Wawekezaji kutoka nchini Uturuki wamewasili nchini Tanzania hivi karibuni kwa ajili ya kujionea fursa za uwekezaji na biashara zilizopo nchini ili waweze kuwekeza na kukuza Diplomasia ya Uchumi baina ya mataifa hayo, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Balozi wa Tanzania nchini Uturuki, Mhe. Prof. Elizabeth Kiondo alithibisha kuwasili kwa wawekezaji hao wakati wa uzinduzi wa Taasisi ya Waturiki ya Compass Partners jijini Dar es Salaam na kuongeza kuwa wawekezaji watano kati ya kumi wamefika nchini na kujumika na Waturuki wengine wanaofanya biashara zao hapa nchini.
Balozi wa Tanzania nchini Uturuki, Mhe. Prof. Elizabeth Kiondo akiongea na wanahabari (hawapo pichani) wakati wa uzinduzi wa Taasisi ya Waturiki ya Compass Partners jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
"Wawekezaji hawa kutoka Uturuki wamekuja na wamefungua taasisi yao
inayojulikana kwa jina la Compass Partners ili kuendeleza biashara na
tunaamini kwa kutekeleza biashara hii tunaenda kuendeleza uchumi wa
Tanzania na kutengeneza ajira kwa watanzania,"amesema Prof. Kiondo.
Prof.
Kiondo ameongeza kuwa, hatua ya kwanza wawekezaji hao wameleta bidhaa
mbalimbali ili watanzania wazione, hatua ya pili itakuwa ni uwekezaji wa
kiwanda hapa nchini kwa ajili ya kuanza uzalishaji wa bidhaa ambazo
zitauzwa hapa nchini.
Kaimu Balozi wa Uturiki hapa Nchini, Mhe. Onur Yah akiongea na wanahabari (hawapo pichani) wakati wa uzinduzi wa Taasisi ya Waturiki ya Compass Partners jijini Dar es Salaam.
Aidha, kwa upande wa bidha zinazozalishwa
hapa nchini ambazo zina fursa ya kuuzwa Uturuki ni pamoja na chai,
pamba, tumbaku na kahawa bidhaa hizi zote zina soko kubwa sana nchini
Uturuki.
"Tunazalisha tani 350,000 za pamba lakini tunaweza
kuchakata asilimia 15 tu, hivyo tumepata tayari mwekezaji ambaye
atawekeza katika kiwanda cha nguo mkoani Simiyu ili kuongeza thamani ya
bidhaa ya pamba hapa nchini,"amesema.
Balozi, Prof. Kiondo ametoa wito
kwa Watanzania kuanza kuchangamkia fursa hizo za biashara ili waweze
kuongeza kipato na kuongeza biashara zao.
Kwa upande wake, Kaimu
Balozi wa Uturiki hapa Nchini, Mhe. Onur Yah amesema kuwa biashara kati
ya Tanzania na Uturiki imekuwa ikiimarika kila wakati kwani Tanzania ni
sehemu salama ya kuwekeza na kufanya biashara.
Balozi wa Tanzania nchini Uturuki, Mhe. Prof. Elizabeth Kiondo pamoja na Kaimu Balozi wa Uturiki hapa Nchini, Mhe. Onur Yah wakikata utepe wakati wa uzinduzi wa Taasisi ya Waturiki ya Compass Partners jijini Dar es Salaam.
"Kupitia
uwekezaji katika sekta mbalimbali ni imani yangu kuwa tutaendelea kukuza
na kuimarisha uhusiano wetu wa kidiplomasia,"amesema Mhe. Yah.
Aidha,
amewataka Waturuki na Watanzania kutumia fursa za biashara
zinazopatikana baina ya mataifa hayo ili kufanya biashara na kukuza
uchumi wao.
Ushirikiano wa Tanzania na Uturuki ni wa muda mrefu,
pamoja na mambo mengine uhusiano huo umekuwa ukijikita zaidi katika
kuendeleza uwekezaji wa viwanda, elimu na utalii hasa katika kutangaza
vivutio vya utalii vya Tanzania nchini Uturuki.
Tags
Uchumi