Waziri Aweso aridhishwa na uchimbaji wa kisima cha Mzakwe

Waziri wa Maji,Jumaa Aweso ameridhishwa na utekelezaji wa kazi ya uchimbaji wa kisima cha maji katika eneo la Mzwake lililopo Makutupora nje kidogo ya jiji la Dodoma, anaripoti Fatuma Malende (WM).
Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) akiwa na Katibu Mkuu, Mhandisi Anthony Sanga (kulia kwake) pamoja na Kaimu Mtendaji Mkuu wa Mamlaka wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) Mhandisi Aron Joseph (kushoto kwake) wakikagua uchimbaji wa kisima cha maji Mzwake mara baada ya Waziri Aweso kufanya ziara ya kushitukiza kukagua uchimbaji wa kisima hicho unaofanywa na Kampuni ya Shanxi Construction Engineering Corporation and Mineral Company ya nchini China.(Picha na WM/Diramakini).

Waziri ametoa kauli hiyo alipofanya ziara ya kushitukiza Desemba 20, 2020 usiku katika eneo linalochimbwa kisima ili kuweza kujiridhisha endapo kampuni iliyopewa kazi hiyo inafanya kazi usiku na mchana kama ilivyo katika mkataba.

“Nimefika hapa usiku huu kwa kushitukiza, lakini nimeridhishwa na kazi kubwa inayofanyika, nimejionea mwenyewe kisima kinachochimbwa kitazalisha lita laki nne kwa saa na ninamuagiza Katibu Mkuu, Mhandisi Anthony Sanga kuongeza visima vingine viwili ili kupunguza shida ya maji katika jiji la Dodoma,"amesema Waziri Aweso.
Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) akikagua uchimbaji wa kisima cha maji cha Mzakwe usiku alipofanya ziara ya kushitukiza ili kujiridhisha na utekelezaji wa uchimbwaji wa kisima hicho.(Picha na WM/Diramakini).

Aidha, Waziri Aweso amewataka watendaji wa wizara kuwajibika ipasavyo ili kukamilisha miradi ya maji kwa wakati. 

“Nitume salamu kwa wataalam wote wa Wizara ya Maji, RUWASA na Wahandisi wote kwenye Halmashauri kuwa janja janja katika wizara sasa imefikia mwisho sisi kama viongozi wa Wizara ya Maji tutafuatilia usiku na mchana utekelezaji wa miradi na kuhakikisha watanzania wanapata maji safi na salama kwa wakati,” Waziri Aweso amefafanua.
Waziri wa Maji, Mhe.Jumaa Aweso (Mb) akitoa maelekezo mara baada ya kufika Mzakwe kwenye uchimbaji wa kisima. (Picha na WM/Diramakini).

Naye Kaimu Mtendaji Mkuu wa Mamlaka wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA), Mhandisi Aron Joseph amesema, kisima kinachochimbwa katika eneo la Mzakwe kina urefu wa mita 150 na kitakuwa kinazalisha maji lita laki nne kwa saa ambapo kwa sasa mahitaji ya maji katika jiji la Dodoma ni mita za ujazo laki moja na elfu tatu na uwezo wa uzalishaji kwa sasa ni mita za ujazo 66.

Kwa upande wake Katibu Mkuu, Mhandisi Anthony Sanga amesema, eneo hilo linalochimbwa kisima ni eneo la mkondo wenye maji mengi hivyo wanategemea kupata maji yatakayopunguza adha ya maji katika jiji la Dodoma.

Kisima cha Mzakwe kinachimbwa kwa muda wa siku 30 badala ya siku 60 kama mkataba unavyoelekeza na kinachimbwa na Kampuni ya Shanxi Construction Engineering Corporation and Mineral Company ya nchini China. 

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news