
Ameongeza kuwa, mgodi huo asilimia kubwa uko kwenye hifadhi ya msitu wa Geita hivyo wanafanya jitihada zote kurudishia uoto kwa kupanda miti ya asili katika maeneo ambayo yaliharibiwa na shughuli za uchimbaji wa madini mgoni hapo.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mwita Waitara akiwa anatoa maelekezo katika kikao na uongozi wa GGML. (Picha na Robert Kalokola/ Diramakini)
Aidha, Mhando amefafanua kuwa miti inayopandwa imeandaliwa kitaalum katika vitalu vinavyopatikana katika eneo la Geita kuzunguka mgodi na wanatumia vibarua kutoka kwenye vijiji vinavyozunguka mgodi huo.
Naibu Waziri Waitara amefanya ziara katika mgodi huo na kutembelea maeneo mengine katika mji wa Geita kama dampo la taka ngumu Halmashauri ya mji pamoja na viwanda vya kuyeyushia dhahabu (elution plants).
Tags
Habari