WAZIRI LUKUVI AWATAKA WATENDAJI SEKTA YA ARDHI KUJIPANGA UPYA

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amewataka watendaji wa sekta ya ardhi kujipanga upya kwa kuwa wabunifu katika utekelezaji majukumu na kusisitiza kwamba hatomvumilia mtendaji atakayeshindwa kutekeleza majukumu yake,anaripoti Munir Shemweta (WNMM) Dodoma. 
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi.

Amesema, katika kuhakikisha utendaji wa sekta ya ardhi unaleta mafanikio katika mikoa nchini atamtuma Naibu wake, Dkt Angeline Mabula kufanya ukaguzi maalum wa ofisi za ardhi za mikoa ili kuangalia kazi zilizotekelezwa tangu kuanzishwa ofisi hizo. 

Akizungumza na Menejimenti Wizara leo Desemba 10, 2020 jijini Dodoma ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu kuapishwa hapo jana, amewataka watendaji wa sekta ya ardhi kujipanga upya na kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwa ushirikiano na kusisitiza kuwa watumishi wa wizara hiyo wakishirikiana vizuri wanaweza kufanya mambo mengi na makubwa zaidi.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi na Naibu Wake wakisalimiana na watumishi wa Wizara ya Ardhi walipowasili katika ofisi za wizara hiyo katika Mji wa Serikali Mtumba Dodoma leo. Kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Mary Makondo.

‘’Kuna mambo katika awamu iliyopita tulitakiwa tuyafanye lakini hayakufanyika safari hii hatutakubali kurudi nyuma, nataka niondoke katika wizara hiyo kwa heshima,"amesema Lukuvi. 

Waziri wa Ardhi aligusia pia sekta ya uwekezaji aliyoieleza kuwa wizara yake inatakiwa kuifanyia kazi kwa umakini ikiwemo kuwa na kumbukumbu sahihi za uwekezaji uliofanyika nchini, faida yake kwa taifa na kama ulisaidia kwa kiasi gani kutoa ajira kwa watanzania. 
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi akisisitiza jambo wakati wa kikao na Menejimenti ya Wizara ya Ardhi alipowasili kwa mara ya kwanza katika ofisi za wizara hiyo katika Mji wa Serikali Mtumba Dodoma leo tarehe 10 Desemba 2020. Wengine ni Naibu wake, Dkt Angeline Mabula (wa pili kulia), Katibu Mkuu Mary Makondo (wa pili kushoto) na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu Zakaria Kerra (wa kwanza kushoto).

Amewataka watendaji wa sekta ya ardhi kuwa na takwimu za taarifa zote za msingi katika wizara na kutolea mifano ya taarifa za hati zilizotolewa, maeneo yaliyopimwa pamoja na maeneo ya uwekezaji katika mashamba na faida yake na kusisistiza msingi wa uwekezaji unaanzia Wizara ya Ardhi. 

‘’Ni lazima tujitayarishe kwa kuwa matajiri wa takwimu na taarifa za msingi katika maeneo yetu kwani inakera kusikia hakuna takwimu katika eneo fulani,"amesema Lukuvi. 

Kwa mujibu wa Lukuvi yeye pamoja na Naibu wake hawakurudishwa kwenye wizara hiyo kwa bahati mbaya na wanataka kufanya kazi maradufu ili kuondoka na rekodi ya kishindo katika utendaji kazi wa wizara hiyo. 

Akigeukia Ofisi za Ardhi za mikoa Lukuvi amesema, baada ya wizara kuanzisha ofisi za ardhi za mikoa sasa kinachofuata ni wizara hiyo kufanya tathmini kwa kuangalia utendaji kazi wa ofisi hizo kama una tija na ulikuwa sahihi. 

‘’Nataka kuona kila ofisi imefanya nini tangu kuanzishwa kwake na kila kamishna wa Ardhi Msaidizi katika mkoa atupatie taarifa yake amefanya nini tangu kuanzishwa kwa ofisi yake,"amesema Lukuvi.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Dkt. Angeline Mabula akiangalia kadi aliyopewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Mary Makondo baada ya kumalizika kwa kikao cha Menejimenti ya Wizara kilichoongozwa na Waziri wa Ardhi William Lukuvi (kulia) walipowasili katika ofisi za Wizara Mtumba jijini Dodoma leo tarehe 10 Desemba 2020.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula amesema, Wizara ya Ardhi ina kazi kubwa ya kuhakikisha inatimiza lengo lake la makusanyao ambapo katika mwaka wa fedha 2020/2021 imepangiwa kukusanya jumla ya shilingi bilioni 200. 

Amewataka watendaji wa sekta ya ardhi kuhakikisha wanajikita katika kuhamasisha ukusanyaji kodi ya pango la ardhi na kupongeza ubunifu ulioanzishwa na wizara kutoa elimu kwa wamiliki wa ardhi kila mwishoni mwa wiki.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi akisalimiana na Mthamini Mkuu wa Serikali, Evelyne Mugasha alipowasili katika ofisi za Wizara hiyo katika Mji wa Serikali Mtumba Dodoma leo tarehe 10 Desemba 2020 (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI).

Akielezea suala la mashamba pori, Dkt. Mabula amesema, pamoja na kazi kubwa kufanyika ya kufanya ukaguzi wa mashamba pori lakini kunahitajika kazi ya haraka na kuchukua hatua kwani kazi bado ndefu katika suala hilo. 

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo William Lukuvi na Naibu wake Dkt. Angeline Mabula ndiyo mawaziri pekee waliorejeshwa katika wizara moja tofauti na wizara nyingine ambapo aidha alibaki waziri ama naibu waziri.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news