Kama njia mojawapo ya kudhibiti utoroshaji wa madini nchini, Waziri wa Madini, Doto Biteko ametoa wiki moja, kuanzia tarehe 21 hadi 28 Desemba, 2020 Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa nchini kuhakikisha mialo ya kuchenjulia madini ya dhahabu imesajiliwa,wanaripoti Greyson Mwase na Steven Nyamiti (WM).
Waziri Biteko ametoa agizo hilo le Desemba 15, 2020 katika kikao chake na Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kilichofanyika jijini Dodoma chenye lengo la kujadili changamoto mbalimbali zinazoikabili Sekta ya Madini pamoja na kuzitatua ikiwa ni pamoja na kujifunza namna ya uandaaji wa bajeti na namna ya kuitekeleza kwa mwaka wa fedha 2021-2022.
Wengine waliohudhuria katika kikao hicho ni pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila, Kamishna wa Madini Nchini, Mhandisi David Mulabwa, Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Prof. Idris Kikula, Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Mhandisi Yahya Samamba, Wakurugenzi wa Tume ya Madini na maafisa bajeti kutoka Tume Makao Makuu na Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa.
Amewataka Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kuhakikisha kunakuwepo na daftari maalum kwenye kila mwalo litakalokuwa na kumbukumbu ya madini yote yaliyozalishwa na kupelekwa katika masoko ya madini.
Katika hatua nyingine Waziri Biteko ameelekeza Wizara ya Madini kuhakikisha ndani ya wiki mbili inabuni mfumo wa sms utakaowezesha kutoa taarifa za madini yanayosafirishwa kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine kama njia mojawapo ya kuwa na kumbukumbu za madini yanayosafirishwa kwenda kwenye masoko ya madini na kuwahakikishia usalama wa wafanyabiashara wa madini.
"Mfumo huu utatuwezesha kama Wizara kubaini mchimbaji au mfanyabiashara wa madini ana kiasi gani cha madini ambapo tunaweza kumpatia ulinzi kama ana madini yenye thamani kubwa," amesema Waziri Biteko.
Wakati huohuo Waziri Biteko amewataka Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kuhakikisha wanadhibiti utoroshaji wa madini kwa kushirikiana na vyombo vya usalama na kusisitiza kuwa Serikali haitasita kumwajibisha Afisa Madini Mkazi wa Mkoa atakayezembea na madini kutoroshwa katika mkoa wake.
"Lazima mhakikishe mnashirikiana na taasisi nyingine kwenye kudhibiti utoroshaji wa madini ikiwa ni pamoja na kuweka mifumo mizuri ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema,"amesisitiza Waziri Biteko.
Pia amewataka Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kuhakikisha kampuni zinazojishughulisha na uchimbaji wa kati na mkubwa zinawasilisha mipango ya ushirikishwaji wa Watanzania kwenye Sekta ya Madini ( Local Content Plans) na ya ufungaji migodi kama Sheria ya Madini inavyotaka.
Katika hatua nyingine ameipongeza Tume ya Madini kwa kuvuka lengo la ukusanyaji wa maduhuli kwa kipindi cha miezi mitano katika mwaka wa fedha 2020-2021 ambapo katika kipindi cha mwezi Julai hadi Desemba, 2020 Tume ya Madini ilikusanya shilingi bilioni 260 ambayo ni sawa na asilimia 118 ya kipindi husika.