Waziri wa Nishati,Dkt. Medard Kalemani amewaagiza watendaji wa TANESCO na REA, kuhakikisha wanawaunganishia umeme wateja wote waliolipia ankara za umeme jijini Mwanza na maeneo ya vijijini ndani ya miezi mitatu kuanzia leo Desemba 30, 2020, anaripoti Dorina Makaya (WN) Mwanza.
Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Medard Kalemani akizungumza na Wafanyakazi wa TANESCO na REA Mkoa wa Mwanza na Wilaya zake katika kikao kikao kilichofanyika jijini Mwanza, 29 Desemba, 2020.(Picha na Dorina Makaya-WN).
Dkt.Kalemani ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) katika kikao kazi cha pamoja kilichofanyika kwenye ukumbi wa Benki Kuu jijini Mwanza.
Waziri Kalemani amewaelekeza watendaji hao wa TANESCO kuhakikisha wateja wote waliopo katika maeneo ya vijijini na kandokando ya miji, wanaunganishiwa umeme kwa gharama ya shilingi 27,000 bila kujali umbali wa mita 30 kwani ni wajibu wa TANESCO kuwafikishia wananchi nguzo za umeme ili kuwafikia wateja hao.
"Mnataka kila mwananchi awe mita 30 ndipo muwafikishie umeme? Ni kazi yenu kupeleka nguzo hadi muwafikie wananchi hao. Nimeambiwa mnasubiri sekula hii sasa ndiyo sekula na wapa. Nisisikie mtu anaongelea suala la mita 30,"amesema Waziri Kalemani.
Watumishi kutoka TANESCO na REA wakiwa katika mkutano wa pamoja na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Medard Kalemani pamoja na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Stephen Byabato. Mkutano ulifanyika jijini Mwanza.(Picha na Dorina Makaya-WN).
Pia Waziri Kalemani ameitaka TANESCO kuanzisha madawati ya huduma kwa wateja ili kuhakikisha wateja wanapatiwa huduma bora na kwa wakati na kuwaondolea adha ya kufuatilia maombi ya kuunganishiwa umeme kwenye ofisi za TANESCO wilayani.
Amewataka watendaji wa TANESCO kuwafuata wateja mahali walipo na kuepuka kutumia lugha ya kukatisha tamaa kwa wateja ili kujenga mahusiano mazuri na wateja jambo litakalopelekea kupanua wigo wa wateja na kuongeza mapato kwa shirika.
"Masurveyor ndio wanaolalamikiwa sana kwa kutoa lugha zinazokatisha tamaa. Ninawasihi mbadilike kuanzia sasa. Atakayebainika anatumia lugha mbaya kwa mteja, huyo tutaachana nae na atachukuliwa hatua za kinidhamu.
Wateja wote wahudumiwe bila kubaguliwa. Tunataka wateja wote wapate umeme bila kubaguliwa,"amesema Dkt. Kalemani.
Aidha, Dkt.Kalemani aliwapongeza watumishi wa TANESCO kwa utendaji mzuri na kueleza kuwa kwa zaidi ya asilimia 80 utendaji wa TANESCO ni wa kuridhisha.
Waziri Kalemani amesifu utendaji mzuri wa Meneja wa TANESCO Kanda ya Ziwa, Mhandisi Henryfried Byabato na kueleza kuwa utendaji mzuri wa kazi katika maeneo mengi aliyofanya kazi ndiyo uliopelekea kupandishwa cheo.
Waziri Kalemani pia alielekeza watumishi walioajiriwa kwa muda wanaohusika na kazi za kuwapimia umeme wananchi wanunuliwe pikipiki zitakazowawezesha kuwafikia wateja kwa urahisi.
Aidha, ameagiza kuwa watumishi hao (STE) wanaofanya kazi vizuri na waliofanya kazi kwa muda mrefu waombewe kibali cha ajira ya kudumu Utumishi kupitia Wizara ya Nishati.
Waziri Kalemani amesisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa kasi, ubunifu na kwa usahihi na amewataka watumishi wa TANESCO na REA kujiepusha na vitendo vya rushwa.
Akizungumza na waandishi wa habari katika kikao kazi hicho, Naibu Waziri Stephen Byabato amewataka watumishi wote kuzingatia maelekezo yaliyotolewa na Waziri Kalemani na atahakikisha anasimamia na kufuatilia utekelezaji wake kwa ukamilifu.
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Stephen Byabato, akizungumza na watumishi wa TANESCO na REA Mkoa wa Mwanza na Wilaya zake katika kikao kilichofanyika jijini Mwanza, 29 Desemba, 2020. (Picha na Dorina Makaya-WN).
Kikao kazi baina ya Waziri Kalemani na watumishi wa TANESCO na REA, ni kikao kazi cha pili baada ya kikao na wafanyakazi wa Mkoa wa Geita wiki moja iliyopita.
Lengo la vikao hivyo ni kuweka misingi ya pamoja ya utendaji kazi unaolenga kuleta matokeo chanya na ya haraka katika Sekta ya Nishati.
Tags
Habari