Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya,
amezungumzia umuhimu wa Chuo cha Reli Tabora kuongeza kozi za reli
zinazoendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia ili kuzalisha
wataalam wengi wa reli wataohudumu katika miradi mikubwa ya reli
inayoendelea kujengwa nchini, anaripoti Mwandishi Diramakini.


Ameyasema hayo mkoani Tabora, wakati alipokagua chuo hicho na
karakana ya reli ambapo pamoja na mambo mengine amesisitiza kuwepo kwa
mikakati madhubuti ya kulisaidia Taifa katika usimamizi na ujenzi wa
miundombinu ya reli mpya ya kisasa na ile ya reli ya kati inayoendelea
kuboreshwa.
“Huu ni wakati wa Shirika la Reli nchini ( TRC),
pamoja na Taasisi zake kuja na mtazamo mpya utakaowezesha juhudi za
Serikali za kufufua Sekta ya Reli kufanikiwa,”amesema Mhandisi
Kasekenya.

Aidha ameitaka TRC kuhakikisha inaboresha mifumo ya ukusanyaji wa mapato
ili fedha inayopatikana iwezeshe kuboresha huduma zake na kupata faida.
Kasekenya ameeleza lengo la Serikali ni kuhakikisha mizigo mizito inasafirishwa kwa reli nchini kote ili kulinda barabara.

Aidha, Naibu Waziri Kasekenya amesisitiza umuhimu wa watumishi wa reli
waliopo kazini kupata mafunzo ya mara kwa mara ili kuondoa kufanya kazi
kwa mazoea.
Amewataka watumishi wa reli kuwa waadilifu na kuacha
vitendo vyote vya rushwa na uhujumu ili kuiwezesha reli kuwa salama
wakati wote.

“Hakikisheni huduma za reli zinakuwa za haraka na uhakika, punguzeni
urasimu kwa wafanyabiashara”, amesisitiza Mhandisi Kasekenya.
Naye
Mkuu wa Chuo cha Reli Tabora, Bw. Damas Mwajanga, amemhakikishia Naibu
Waziri huyo kuwa chuo hicho tayari kimepata ithibati ya NACTE na hivyo
kimeanza kuongeza udahili wa wanafunzi ili kuweza kuhudumia soko la reli
katika Ukanda wa Afrika Mashariki.

Zaidi ya wanafunzi 200 wa ngazi za cheti na diploma wanasomea mafunzo ya reli katika kampasi zake za Tabora na Morogoro.
Chuo cha Reli cha Tabora kilianzishwa mwaka 1947 ikiwa ni kituo kikuu cha kuhudumia reli katika Ukanda wa Afrika Mashariki na kimekuwa kikitoa mafunzo ya ufundi wa treni, udereva wa treni, umeme, watalaam wa mawasiliano ya treni na wakaguzi wa mabehewa.