Watuhumiwa tisa wa mauaji ya watu 17 wanayodaiwa kuyatekeleza Februari 16, 2010 eneo la Mugaranjabo Kata ya Buhare Manispaa ya Musoma wakiwa ndani ya Mahakama Kuu Kanda ya Musoma leo Desemba 11,2020 ambapo tarehe ya hukumu imepangwa na Jaji anayeendesha kesi hiyo Mustapha Siyani kuwa ni Januari 15, 2021. (Picha na DIRAMAKINI).
Watuhumiwa tisa wa mauaji ya watu 17 yaliyofanyika Februari 16, 2010 katika eneo la Mugaranjabo Kata ya Buhare Manispaa ya Musoma mkoani Mara wamerudishwa mahabusu baada ya Jaji aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo namba 56 ya mwaka 2018, Mustapha Siyani kupanga tarehe ya hukumu kuwa ni Januari 15,2021,anaripoti Amos Lufungilo (Diramakini) Mara.
Ni baada ya kupokea mapendekezo ya wazee wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma na kufanya majumuisho kutoka upande wa Jamhuri na upande wa utetezi kuhusiana na kesi hiyo kwa mara ya mwisho kabla ya hukumu kwa tarehe aliyoitaja.
Kesi hiyo imeendeshwa kwa njia ya mtandao Desemba 11, 2020 katika Mahakama Kuu Kanda ya Musoma na Jaji Mustapha Siyani ambapo watuhumiwa wa kesi hiyo tisa walifikishwa mahakamani hapo chini ya ulinzi mkali wa Polisi, huku Mawakili wa pande zote mbili wakihudhuria, na kupata wasaa wa kusikiliza mapendekezo ya Wazee wa mahakama waliyokuwa wakiyaeleza kwa Mh.Jaji Siyani na kufikia majumuisho kabla ya tarehe ya hukumu kama ilivyotajwa na Jaji kuwa ni Januari 15, 2021.
Kesi hiyo, imedumu kwa miaka 10, ambapo watuhumiwa wanadaiwa kutekeleza mauaji ya watu 17 kwa ajili ya kulipa kisasi ambapo watu 17 waliuawa kwa kukatwa mapanga sehemu mbalimbali za miili yao.
Tukio ambalo liliacha simanzi kwa wakazi wa Musoma na Watanzania kwa ujumla.
Katika kesi hiyo, upande wa Jamhuri una mashahidi wapatao 23 na vielelezo vipatavyo 44 ukiongozwa na mawakili wa Serikali akiwemo Wallace Mahenga na Yese Temba huku upande wa utetezi jopo la mawakili likiongozwa na Wakili Ostack Muligo na wenzake.
Watuhumiwa tisa wa mauaji ya watu 17 wanayodaiwa kuyatekeleza Februari 16, 2010 eneo la Mugaranjabo Kata ya Buhare Manispaa ya Musoma wakiwa ndani ya Mahakama Kuu Kanda ya Musoma leo Desemba 11,2020 ambapo tarehe ya hukumu imepangwa na Jaji anayeendesha kesi hiyo Mustapha Siyani kuwa ni Januari 15, 2021. (Picha na DIRAMAKINI).
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya Mahakama Kuu Kanda ya Musoma iliyopo Bweri Manispaa ya Musoma, Wakili wa Serikali Wallace Mahenga amesema baada ya wazee wa Mahakama kutoa ushauri wao kwa Jaji na kufanya majumuisho kwa kusikiliza shauri na vielelezo vyote na ushahidi uliowasilishwa upande wa Jamhuri amesema anaamini kwamba mahakama itatenda haki Januari 15, 2021 ambapo ndiyo tarehe ya hukumu ya kesi hiyo.
Kwa upande wake Wakili anayeongoza jopo la utetezi wa washitakiwa hao, Ostack Muligo, amesema pia kuwa haki itatendeka kwa kutolewa adhabu kwa watuhumiwa watakaokutwa na hatia katika kesi hiyo.
Watuhumiwa hao ni Juma Mgaya, Aloyce Nyabasi,Nyakangara Wambura, Marwa Mgaya, Nyakangara Masemere,Sadock Alphonce, Kumbata Bur'Jai, Mgesi Mgendi Ngoso na Sura Bukari ambao wote wanasubiria hukumu kutolewa hapo Januari 15, 2021.