Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe.Hemed Suleiman Abdulla amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ipo makini katika kuona kasi ya uwekezaji nchini inaendelea kuimarika ili lengo la Taifa la kuwa na jamii yenye ustawi mzuri liweze kufikiwa kwa wakati, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Mheshimiwa Makamu wa Pili wa Rais ameyabainisha hayo wakati akizungumza na Mwakilishi wa kampuni ya ufuaji wa umeme kwa kutumia usarifu wa taka taka kutoka nchini Romania.
Mazungumzo ambayo yamefanyika ofisini kwake Vuga jijini Zanzibar, pia Makamu wa Pili wa Rais, Mheshimiwa Suleiman amesema Serikali inaelewa fika umuhimu wa uwekezaji kwa vile ndio njia kuu ya kuongeza mapato sambamba na upatikanaji wa fursa za ajira.
Amesema, Zanzibar imeshajiweka tayari kuyaandaa mazingira rafiki yatakayotoa nafasi kwa taasisi, kampuni na hata mashirika ya Kitaifa na Kimataifa kutumia rasilmali zilizopo nchini katika kuwekeza miradi ya kiuchumi kupitia usimamizi wa Mamlaka inayohusika na Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA).
Pia ameyahakikishia makampuni, taasisi na mashirika wakiwemo watu binafsi kuwa,Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kutoa ushirikiano wa kina ili wale waliyoonyesha nia ya dhati ya kuwekeza vitega uchumi waweze kukamilisha taratibu mapema.
Naye Mwakilishi wa Kampuni ya ufuaji wa umeme kwa kutumia usarifu wa taka taka kutoka Romania, Bw.George Alexandru amesema uongozi wa kampuni hiyo uko tayari kuiunga mkono Zanzibar katika muelekeo wake wa kuimarisha Sekta ya Uwekezaji.
Alexandru amemueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Mradi wa Ufuaji wa Umeme kwa kutumia taka taka wanaokusudia kuuanzisha endapo watafanikiwa kupata fursa hiyo utatengewa dola za Kimarekani milioni 100.
Mwakilishi huyo amesema kuwa,kwa mujibu wa uzoefu wa kampuni hiyo, taka taka zenye kiwango cha tani zipatazo 180 zikisarifiwa vyema zina uwezo wa kufua Megawati 11.5 za umeme.
Mwakilishi wa kampuni hiyo ya ufuaji wa umeme kutoka Romania amesema kwamba, utafiti wa awali uliofanywa katika dampo liliopo Kibele umeonyesha lina uwezo wa kutosheleza kuanzishwa kwa mradi huo wa ufuaji umeme.