Bodi ya Maziwa nchini Tanzania (TDB) imekamata tani tatu za maziwa ya unga ya Cowbell yaliyokuwa yanakaribia kuisha muda wa matumizi yakiwa yameongezwa muda wa matumizi zaidi kwa ajili ya kuyauza, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Ukaguzi ukiendelea katika kiwanda hicho kilichopo Keko Chang'ombe katika Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam. (Picha na Diramakini).
Kaimu Msajili wa Bodi hiyo, Noel Byamungu amesema jijini Dar es Salaam kuwa, wamebaini kitendo hicho katika kiwanda cha Kampuni ya Hawai Limited kilichopo Keko Chang'ombe katika Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam wakiwa katika majukumu yao ya ukaguzi na usimamizi wa kuhakikisha wananchi wanapata maziwa bora nchini.
Byamungu amesema, maziwa hayo yalitakiwa kumaliza muda wake wa matumizi mwezi Juni, Agosti na Oktoba, mwaka huu lakini kiwanda hicho kilifanya kitendo cha kufunga upya maziwa hayo katika vifungashio vipya vinavyoonesha mwisho wa matumizi ya maziwa hayo kuendelea kutumika hadi mwezi Agosti mwaka 2022.
Amesema, watendaji wamewaachia Jeshi la Polisi mkoa wa Kipolisi Temeke ambao ni Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, Ahemed Suleiman Mohamed pamoja na Meneja uzalishaji, Ahmed Amanzi kujibu tuhuma zinazowakabili.
Kamishina Msaidizi wa Mkoa Kipolisi Temeke Amon Kakwale amesema tayari wanawashikilia watendaji wa kampuni hiyo kwa hatua za kichunguzi zaidi kabla ya kufikishwa katika mamlaka za kisheria.