Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa amesema kuwa katika uongozi wake atahakikisha heshima ya michezo hapa nchini inarejea, anaripoti Shamimu Nyaki (WHUSM) Dar es Salaam.
Bashungwa ameyasema hayo jijini Dar es Salaam ambapo alifanya kikao na makocha pamoja na wanamichezo wa zamani na ameeleza kuwa Serikali imeanza kutenga fedha kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo ya Michezo.
Bashungwa ameongeza kuwa marekebisho yaliyofanywa katika Sheria za Baraza la Michezo la Taifa (BMT) ya mwaka 1967 kuhusu michezo ya ridhaa na kulipwa, kwa sasa inatambua michezo ya kulipwa ambapo kuna wachezaji zaidi ya 2000 wanaocheza michezo ya kulipwa ndani ya nchi na wanamichezo takriban 28 wanacheza michezo ya kulipwa nje ya nchi.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Abdallah Ulega ameiagiza Idara ya Michezo kusimamia maazimio yote ya kikao hicho kufanyiwa kazi na matokeo yaonekane.
"Nia yetu ni kuendeleza michezo, na hili tutalisimamia vyema hivyo tunaomba mawazo mazuri kutoka kwenu namna ya kuendeleza michezo,"amesema Ulega.
Ulega ameongeza kuwa dhamira ya vikao na wadau wa michezo ni kutathmini michezo ilipotoka, ilipo na wapi ielekee kwa maslahi ya taifa.
Naye kiungo wa zamani wa Yanga na timu ya taifa, Ally Mayai Tembele ameishukuru Serikali kwa kuandaa vikao vya kukutana na wadau kupokea mawazo kuhusu maendeleo ya michezo nchini, huku akieleza kuwa michezo inahitaji nidhamu na kuwekeza kwa Watoto wa shule za msingi na sekondari, vifaa vya michezo na miundombinu bora ya michezo.