Zanzibar yampa kongole Rais Magufuli utekelezaji wa TASAF

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema uamuzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli wa kuutaka Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kufanya kazi maeneo yote ya nchini ni jambo la msingi litakaloleta ustawi zaidi hasa kwa wananchi wa kaya maskini,anaripoti Mwandishi Diramakini.

Amesema, Watanzania walio wengi wanaendelea kushuhudia jinsi Mfuko huo wa Maendeleo ya Jamii Tanzania ulivyokomboa maisha ya wananchi wa kipato cha chini na kwa sasa baadhi wao wameanza kujihakikishia upatikanaji wa mahitaji yao ya msingi.
Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla ameyaeleza hayo wakati akizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania, Ladislaus Mwamanga alipofika ofisini kwake kuelezea Mikakati ya Mfuko huo kwa Awamu ya Tatu ya utekelezaji wake.

Amesema, upo ushahidi wa wazi katika uimarikaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ya jamii akitolea mfano Sekta ya Elimu baada ya kupata msukumo kupitia Mfuko wa TASAF ambapo hata takwimu za idadi ya uandikishaji wa wanafunzi wa elimu ya msingi imepanda sana.

“Ukweli nimefarajika na kukiri kwamba wananchi wengi wa kaya maskini hasa vijijini wamefaidika na matunda ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania,”amesisitiza Makamu wa Pili wa Rais.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema, wakati kipindi cha Pili cha Awamu ya Tatu TASAF kimeshaanza kuonyesha muelekeo mzuri katika utekelezaji wake, ameuhakikishia uongozi huo wa juu wa mfuko huo kwamba ofisi yake kama Msimamizi Mkuu kwa upande wa Zanzibar itaongeza ushirikianozZaidi ili malengo ya mfuko huo kufikia maeneo yote yalete tija.

Mheshimiwa Hemed ameupongeza mfumo mpya wa teknolojia ya sasa ya mtandao katika utoaji fedha utakaotumiwa na mfuko huo katika Awamu ya Tatu Kipindi cha Pili cha TASAF.

Amewataka watendaji wote watakaohusika na uwekelezaji wa miradi ya TASAF wazingatie vyema masuala ya uadilifu katika majukumu watakayopangiwa.

Makamu huyo wa Rais amesisitiza kwamba Zanzibar itaendelea kujitahidi kufanya vizuri zaidi kwenye utekelezaji huo na pale itakapojitokeza changamoto yoyote hatua za haraka zitachukuliwa ili kuleta ufanisi uliokusudiwa.

Mapema Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania(TASAF), Ladislaus Mwamanga alisema jumla ya wana kaya elfu 1,320 Tanzania Bara na zaidi ya 100 upande wa Zanzibar wametosheka na Mradi ya Kaya Maskini ambapo wameamua kujitoa baada ya maisha yao kubadilika.  

Mwamanga amesema, TASAF imekamilisha zoezi la uhakiki kwa wananchi wa kaya maskini ikilenga maisha ya wanajamii wa kaya maskini lazima yabadilike katika kuimarisha uchumi ndani ya kaya hizo.

Amesema, hatua ya kuvijengea uwezo wa taaluma vikundi vya kuweka na kukopa utazingatiwa kwa vile takwimu zinazonyesha kwamba eneo hilo lina mchango mkubwa wa kupunguza umaskini. 

Mwamanga amesisitiza kwamba kwa vile miradi mingi inayoanzishwa kupitia mfuko huo itakuwa endelevu wananchi wanaosimamia miradi hiyo lazima wafanye kazi ya ziada katika kufanikisha uwajibikaji wake.

Mkurugenzi Mkuu huyo wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF) aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na wananchi wake kwa hatua kubwa iliyofikiwa ndani ya miradi ya TASAF na matokeo yake Zanzibar imekuwa mfano katika utekelezaji wake.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news