WAZIRI MPANGO KUMALIZA TATIZO LA KUCHELEWESHA MISAMAHA YA KODI KWA WAKANDARASI WA MIRADI YA SERIKALI

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango ameahidi kumaliza tatizo la kuchelewa kutolewa kwa misamaha ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa Wakandarasi wanaopewa zabuni kutekeleza miradi mbalimbali ya Serikali ili kuwezesha miradi hiyo kuanza na kukamilika kwa wakati, anaripoti Robert Kalokola (Diramakini) Geita.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt.Philip Mpango akihutubia mkutano mkuu wa Baraza la Wafanyakazi wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) katika ukumbi wa Magufuli uliopo Kituo cha EPZA Mjini Geita (Picha na Robert Kalokola/Diramakini).

Amesema, atashirikiana na taasisi nyingine za Serikali kama vile Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali ili kuhakikisha taratibu zote za kutoa misamaha hiyo inatolewa kwa muda muafaka na nyaraka za Gazeti la Serikali za Misamaha (GN) kuhakikisha zinachapishwa kwa wakati ili wazabuni waweze kuanza miradi kwa wakati.

Dkt.Philip Mpango amesema hayo leo Desemba 10, 2020 katika Ukumbi wa Magufuli katika Kituo cha Uwekezaji (EPZA) Mjini Geita wakati akifungua mkutano mkuu wa 15 wa Baraza la Wafanyakazi wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS).

Dkt.Mpango alikuwa akitolea ufafanuzi hoja ya Mtendaji Mkuu wa TANROADS nchini, Mhandisi Patrick Mfugale aliyeomba waziri kuliangalia suala hilo la kuchelewa kwa misamaha ya Kodi ya VAT kwa wakandarasi.

Mhandisi Patrick Mfugale amesema kuwa, kumekuwa na tatizo la kuchelewa kuanza kutelezwa kwa miradi mbalimbali ambayo wazabuni wanachelewa kupata nyaraka za kusamehewa Kodi ya VAT.

Amesema kuwa, Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) imekuwa ikitimiza wajibu wake kwa kuwafuatilia wakandarasi hao kwa sababu wanakuwa hawajapata nyaraka za GN za kusamehewa VAT, hivyo kushindwa kuanza kazi.

Mhandisi Mfugale amesema, si kosa la TRA kuwafuatilia wakandarasi,bali wanatimiza matakwa ya kisheria,hivyo amemuomba Waziri wa Fedha kuingilia kati ili nyaraka hizo zipatikane kwa muda muafaka ili wakandarasi watekeleze miradi hiyo kwa wakati.
Mtendaji Mkuu wa TANROADS nchini, Mhandisi Patrick Mfugale akizungumza katika mkutano mkuu wa Baraza la Wafanyakazi wa Tanroads katikati ukumbi wa Magufuli uliopo Kituo cha EPZA Mjini Geita. (Picha na Robert Kalokola/Diramakini).

Mbali na kutangaza kumaliza tatizo la kuchelewa,msamaha wa VAT pia Waziri Mpango ametoa maagizo mbalimbali kwa wakala wa barabara nchini TANROADS.

Miongoni mwa maagizo hayo ni kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kusimamia wakandarasi ili wasitumie misamaha ya kodi ya ongezeko la thamani VAT kwa maslahi yao binafsi.

Agizo jingine ni kuundwa kwa mfumo wa pamoja wa kiutendaji unaohusisha Wizara ya Ujenzi kupitia TANROADS,Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi kupitia Kitengo cha Uthamini pamoja na Wizara ya Fedha Mipango ili kushughulikia masuala ya uthamini na ulipaji wa fidia kwa mali zinazoathiriwa na utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa miundombinu ili kupunguza mlolongo usio na tija.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel ameomba TANROADS kuwajengea uwezo wakandarasi wa ndani ya nchi ili wawe na uwezo wa kutekeleza miradi mikubwa badala ya kutegemea makampuni makubwa kutoka nchi za nje.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel akizungumza katika mkutano mkuu wa Baraza la Wafanyakazi wa Tanroads katika ukumbi wa Magufuli katika kituo cha EPZA Mjini Geita. (Picha na Robert Kalokola/Diramakini).

Amesema kuwa, wakandarasi wa ndani ya nchi wana uwezo mkubwa wa kutekeleza miradi mikubwa huku akitolea mfano wa mkandarasi wa ndani aliyejenga kiwanja cha ndege cha Geita wilayani Chato.

Amesema, mkandarasi huyo amejenga kiwanja hicho kwa viwango vya kimataifa na hakuna tofauti na makampuni kutoka nje ya nchi.
Baadhi ya wafanyakazi wa Tanroads ambao ni wajumbe wa baraza la wafanyakazi waliohudhuria mkutano mkuu (Picha na Robert Kalokola).

Mkutano mkuu wa baraza la wafanyakazi wa Tanroads nchini unafanyika kwa siku mbili kuanzia Desemba 10 hadi 11, mwaka huu katika ukumbi wa Magufuli katika kituo cha EPZA Mjini Geita ukiwa ni mkutano wa 15 tangu kuanza kwa baraza hilo mwaka 2002.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news