Waliokuwa wafanyakazi nane wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na wafanyabiashara watano wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Watuhumiwa hao wanakabiliwa na mashtaka sita likiwemo la kuisababishia benki hiyo hasara ya sh. bilioni 4.6 baada ya kuzikatakata noti za shilingi 10,000 zipatazo 460,000 ili kuzibadilisha na kupata noti mpya kwa manufaa yao.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka dhidi ya washtakiwa hao iliyosomwa mahakamani leo Desemba 13, 2020 na jopo la mawakili wanne wa Serikali wakiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Paul Kadushi, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, Wakili wa Serikali, Jackline Nyantori na Wakili wa Serikali, Tulamanya Majigo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Godfrey Issaya.
Wakili Majigo amewataja washtakiwa hao kuwa ni Mariagoreth Kunzugala, Henry Mbowe, Cesilia Mpande, Agripina Komba, Zubeda Mjewa, Khadija Kassunsumo na Mwanaheir Omary (wote wafanyakazi wa BoT).
Wengine ni wafanyabiashara, Alistides Genand (Stide), Shukuru Mchegage, Musa Chengula, Zaituni Chihipo (Zai) na Respicius Rutashubilwa.
Amedai kuwa, kati ya Januari Mosi, 2017 na Septemba 30, 2019 katika maeneo tofauti tofauti ndani ya jiji na Mkoa wa Dar es Salaam, wafanyakazi hao wa BoT wakiwa watumishi waliongoza kutendeka kwa makosa ya kupanga ambapo walikiuka majukumu yao na kuwezesha kutendeka kwa makosa.
Katika shtaka la pili ilidaiwa kuwa wakiwa mahali hapo hapo washtakiwa, Genand, Nchegage, Chengula Chihipo na Rutashubilwa wanadaiwa kushirikiana na watumishi hao wa BoT kuharibu noti kwa kuzikatakata kwa kwa lengo la kujipatia faida.
Ilidaiwa kuwa washtakiwa wote kwa pamoja kwa ridhaa yao na bila ya kuwa na kibali ama mamlaka, kwa makusudi waliharibu noti za sh. 10,000 zipatazo 460,000 kwa kuzikatakata na kwenda kuzibadilisha BoT kwa lengo la kujipatia faida.
Katika shtaka la nne, Nyantori amedai kuwa, siku na mahali hapo washtakiwa hao walipanga mpango wa kitapeli wa kimawasiliano ya kulaghai na kujipatia kiasi cha sh. bilioni 1.5 kwa kuwasilisha noti ambazo wameziharibu kwa kuzikatakata ili wapatiwe noti mpya.
Nyantori amedai kuwa, washtakiwa hao wakiwa katika ofisi ya BoT jijini Dar es Salaam wanadaiwa kujihusisha na muamala wa sh.Bilioni 1.5, huku wakijua kuwa fedha hizo ni zao la makosa tangulizi ya kuongoza genge la uhalifu, makosa ya kupanga na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Katika shtaka la mwisho imedaiwa kuwa washtakiwa hao kwa makusudi waliisababishia Benki Kuu ya Tanzania hasara ya sh.Bilioni 4.6.
Hata hivyo, washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu mashtaka mahakamani hapo kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi ambazo kwa kawaida husikilizwa Mahakama Kuu ama Mahakama ya Mafisadi.
Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi katika kesi hiyo bado haujakamilika na kesi hiyo imeahirishwa hadi Desemba 28,2020.