WAZIRI BITEKO ASHUSHA RUNGU MIRERANI

AKATAA KUONGEZWA LANGO LA PILI, MGODI UTAKAOHUSISHWA NA UTOROSHAJI KUFUTIWA LESENI, AAGIZA MAENEO YA UKAGUZI KUONGEZWA, PROF. MANYA ASEMA WANATAMANI TANZANITE KUWA NEMBO YA TANZANIA

Waziri wa Madini, Doto Biteko amesema Serikali haitaongeza Lango la Pili katika Ukuta unaozunguka Migodi ya Tanzanite Mirerani bali itaendelea kuwa na lango moja tu la kuingilia kama ilivyo sasa kutokana tabia ya baadhi ya wadau katika eneo hilo kuendeleza vitendo vya kutorosha madini ya Tanzanite, wanaripoti Asteria Muhozya na Steven Nyamiti, Mirerani (WM).
Kauli ya Waziri Biteko imekuja kufuatia ombi lililowasilishwa na Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka ambaye ameiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuongeza lango la pili ili pia kuwapatia nafuu wananchi wa Kijiji cha Naishoi wanaoishi nga’mbo ya ukuta huo.

Waziri Biteko amesisitiza kwa sasa serikali haiwezi kuongeza lango hilo mpaka hapo baadaye itakapoona ipo haja ya kufanya hivyo baada ya kufanya utafiti wa kina na kujiridhisha kwamba, hakuna vitendo vyovyote vinavyotokea vya utoroshaji wa Tanzanite.
Aidha, Waziri Biteko amekubali ombi la wadau hao la kujengwa eneo kwa ajili ya kusubiri ukaguzi na kuongezwa kwa vituo vya ukaguzi ili kuepukana na adha ya kuwepo kwa foleni ndefu za kusubiri ukaguzi suala ambalo limekuwa na usumbufu kwa wadau ikiwepo adha ya kusubiri kwa muda mrefu hususan kipindi cha jua kali na mvua. 

Kufuatia malalamiko hayo, Waziri Biteko amemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini kuwasiliana haraka na Kampuni ya SUMA JKT ili kuanza haraka kwa ujenzi huo.
Akisisitiza mkakati wa udhibiti wa madini hayo, Waziri Biteko amesema endapo mtu yoyote atakayebainika ametorosha Tanzanite, atatakiwa kutaja mgodi alipotoa madini hayo na moja kwa moja serikali itaufutia leseni.

Kufuatia kauli hiyo, Waziri Biteko amemwagiza Afisa Madini Mkazi Mirerani kuwaandikia barua wasimamizi wote wa migodi iliyopo ndani ya ukuta ili kufahamishwa kuhusu suala hilo.
‘’Haitakuwa rahisi tena kwa Tanzanite kutoka eneo hili, kama kuna mtu anadhani ataweza, ajiandae kushindwa. Kuanzia leo atakayesaidia utoroshaji atafutiwa leseni,’’ amesisitiza Waziri Biteko na kuongeza kuwa, udhibiti huo unakwenda sambamba kwa broker na wanunuzi ambapo hao watalazimika pia kulipa faini ya shilingi milioni 50.

Katika hatua nyingine, Waziri Biteko ametoa ruksa kwa wachimbaji katika eneo hilo kupata huduma ya baruti kutoka kwa kampuni yoyote isipokuwa tu iwe na uhalali wa kufanya shughuli hizo ka mujibu wa Sheria.
Ruksa hiyo inafuatia kero iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Chama Cha Wachimbaji Madini Mirerani (MAREMA), Francis Nyari ambaye ameiwasilisha kwa Wizara na kueleza kuwa kumekuwepo na maelekezo ya kupata huduma ya baruti kutoka kwa kampuni kadhaa.

Akijibu kuhusu suala la TAMIDA kupatiwa sehemu ya kufanya biashara badala ya kutembea umbali mrefu kwenda jijini Arusha, Waziri Biteko amewashauri wadau hao kutafuta eneo kwa ajili ya kazi hiyo na serikali kupitia wizara italiidhinisha kwa mujibu wa sheria na kusititiza kuwa, sehemu ya kufanya Arusha itabaki kuendelea kuwa Soko la Kimataifa.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini, Prof. Shukrani Manya amesema kuwa, kama Wizara inatamani kuyafanya madini ya Tanzanite kuwa Nembo ya Taifa ikiwa wadau wa madini hayo wataheshimu na watashirikiana na serikali katika ulinzi wa rasilimali hiyo ikiwemo kufanya biashara ya tanzanite kwa kuheshimu taratibu zilizowekwa.

Amesema kuwa, serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi ya usalama ikiwemo miundombinu ya barabara ndani ya eneo linalozunguka migodi ya tanzanite na kuongeza kwamba, tayari serikali imekwishaanza kulifanyia kazi suala hilo. Naibu Waziri Manya amelielezea suala la barabra ndani ya ukuta baada ya Mbunge wa Simanjiro kulieleza kama changamoto kwa wadau ambayo serikali inapaswa kuifanyia kazi.
Prof. Manya ametumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dkt. John Magufuli kwa kumteua tena Waziri Biteko kuongoza wizara hiyo na kuahidi kuendelea kushirikiana naye kutekeleza majukumu yake ya Unaibu Waziri kwa uaminifu ili kuiwezesha Sekta ya Madini kuendelea kuleta heshima kwa watanzania na kuiwezesha kuchangia zaidi katika pato la taifa, na kuongeza, ‘’ tutaendelea kujali na kutatua matatizo katika sekta hii ili kuifanya kuwa bora zaidi, ‘’ amesema Naibu Waziri. 

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Joseph Mkirikiti amewataka wadau wa madini mkoani humo kutumia mamlaka kwa kufuata ngazi za kiutendaji pindi wanapotafuta nafasi ya kutatuliwa kero zao.
Ameahidi kukutana na wadau wa madini Desemba 21, ili kusikiliza na kuzitatua kero zinazowakabili wadau mabalimbali wa madini mkoani humo ikiwemo wanaofanya shughuli zao katika eneo la mirerani na kuongeza kuwa, changamoto zilizotolewa na wadau ambazo zinahusu mkoa huo zitafanyiwa kazi.

Kauli ya Mkuu wa Mkoa imekuja kufuata ombi lililowasilishwa na Mwenyekiti wa Chama Cha Wafanyabiashara wa Madini Nchini (TAMIDA), Sam Mollel ambaye amelalamikia kuwepo kwa hali ya kutozwa kodi ya pango katika Soko la Madini ambalo wameiomba iondolewe ikiwemo changamoto kadhaa kati ya wadau hao na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambapo ameeleza kuwa, kutatuliwa kwa changamoto zinazowakabili kutapelekea kuwawezesha wadau hao kupata hamasa ya kuendelea kufanya shughuli zao vizuri na hivyo kuchangia zaidi katika sekta husika.
"Kodi kwa wachimbaji na wamiliki wa migodi tutaziangalia na kushauri. Mimi kama Mwenyekiti wa Kodi wa Mkoa nitakutana na wadau hawa tarehe 21 Desemba, 2020,"amesema.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Mhandisi Zephania Chaula amesisitiza ukaguzi wa kina kuendelea kufanyika katika eneo hilo kutokana na wadau kutoheshimu taratibu kwa kuendeleza na tabia za kutorosha madini ya tanzanite.

‘’Ukitaka uheshimiwe, tuheshimu. Kama kusingekuwa na tabia ya kudokoa hata askari tusingewaweka hapa, lakini kwa tabia hii inayofanyika, ukaguzi uko pale pale,"amesisitiza Mhandisi Chaula.

Kauli ya Mhandisi Chaula inafuattia wadau hao kuwasilisha kero kuhusu ukaguzi wa kina unaofanywa eneo hilo.

Mkutano huo kati ya Waziri wa Madini uliomshirikisha pia Naibu Waziri wa Madini Prof. Shukrani Manya, Uongozi wa Mkoa wa Manyara, Watendaji wa Wizara, Tume ya Madini na wadau wa madini mkoani humo, umelenga kusikiliza na kutatua kero mbalimbali katika eneo la Mirerani.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news