Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) ndicho chombo muhimu na chenye mchango mkubwa katika kuleta maendeleo ya kiuchumi Tanzania, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na viongozi wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) kwenye ukumbi wa Ofisi Ndogo ya Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es salaam, Desemba 22, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuui).
Ameyasema hayo leo Desemba 22, 2020 alipokutana na Bodi mpya ya taasisi hiyo katika ukumbi wa Ofisi Ndogo ya Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es Salaam.
“Sisi Serikali tunapofurahi na kuwaambia Watanzania kwamba nchi yetu imeingia kwenye uchumi wa kati, hatuachi kuzungumzia namna ambavyo sekta binafsi ilivyoshiriki kiiamilifu kuleta mabadiliko,"amesema.
Kikao hicho ambacho ni uetekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli alipozindua Bunge la 12, jijini Dodoma, kuhusu ushirikiano kati ya Serikali na TPSF.
“Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi hii na kwenye changamoto tutahakikisha tunazipatia ufumbuzi kwa pamoja. Serikali inaimani kubwa na Taasisi hii ya Sekta Binafsi Tanzania,"amesema Waziri Mkuu.
Kwa upande wao viongozi wa taasisi hiyo wameishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa ushirikiano inaowapatia ambao unawawezesha kutekeleza majukumu yao kwa urahisi na ufanisi mkubwa.
Kikao hicho pia kimehudhuriwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo, Waziri wa Viwanda na Biashara Geofrey Mwambe na watendaji wa taasisi za Serikali wanaohusika na usimamizi na uratibu wa maendeleo ya sekta binafsi.
Tags
Uchumi