Waziri Kalemani apigilia msumari TANESCO kukata umeme

Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani ameendelea kukazia msimamo wa agizo lake kwa Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kukata umeme kwa wateja wake wote ambao ni wadaiwa sugu bila kujali mteja huyo ni taasisi ya Serikali,anaripoti Robert Kalokola (Diramakini) Geita.
Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani akikata utepe wakati wa kuzindua rasmi na kuweka jiwe la msingi na kuwasha umeme katika Kituo cha Afya Nyarutembo wilayani Chato mkoani Geita. (Picha na Robert Kalokola/ Diramakini).

Amesema, TANESCO inatakiwa kukata umeme hata kwa Jeshi la Wananchi pamoja na Jeshi la Polisi kama na taasisi hizo zitakuwa zinadaiwa ankara za matumizi ya umeme.

Waziri Kalemani amesema hayo wakati akiweka jiwe la msingi katika kituo cha Afya Nyarutembo na kuwasha umeme katika kituo hicho kilichojengwa wilayani Chato.

Amesema kuwa, kwa sasa TANESCO haipokei ruzuku tena kutoka serikalini, hivyo inatakiwa kujiendesha kwa mapato yake ya ndani na inatakiwa kukusanya mapato.
Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani akihutubia wananchi wa Nyarutembo waliofika kushuhudia uwekaji jiwe la msingi na uwashaji umeme katika kituo hicho.(Picha na Robert Kalokola/Diramakini).

Amewataka watendaji wa shirika hilo kutokubali kupokea maelekezo kutoka kwa mtu yoyote kuhusu madeni ya umeme badala yake wakate umeme kwenye taasisi zote za Serikali zinazodaiwa ili ziweze kulipa madeni hayo na shirika liweze kujiendesha.

Aidha, Waziri Kalemani amewataka wananchi wanaopata huduma katika kituo cha Afya Nyarutembo kuhakikisha wanachangia bima ya afya ya jamii(CHF) iliyoboreshwa ili waweze kupata huduma bila changamoto.

Amewataka wanawake wajawazito kutumia kituo hicho cha afya kwa ajili ya kujifungua badala ya kujifungulia nyumbani ambapo hakuna wataalam wa afya.

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Chato, Benedict Ngaiza akisoma taarifa ya ujenzi huo kwa Waziri wa Nishati amesema, kituo hicho kimejengwa kwa zaidi ya sh.milioni 200.
Mganga mkuu wa Wilaya ya Chato, Dkt. Benedict Ngaiza akitoa ufafanuzi kwa Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani) kuhusu ujenzi wa kituo cha afya Nyarutembo. (Picha na Robert Kalokola).

Ameeleza kuwa,kituo hicho kilianza kama zahanati kwa kujengwa na wananchi mwaka 2010 lakini mwaka huu serikali ilitoa sh.milioni 200 na kufanikiwa kujenga jengo la watumishi ,jengo la baba,mama na mtoto, vyoo.

Amesema, kituo hicho wananchi walichangia nguvu zao kwa kuleta mawe,mchanga,maji vyenye thamani ya sh. 10,161,000 na kimesajiliwa na kilifunguliwa rasmi Machi 23, mwaka huu.

Mkuu wa Wilaya ya Chato, Mhandisi Charles Kabeho amewataka wananchi wa Nyarutembo kuchangia bima ya afya ya CHF iliyoboreshwa ili waweze kutibiwa popote.

Amemtaka Mratibu wa CHF iliyoboreshwa kufika katika eneo hilo kuhamasisha wananchi kujiunga na bima hiyo ili waweze kupata huduma stahiki.

Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani amefanya ziara katika kituo hicho ambacho kipo ndani ya jimbo lake la uchaguzi la Chato na kuchangia laki tatu ili kuwaunga mkono wananchi siku ambayo watakusanyika kuchimba msingi wa jengo lingine.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news