Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Benson Ndiege ameivunja Bodi ya Chama Kikuu cha Ushirika cha Milambo Ltd kwa kushindwa kushughulikia kikamilifu suala la wizi wa pembejeo zenye thamani ya sh.milioni 55,426,228, anaripoti Mwandishi Diramakini.Pia Dkt.Ndiege ameiagiza bodi hiyo kurejesha pembejeo zote zilizoibiwa, ameivunja bodi hiyo kwenye kikao kilichofanyika mjini Urambo kwenye Ukumbi wa Milambo Union.Kikao ambacho kimehudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Urambo, Angelina Kwingwa pamoja na wajumbe wa Bodi na Meneja Mkuu wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Milambo.
Mrajis wa Vyama vya Ushirika amewataka wajumbe wa bodi iliyovunjwa kutoa ushirikiano kwa vyombo vya usalama ili waliosababisha au kuhusika katika wizi huo wa pembejeo wajulikane na kuchukuliwa hatua.
Aidha, wajumbe wa bodi iliyovunjwa hawaruhusiwi kugombea uongozi wa bodi katika vyama vyao vya Ushirika vya Msingi na Chama Kikuu (Union).
Mtendaji huyo ameelekeza kuwa mtunza stoo asimamishwe kazi au aondolewe kazini kwa kufuata taratibu za utumishi zinavyoelekeza na amemwagiza Meneja Mkuu wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Milambo, Leak Madel, kuandaa taarifa ya kina kuanzia kipindi cha maombi ya mbolea kutoka kampuni ya Petrobena, kusambazwa kwenye AMCOS, Mikataba iliyotumika, pembejeo zilizopokelewa na utaratibu uliotumika.
Akizungumza katika Kikao hicho, Mkuu wa Wilaya ya Urambo, Angelina Kwingwa amesema kuwa, baada ya kupewa taarifa ya wizi wa pembejeo uliotokea katika Chama Kikuu cha Ushirika cha Milambo alikwenda na Kamati yake ya Ulinzi na Usalama kwenye Ghala la chama hicho ulipotokea wizi na kufanya mahojiano na Wahusika.