Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Damas D.Ndumbaro (Mb) kwa mamlaka aliyonayo kwa mujibu wa Sheria ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Sura Na. 284, Desemba 19, 2020 amefanya mabadiliko ya Manaibu Makamishna wa Uhifadhi wawili wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kwa lengo la kuboresha utendaji kazi wa taasisi hiyo, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Kwa mujibu wa Mheshimiwa Waziri, katika mabadiliko hayo amemteua Dkt. Christopher D. Timbuka, kuwa Kaimu Naibu Kamishna (Uhifadhi, Utalii na Maendeleo ya Jamii).
Kabla ya uteuzi huo, Dkt. Timbuka alikuwa Kamishna Mwandamizi wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Kanda ya Kusini. Anachukua nafasi ya Bw. Ephraim A. Mwangomo ambaye amerejeshwa TANAPA.
Aidha, Mhe Waziri amemteua Bw. Audax R. Bahweitima, kuwa Kaimu Naibu Kamishna wa Uhifadhi (Huduma za Shirika). Kabla ya uteuzi huo, Bw. Bahweitima alikuwa Mchumi Mkuu katika Idara ya Sera na Mipango, Wizara ya Maliasili na Utalii. Anachukua nafasi ya Bw. Abdallah O. Kiwango ambaye amerejeshwa TANAPA ambapo uteuzi wao unaanza rasmi Desemba 19, 2020.
Tags
Habari