Waziri Kalemani autaka uongozi Wizara ya Nishati kufanya kazi kwa ubunifu

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amewataka watumishi wa wizara hiyo kufanya kazi kwa kasi na kwa ubunifu ili kuhakikisha Sekta ya Nishati inaendelea kukua ili kuwezesha upatikanaji wa umeme wa kutosha na wa uhakika kwa maendeleo ya viwanda na kuliletea Taifa maendeleo.
Baadhi ya wajumbe wa Menejimenti ya Wizara ya Nishati wakifuatilia kwa umakini maelekezo ya Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Medard Kalemani wakati wa kikao cha Menejimenti kilichofanyika leo katika ofisi za wizara hiyo zilizopo Mtumba jijini Dodoma. 

Waziri Kalemani ameyasema hayo leo Desemba 10, 2020 wakati akiwa kwenye kikao na wajumbe wa Menejimenti ya Wizara ya Nishati kilichofanyika katika ofisi za wizara hiyo zilizopo katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.
Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Medard Kalemani akizungumza na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Stephen Byabato ofisini kwake leo katika mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.

Kikao hicho cha Waziri na wajumbe wa Menejimenti ya Wizara ya Nishati, kilichohudhuriwa na Naibu Waziri, Mhe. Stephen Byabato,kimelenga kutambulisha viongozi wa wizara hiyo na kutoa maelekezo yanayolenga kuwa na utekelezaji mzuri wa malengo yaliyowekwa katika Sekta ya Nishati.

Akizungumza katika kikao hicho, Dkt. Kalemani ameiagiza Menejimenti ya Wizara hiyo kuhakikisha kuwa umeme wa uhakika na wa kutosha unazalishwa nchini kutoka kwenye vyanzo vya gharama nafuu hasa maji.

Pia, ameitaka Menejimenti ya Wizara ya Nishati, kuhakikisha kuwa ujenzi wa miundombinu ya kusafirishia umeme kutoka kona zote nne unakamilika kwa wakati na kuwe na mtandao wa njia ya kusambazia umeme kwa kona zote nne kaskazini, Kusini, Mashariki na Magharibi.
Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhe. Leonard Masanja akiwasilisha taarifa ya majukumu ya Wizara ya Nishati pamoja na taasisi zake kwa Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Medard Kalemani na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Stephen Byabato ( hawapo pichani) katika mkutano wa Menejimenti ya Wizara ya Nishati uliofanyika leo katika ofisi za wizara hiyo zilizopo Mtumba jijini Dodoma. 

Vilevile, Waziri Kalemani ameuagiza uongozi wa Wizara ya Nishati kuhakikisha kuwa vijiji vyote 2,884 ambavyo havijaunganishwa na umeme, ifikapo mwezi Desemba 2022, viwe vimeunganishwa na huduma hiyo.

Naye Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Stephen Byabato ameahidi kutoa ushirikiano mzuri na kufanya kazi kwa weledi katika kuhakikisha majukumu ya Waziri wa Nishati yanafanyika kwa ufanisi mkubwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news