Serikali imeutaka Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) wenye
maskani yake jijini Dar es Salaam kuanza mchakato wa haraka kuhakikisha
unahamia Jijini Dodoma, anaripoti Mathias Canal, (WKS) Dar es Salam
Agizo
hilo limetolewa na Waziri wa Katiba na Sheria,Dkt. Mwigulu Nchemba leo Desemba 21, 2020 wakati akizungumza na watumishi wa taasisi hiyo
akiwa katika ziara ya kikazi jijini Dar es salaam.
Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe Dkt. Mwigulu Nchemba akisisitiza jambo wakati akizungumza na watumishi wa Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) akiwa katika ziara ya kikazi jijini Dar es Salaam Desemba 21, 2020.
Sehemu ya watumishi wa Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA), Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na waandishi wa habari wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe Dkt.Mwigulu Nchemba akisisitiza jambo wakati akiwa katika ziara ya kikazi jijini Dar es Salaam Desemba 21, 2020.
Waziri Mwigulu amesema kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
,Mhe Dkt.John Pombe Magufuli ametoa maelekezo ya Serikali kuhamia jijini
Dodoma hivyo taasisi zote zinapaswa kuhamia haraka iwezekanavyo.
“Bahati
nzuri mmeniambia kuwa mna kiwanja jijini Dodoma hivyo safari ya Dodoma
inawahusu ni lazima mhamie Dodoma, zile taasisi zinazochelewa kuhamia
Dodoma itafikia wakati tutafanya uamuzi wa kuziuza mkiwa ndani ya ofisi,"amesema Dkt. Mwigulu.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Geofrey Mizengo Pinda akizungumza wakati akizungumza na watumishi wa Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) wakati alipoandamana na Waziri wa Katiba na Sheria,Dkt. Mwigulu Nchemba katika ziara ya kikazi jijini Dar es Salaam.
Waziri Mwigulu amemuagiza Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa RITA
pamoja na Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA kuhakikisha kuwa wanaweka mkazo
kuhakikisha taasisi hiyo inahamia Dodoma haraka iwezekanavyo.
Ameongeza
kuwa Rais Magufuli ameonyesha mfano kwa kujenga Ikulu ya Chamwino
inayofanana na Ikulu ya jijini Dar es Salaam huku tayari akiwa amehamia
Jijini Dodoma hivyo taasisi hiyo ni muhimu kuhamia Dodoma.
Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA), Bi Emmy Hudson akitoa taarifa ya Wakala mbele ya Waziri na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria mara baada ya kuwasili kwa ajili ya ziara ya kikazi Jijini Dar es salaam.
“Binafsi sitopenda ikifanyika sensa ya Taasisi ambazo
zinastahili kuhamia Dodoma halafu zikutwe bado zipo Jijini Dar es salaam
zikiwemo taasisi za Wizara ya Katiba na Sheria,”amesema.
Kadhalika
ameagiza kuhakikisha kuwa watendaji wa taasisi ya RITA wanatembelea mara
kwa mara Jijini Dodoma katika shughuli za kikazi ili kuendelea kuzoea jiji hilo wakati wanafanya maandalizi ya kuhama.
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Dkt. Mwigulu Nchemba pamoja na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Geofrey Mizengo Pinda wakikagua maktaba ya kumbukumbu za vyeti vya kuzaliwa na vifo wakati walipotembelea ofisi za Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) wakiwa katika ziara ya kikazi jijini Dar es Salaam.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mh.e Geofrey Mizengo
Pinda ameitaka taasisi hiyo kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi ili
kurahisisha utendaji kazi kadhalika kuongeza uwezekano wa kujitangaza
katika vyombo mbalimbali vya habari.
Pinda ameongeza kuwa
serikali imekusudia kuimarisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi hivyo
RITA inapaswa kuongeza urahisi wa upatikanaji wa huduma hususani katika
utoaji wa vitambulisho kwa ngazi ya majimbo.
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Dkt. Mwigulu Nchemba pamoja na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Geofrey Mizengo Pinda wakikagua mitambo ya kuhifadhia kumbukumbu wakati walipotembelea ofisi za Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) wakiwa katika ziara ya kikazi Jijini Dar es salaam tarehe 21 Disemba 2020.
Awali akitoa taarifa ya taasisi hiyo, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) Bi Emmy Hudson amesema kuwa taasisi hiyo ipo katika mpango mkakati wa kuharakisha ufungaji wa mirasi kwa wakati pamoja na kuboresha mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara kwa kuhakikisha sheria ya ufilisi inakamilika na kupitishwa na bunge.
Sambamba na hayo amezitaja changamoto mbalimbali zinazoikumba taasisi hiyo ikiwemo kushindwa kuongeza ada ya utoaji wa vyeti vya kuzaliwa pamoja na upungufu wa watumishi kwani waliopo ni 203 kati ya 361 wanaohitajika.
Tags
Habari