Mgombea urais na mwanasiasa wa upinzani nchini Uganda, Robert Kyagulanyi (Bobi Wine) ameitisha maandamano ya amani nchini humo kupinga anachodai ni wizi wa kura katika uchaguzi wa hivi karibuni ambao ulimpa ushindi Rais Yoweri Kaguta Museveni.
Bobi Wine akizungumza kupitia ukurasa wake wa Youtube kutoka nyumbani kwake anakozuiliwa na wanajeshi wa Uganda UPDF amewataka wafuasi wake kujitokeza kwa wingi kote nchini na kuandamana kwa amani, bila kuvunja sheria yoyote.
Amesema kwamba, kwa kufanya hivyo, watakuwa wanadai haki yao ya kikatiba.
Pia amesema, hatakubali kunyamazishwa na polisi ambao wamemtaka kusema wazi kwamba hataitisha maandamano.
“Nimesikia polisi wakiniambia kwamba niwaambie watu wangu wasifanye maandamano ndipo waniachilie huru. Hilo sio jukumu langu. Raia wa Uganda wanajua kwamba hawajavunja sheria yoyote,”amesema.
Bobi Wine amesisitiza kwamba alishinda uchaguzi mkuu uliofanyika Januari 14, mwaka huu.
Tume ya Uchaguzi nchini humo ilimtangaza Rais Museveni kuwa mshindi wa uchaguzi huo kwa asilimia 58.64 ya kura zilizopigwa huku Bobi Wine akipata asilimia 34.83.
Bobi Wine amedai kwamba chama chake cha National Unity Platform, kina ushahidi wa kutosha kwamba udanganyifu mkubwa wa kura ulifanyika na kumpa ushindi Rais Museveni.