Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Ummy Mwalimu amelitaka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), kuimarisha ofisi zake za kanda na kuwajengea uwezo wafanyakazi ili wamudu kasi ya uwekezaji nchini, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Akizungumza na Menejimenti ya NEMC jijini Dar es Salaam, Waziri Ummy amesema NEMC haipaswi kuwa kikwazo kwa namna yoyote ile kwa wawekezaji.
"Tunahitaji kufanyakazi kwa kasi kubwa ili kukidhi mahitaji ya wawekezaji na hilo litawezekana kama NEMC mtaimarisha ofisi za kanda kwa kuwajengea uwezo wafanyakazi waliopo kwenye ofisi hizo ili kuondoa mrundikano wa mambo hapa makao makuu ya baraza,"amesema.
Amesema, uchumi wa viwanda utafikiwa kwa kuwekwa mazingira mazuri ambayo wawekezaji watavutika na kuja kuwekeza na hilo linawezekana kama taasisi zote zitajipanga kwa kuweka mikakati mizuri.
"NEMC mbali ya kusimamia mazingira lazima pia mhakikishe mnasimamia miradi ya kimkakati ambayo inatekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais Dkt.John Magufuli,"amesema na kuongeza kuwa NEMC haipaswi kuwa kikwazo katika kutekeleza azma ya ujenzi wa uchumi wa viwanda.
Aidha, Waziri Ummy amesema, baraza lifanye pia kazi ya kuwashuri wawekezaji licha ya uwepo wa wataalamuelekezi kwani baadhi yao siyo waaminifu alisama na kufafanua kwamba hao wachache wamekuwa wakirefusha michakato ya upatikanaji wa huduma kwa wawekezaji ikiwemo utoaji wa vibali.
"Tusibaki tu ofisini huku tukiamini kuna wataalamu elekezi ambao wachache kwa maslahi yao wamekuwa wakichelewesha mchakato wa baadhi ya huduma na hivyo kuipa doa NEMC.
"Mnayo nafasi ya kushauri wawekezaji ili waweze kupata wataalamu elekezi ambao wapo makini na kazi zao jambo ambalo litaondoa malalamiko yasiyo na ulazima kwenu,"amesema.
Waziri Ummy amewakumbusha Watanzania umuhimu wa kutunza mazingira kwa faida ya kizazi cha leo na cha baadaye.
"Siku za karibuni kumekuwa na ongezeko kubwa la joto duniani na hii inatokana na uharibifu wa mazingira unaotokana na shughuli za binadamu.Nawakumbusha Watanzania kuyatunza mazingira ili nayo yatutunze,"amesema.
Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt.Samuel Gwamaka amesema watayafanyia kazi mapendekezo yote ya Waziri yanayohusu menejimenti na watumishi.
"Baraza limejipanga kutekeleza na kusimamia miradi yote ya kimkakati kwa ufanisi mkubwa na baada ya maelekezo ya waziri itakuwa rahisi kutekeleza mipango yetu, kwani mingi ya mikakati aliyoelekeza tulikwishaanza kuitekeleza na hata mikakati ambayo bado hatujaanza utekelezaji wake tutaitekeleza kwa maelezo aliyotupa Waziri,"amesema Dkt.Gwamaka.
NEMC ina ofisi za kanda sita katika Kanda ya Kati (Dodoma),Kanda ya Ziwa (Mwanza), Kanda ya Nyanda za Juu Kusini (Mbeya), Kanda ya Mashariki (Dar es Salaam), Kanda ya Kusini (Mtwara) pamoja na Kanda ya Kaskazini (Arusha).
Tags
Habari