Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Allan Kijazi
amewataka watumishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii kuwa na utaratibu
wa kufanya mazoezi ili kuimarisha afya zao na kujenga mshikamano na
upendo katika maeneo yao ya kazi,anaripoti Happiness Shayo.
Washiriki wa mchezo wa mbio za magunia wakichuana wakati wa bonanza la watumishi lililoandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii lililofanyika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma leo.
Dkt.
Kijazi ametoa wito huo wakati wa bonanza la watumishi lililoandaliwa na
Wizara ya Maliasili na Utalii lililofanyika leo katika uwanja wa
Jamhuri jijini Dodoma.



"Mazoezi iwe ni sehemu ya maisha yetu na pia iwe ni sehemu ya kazi zetu," amesisitiza Dkt. Kijazi.
Ameongeza
kuwa, Wizara yake itajipanga kuhakikisha kila mtumishi anashiriki
katika kufanya mazoezi na pia kila mtumishi anashiriki kwenye mabonanza
na amewataka watumishi kuendelea kuhamasishana ili ushiriki uzidi
kuongezeka katika matamasha yanayokuja.
Dkt. Kijazi amefafanua
kuwa Wizara itaweka utaratibu wa kuwatambua washiriki bora wa kila mwaka
wanaofanya mazoezi na wanaoshiriki kikamilifu katika matamasha kama
hayo na kuwapa zawadi maalumu.


Pia, amesema kuwa, Wizara itahakikisha ushiriki wa watumishi katika
matamasha hayo hauishii Dodoma bali utaendelea kwenye matamasha mengine
yanayofanyika nchini, kama Kilimanjaro Marathon, Ngorongoro Marathon na
Serengeti Marathon.
"Watumishi watakaofanya vizuri tutawadhamini ili waiwakilishe Wizara kwenye Marathon hizo,"amesema.
Naibu
Katibu Mkuu, Dkt. Kijazi amewapongeza washiriki wote walioweza kukimbia
mbio za kilomita tano kwa kupata medali na kuwataka ambao wameshindwa
wajitahidi kipindi kijacho wamalize mbio hizo.


"Ni imani yangu kuwa bonanza linalokuja wote tutamaliza mbio za kilomita tano, cha msingi tuendelee kufanya mazoezi ,tusisubiri hadi matamasha haya yafike ndo tufanye mazoezi,"amesema Dkt. Kijazi amesema.
Dkt. Kijazi amewashukuru Dodoma Fitness Club na Muungano Fitness Club kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii katika kufanikisha bonanza hilo na kusema kuwa uwepo wao ni chachu kwa Wizara katika kuimarisha mabonanza.
Naye, Mwenyekiti wa Jogging Clubs Dodoma, Bw.Mugisha Mujungu ameahidi kuendelea kushirikiana na Wizara kila itakapohitaji ushirikiano katika kufanya mazoezi na kuwataka watumishi wa serikali kujiunga na Jogging Clubs ili kuimarisha afya zao.
Bonanza hilo limehudhuriwa na watumishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii na washiriki kutoka Dodoma Fitness Club na Muungano Fitness Club za Dodoma.
Tags
Michezo